Kwa nini Watanzania wanahesabiwa | Matukio ya Afrika | DW | 24.08.2012
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Kwa nini Watanzania wanahesabiwa

Kwa mara nyingine wakati umefika kwa Watanzania wajitokeze kuhesabiwa. Zoezi hili hufanyika kila baada ya miaka kumi.

kikwete.jpg Tanzanian President Jakaya Mrisho Kikwete, left, and Japanese Prime Minister Shinzo Abe shake hands upon meeting at Abe's official residence in Tokyo Wednesday, Nov. 1, 2006. Kikwete is on a five-day official visit to Japan. (AP Photo/Toshiyuki Aizawa, POOL)

Rais wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete

Safari hii ambapo siku ya sensa inakaribia, baadhi ya watu hawatulii na kuwapa fursa wale watakaowahesabu kufanya kazi kwa urahisi baada ya kupewa mafunzo na mazoezi mengi. Kwa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania, serikali inafanya juhudi za ziada kumshawishi kila mtu atakayekuwepo nchini usiku wa kuamkia 26 Agosti 2012 ajitokeze kuhesabiwa.

Cha kustaajabisha ni kwamba baadhi ya watu wanaopinga kufanyika kwa sensa wanatumia njia ya mawasiliano ambayo imekuwa rahisi, yaani simu za mkononi, kueneza ujumbe wa kuzuia juhudi za serikali. Katika baadhi ya taarifa zao wanadai kwamba kuhesabu watu ni shughuli ambayo haiendani na imani yao. Wanaeleza pia hofu yao kwamba matokeo ya sensa yatatumika kuwatenga baadhi ya watu katika jamii. Jambo la aina hiyo halijawahi kutokea Tanzania

Kwa nini basi litokee wakati huu?

Sababu ni kwamba bado wako watu wengi ambao hawana habari au elimu ya kutosha juu ya wajibu wao kama raia, hata kama wanazingatia imani zao kwa uangalifu sana. Kwa mfano, wakati wa maafa kama serikali itahitaji hesabu za watu ili wapatiwe msaada, hakuna hata mmoja atapenda jamaa zake wafichwe na kukosa msaada huo.

Hoja za kupinga sensa zimesikika zaidi kutoka kwa baadhi ya waumini wa dini ya Kiislamu lakini wasomi Waislamu wanasema upinzani wa sensa ni potofu. “Mimi ni Mwislamu, lakini nawasisitizia waumini wenzangu kutoa ushirikiano kufanikisha zoezi hili ambalo litasaidia kufanikisha adhma ya maendeleo yetu … itatuwezesha pia kupanga namna ya kuwasaidia wananchi wetu baada ya kujua maisha yao halisi,”amesema Bi. Mwantumu Mahiza, Mkuu wa Mkoa wa Pwani.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Bwana Said Meck Sadiki ametoa onyo kali akisema kwamba serikali itatumia mbinu zake zote kuwatia nguvuni watu wanaotaka kuvuruga sensa, hasa wale wanaopita mitaani usiku na kubandika matangazo yanayowashawishi watu kugomea sensa.

“Tutahakikisha tunawanyima nafasi ya kuwasikiliza watu wa aina hii kwa kuwa ni dhahiri wanaonesha kutokuwa na ufahamu juu ya kile wanachokizungumza na zaidi faida ya sensa kwa taifa hili,” alisema Bwana Sadiki wakati wa Futari iliyowashirikisha viongozi mbalimbali wa serikali na vyama vya siasa katika viwanja vya manisapaa ya Kinondoni.

Takwimu ni muhimu

Takwimu zinaonesha uchumi wa Tanzania haukuwa katika hali mbaya sana katika miaka ya karibuni, lakini kupanda kwa bei za vyakula, idadi ya watu wasio na ajira, rushwa na ugumu wa maisha kwa jumla vimechangia kuongeza idadi ya watu maskini mijini na vijijini.

Hii ina maana kwamba idadi ya watu wanaoweza kujikimu kwa kiasi cha dola 1.25 kwa siku, kiwango kinachokubalika kama daraja la umaskini duniani, haikupungua, na nchi hii inaonekana itashindwa kufikia lengo la Umoja wa Mataifa la kupunguza umasikini angalau kwa nusu ya idadi ya watu wake wote ifikapo mwaka 2015.

Matokeo ya mipango ya maedneelo ya jamii ambayo wanasiasa hudai mara kwa mara kuwa imekuwa ya mafanikio, hasa katika sekta za elimu na afya, bado yako mbali sana yakilinganishwa na matarajio ya wananchi wengi wa Tanzania. Ukweli ni kwamba matokeo hayo hayaonekani katika maeneo ya watu masikini.

Katika hali hiyo si ajabu kuona kuwa masikini umuhimu wa wajibu wa kiraia kushiriki katika zoezi kama vile la kupiga kura, mbali ya hilo la la sensa ambayo ni ya msingi katika kupanga uwakilishi wao katika uongozi wa nchi na kupanga maendeleo kwa jumla. Kwao, ukusanyaji na uchambuzi wa takwimu zinazohusu maisha yao, nyumba wanamoishi, jinsia zao, viwango vya elimu yao, umri, ulemavu na kama wameoa au kuolewa ni kuingilia maisha yao binafsi.

Hawatambui jinsi sensa inavyowahusisha na serikali yao wakati takwimu zinazokusanywa ni chanzo cha maana sana cha taarifa za watafiti na wataalamu wa mipango ya maendeleo. Chini ya Sheria ya Takwimu ya 2002, Ofisi ya Taifa ya Takwimu imepewa madaraka kukusanya taarifa maalum kuhusu idadi ya watu wa Tanzania na kila mkazi wa nchi anatakiwa kutoa maelezo kama inavyotakiwa kutimiza azma ya sensa.

Mbali na hayo, sheria hii ambayo inatumika Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar (Visiwani) kuhusu sensa ya watu na makazi, inaitaka Ofisi ya Takwimu kuhakikisha usalama na usiri kuhusu taarifa zote inazokusanya.

Sensa itatoa sura mpya

Sensa ya kwanza ilifanyika Tanzania, wakati huo ikiwa koloni la Wajerumani la Afrika Mashariki mwaka 1910. Baada ya uhuru mwaka 1961 zimefanyika sensa nyingine nne mwaka 1967, 1978 na 1988. Sensa ya mwisho ya Agosti 2002 ilionesha kuwa Tanzania ilikuwa na idadi ya watu 34,443,603.

Kila sensa kwa kawaida hutoa sura tofauti. Dunia sasa inatarajia sensa ya mwezi huu itatoa taswira yenye kuonesha mambo mbalimbali na kwa hali halisi hasa kwa sababu inafanyika miaka 14 baada ya hesabu iliyopita.

Angalau itatoa sura ya mabadiliko ya demografia na jinsi watu wanavyohama kwenda mahali wanapopenda zaidi au kuna vivutio vilivyowaelekeza huko, sababu za kuhama kwao na jinsi ya kuboresha masuala ya ulipaji kodi, elimu, jinsia, uzalishaji wa chakula, nafasi za kiuchumi pamoja na uendelezaji wa miji na viwanda.

Sensa zote Tanzania huwa ni zoezi la gharama kubwa, lakini kama litahakikiwa vyema matokeo yake yanaweza kusukuma maendeleo ya nchi hii mbele zaidi.

Mwandishi: Anaclet Rwegayura

Mhariri: Mohammed Abdulrahman