1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Janga

Kwanini ajali za boti hutokea mara kwa mara Afrika?

13 Oktoba 2025

Zaidi ya watu 148 wamepoteza maisha katika ajali za boti kwenye mto Kongo tangu mwezi Julai mwaka 2024, licha ya serikali kuwaonya wamiliki wa vyombo vya usafiri wa majini kutovunja sheria ikiwemo kujaza kupita kiasi.

https://p.dw.com/p/51uFX
Ajali za boti hutokea mara kwa mara Afrika
Kila siku boti kubwa za abiria husafiri kwenye Mto Kongo, zikiwa zimejaa kupita kiasi bila kuzingatia kanuni za usalama.Picha: IANS

Wakazi wa Mbandaka, mji wa bandari kaskazini magharibi mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, wanakabiliwa na uhaba mkuwa wa usafiri si kwa njia ya barabara wala nchi kavu. Mvua zinazonyesha takriban mwaka mzima husababisha barabara nyingi kutopitika , hivyo wakazi hao hulazimika kutumia boti duni kusafiri kwenda katika shughuli zao za kila siku.

Kila siku, boti kubwa za abiria husafiri kwenye Mto Kongo, mto wa pili kwa urefu barani Afrika na wenye kina kirefu zaidi duniani, boti hizo huwa zimejaa kupita kiasi na bila kuzingatia kanuni za usalama. Mwalimu Nestor Mokwanguba anansema hawana chaguo lingine linapokuja suala la usafirishaji katika eneo  hilo.

"Tunajitia kwenye hatari kusafiri katika mazingira kama haya kwa sababu hakuna njia mbadala kama barabara zinazoweza kutufikisha hapa Mbandaka, njia pekee tuliyonayo ni ya majini, zaidi ya hayo kwenye mto huu boti ni chache na zilizopo sio salama hata hivyo tunalazimika kutumia boti hizi chakavu sababu hatuna chaguo lingine."

Kulingana na shirika la habari la AFP, tangu Julai 2024, angalau watu 148 wamefariki katika ajali za boti kwenye mto huo, huku kadhaa bado hawajulikani walipo. Idadi hii huenda ikawa ni kubwa zaidi, kutokana na kile kinachosemwa ni agharabu kuwepo kwa orodha rasmi za abiria.

Katika makaburi ya Mbandaka, Florence, mama wa Munzanza, alipiga magoti kando ya kaburi la mwanawe huku machozi yakimtiririka, uhai wa kijana wake ukikatizwa na ajali ya boti anainyooshea kidole mamlaka kwa kutochukuwa hatua dhidi ya wahusika.

"Alikwenda safari ya kikazi, wakati wa kurudi boti yao ilipinduka, mwanangu alikuwa ni miongoni mwa waliokufa, tangu wakati huo serikali haijafanya lolote, hawana wanalojali kabisa. Katika nchi nyingine kungelikuwa na uchunguzi na kesi mahakamani ili kuwawajibisha waliohusika, lakini hapa kwetu hakuna chochote."

Onyo latolewa kuhusu usafirishaji abiria na mali usiozingatia kanuni na shaeria

Meya wa Mbandaka, amefanya ziara kadhaa katika bandari katika mto Kongo na kuoonya juu ya usafirishaji abiria na mali usiozingatia kanuni na shaeria, wamiliki wa vyombo hivyo wakipuuzia maagizo ya kutoa vifaa vya kujiokoa wakati wa majanga na kupunguza mizigo. Clovis Eng'ombe ni makamu wa rais wa chama cha wamiliki wa meli anakiri juu ya kadhia hiyo, lakini ipo changamoto kutoka kwa mamalaka.

"Ndio tunapakia abiria na mizigo kupita kiasihiyo ni kawaida. Ninapotumia dola elfu kumi na tano hadi elfu thelathini za Marekani kununua boti na kuiweka kazini, lengo kuu ni kupata faida. Kumbuka kuna ushuru wa mazingira, mabaharia wanataka kuonyeshwa ripoti za usalama wa vyombo vyetu na malipo mengine chungu nzima na usipolipa wanaizuia boti kusafiri."

Kwa mujibu wa serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kupitia wizara ya uchukuzi ina kilometa 58,000 za barabara, lakini chini ya asilimia 5 sawa na takriban kilometa 2,700 ndizo zilizokamilika kwa kiwango cha lami. Mnamo mwaka 2019 katika awamu ya kwanza ya muhula wake rais Felix Tshisekedi alitangaza kuboresha miundombinu kwa kuinganisha nchi kwa njia ya barabara. Hata hivyo, ukosefu wa fedha, ufisadi na changamoto za usimamizi umefanya maendeleo kwa mwendo wa kinyonga.

Licha ya mpango huo uliokwama, wananchi hawana budi kuendelea kutumia usafiri wa majini ambao hauna uhakika wa usalama wao, huku vifo vikiendelea kushuhudiwakutokana na ajali zinazoweza kuzuilika.