Kwa nini UN imeshindwa kulinda amani Afrika? | Matukio ya Afrika | DW | 04.06.2021
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Kwa nini UN imeshindwa kulinda amani Afrika?

Barani Afrika ujumbe wa kijeshi unaopelekwa kwenye maeneo ya mizoz umeshindwa kumaliza machafuko katika maeneo tete zaidi barani humo. Kwa pamoja maslahi ya ndani na nje pia yanachangia pakubwa kushindwa huko.

Ujumbe wa kijeshi kwa jina la Umoja wa mataifa umekuwa ukipelekwa barani Afrika kukabiliana na mizozo ya vita. Hata hivyo licha ya kuwa na silaha kali ikilinganishwa na zile za makundi ya wanamgambo kote barani humo, vikosi hivyo vya jeshi vya Umoja huo vilishindwa na vinaendelea kushindwa  vibaya kwenye utekelezaji wa majukumu yao. 

Kwenye mataifa kama Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Sudan Kusini, Mali na Jamhuri ya Afrika ya Kati, wanajeshi wa kulinda amani wamejikuta wakipambana na mazingira tofauti ya kisiasa na kitamaduni ambayo mara nyingi hawayajui. Kwa mfano mwaka 1999 kilianzishwa kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa nchini Congo, MONUSCO ambacho kimsingi kilitakiwa kuyasambaratisha makundi ya wanamgambo, kupunguza kitisho dhidi ya mamlaka ya serikali na kurejesha amani.

Lakini hadi leo, Kivu Kusini na Kaskazini bado kuna ukiukwaji wa sheria na makundi mengi ya wanamgambo yanaendelea kuwaua raia, kuwabaka wanawake na wasichana na kuwajeruhi watu wasiokuwa na hatia.

Phil Clark wa chuo kikuu cha SOAS kilichoko London, Uingereza ameiambia DW kwamba MONUSCO imekuwa ikijifunza taratibu mno hadi kung'amua namna ya kulinda amani nchini Congo.  Amesema wakati kikipambana kuhakikisha kinaimarisha mahusiano na serikali ya Kishansa, badala yake kimejikuta kikijifungamanisha kwa tahadhari na jeshi la Congo hata katika wakati ambapo jeshi hilo lilifanya mauaji ya kiholela dhidi ya raia.

Mahusiano kama hayo, amesema Clark, yamechochea umwagikaji mkubwa wa damu miongoni mwa wakaazi ambao hawaioni MONUSCO kama mtetezi katika mazingira tete. Mwezi Aprili, mamia ya vijana waliandamana katika miji ya Beni na Goma wakitaka kuondolewa kwa wanajeshi hao kwa kuwa wameshindwa kurejesha amani.

DR Kongo UN-Soldaten in Djugu-Territorium | Ituri-Provinz nach Unruhen

Wanajeshi wa MONUSCO wakiwa kwenye harakati zake nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Giza nene linalohusiana na madai ya kingono

Clark amesema kumekuwepo pia na madai ya unyanyasaji wa kingono dhidi ya wanajeshi kutoka Bangladesh na Afrika Kusini waliokuwa Kivu Kusini na Kaskazini, na kuibua wasiwasi mkubwa kwa wakazi. Kulingana na Umoja wa Mataifa, jumla ya visa 387 vya unyanyasaji wa kingono viliripotiwa katika mifumo ya Umoja huo mwaka 2020.

Mmiliki wa kampeni inayolenga kumaliza visa vya safishasafisha ya kikabila na unyanyasaji wa kingono unaofanywa na wanajeshi inayoitwa Code Blue Paula Donovan ameiambia DW kwamba pamoja na madai hayo, lakini hawawajibishwi. Amesema hiyo inapeleka ujumbe kwa kila mmoja kwamba visa hivyo vinakubalika.

Mkono wa mataifa ya nje.

Makampuni mengi ya uchimbaji ya kimataifa yanaushinikiza Umoja wa Mataifa kuongeza muda wa MONUSCO na kuna uwezekano kwamba hawataondoka hivi karibuni, hatua inayoibua mashaka kwa wafuatiliaji wa mzozo nchini humo. 

Maslahi ya nje pia yanaonekana huko Jamhuri ya Afrika ya Kati. Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo MINUSCA ulipelekwa kuilinda serikali katika mji mkuu Bangui dhidi ya waasi wanaotishia kuipindua. Lakini tangu mwaka 2018, Urusi kwa uwazi kabisa iliiunga mkono serikali ya rais wa sasa Faustin Touadera inayodhibiti kiasi theluthi moja tu ya taifa hilo. Na sasa makampuni ya Urusi yamefanikiwa kuingia kwenye migodi iliyo chini ya udhibiti wa serikali.

Hata hivyo, wataalamu wa Umoja wa Mataifa mwezi Machi walielezea wasiwasi kuhusiana na madai ya ukiukwaji mkubwa wa haki za binaadamu unaofanywa na vikosi ya Urusi. Madai hayo ni pamoja na watu kunyongwa holela, kuteswa, unyanyasaji wa kijinsia, ukatili, unyama na udhalilishaji, na yaliungwa mkono pia na serikali.

Mali I Protest in Bamako

Wakazi nchini Mali wakiwa na mabango yanayoshinikiza wanajeshi wa Umoja wa Mataifa kuondoka nchini humo.

MINUSMA inaeleka wapi baada ya mapinduzi ya Mali?

Licha ya uwepo wa wanajeshi wa nje nchini Mali hali ya kisiasa kaskazini mwa nchi hiyo ambako makundi ya Kiislamu yanaendeleza kampeni zake bado ni tete. Kuna takriban wanajeshi 5,000 waliopo kwenye eneo la Sahel kukabiliana na wakundi ya jihadi na wengine wachache kutoka Ujerumani, chini ya ujumbe wa umoja wa Mataifa, MINUSMA unaowafunza wanajeshi wa Mali.

Wasiwasi mkubwa kuhusu ulinzi wa amani barani Afrika ni kwamba bado haujaimarika tangu ulipoanza kuwepo miaka 25 iliyopita na badala yake umeonekana kugubikwa na maslahi kuliko kulinda wakazi. Hadi pale mfumo mzima wa ulinzi wa amani utakapofanyiwa mageuzi, maeneo tete ya Afrika yataendelea kuomba dua ya salama kutokana na vitisho vya wanamgambo na makundi mengine yenye mahusiano nayo.

 LINK: http://www.dw.com/a-57767805