Mali: Mzozo wa Tuareg wazuka tena | NRS-Import | DW | 20.08.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

NRS-Import

Mali: Mzozo wa Tuareg wazuka tena

Mzozo wa Watuareg nchini Mali umeanza kuchipuka tena. Kumetokea makabiliano kati ya makundi yanayohasimiana ya Watuareg ambayo yameuvunja mkataba wa amani uliosainiwa wiki kadhaa zilizopita.

Machafuko kaskazini mwa Mali yanaonekana hayana kikomo. Kufuatia mashambulizi ya wanamgambo wa kiislamu siku kadhaa zilizopita yaliyowaua wanajeshi kadhaa wa Mali na kutekwa nyara kwa watu wengi katika hoteli moja, inaonekana pia mkataba wa amani kati ya makundi ya Watuareg yanayohasimiana umevunjika.

Katika eneo la Kidal kulitokea makabiliano makali kati ya kundi la Watuareg la Imghad na wafuasi wa kundi la Gatia na kundi lengine la vuguvugu la Azawad, CMA. Takriban watu 20 waliuawa katika mapambano hayo. Kila upande unaulaumu mwingine kwa kusababisha mapigano hayo.

Serikali ya Mali imeyalaani machafuko ya hivi punde na inasubiri matokeo ya uchunguzi unaofanywa na tume ya Umoja wa Mataifa. Waziri anayehusika na Maridhiano Zahabi Ould Sidi Mohamed haoni mchakato wa amani uko hatarini kutokana na mapigano hayo. "Matukio kama haya ya bahati mbaya hutokea. Hatupaswi kuyatilia maanani sana. Mchakato wa kutafuta amani unatakiwa uendelee."

Mkutano kuhusu amani uliokuwa ufanyike Jumatano wiki hii katika mji mkuu wa Niger, Niamey, umeahirishwa kwa mujibu wa shirika la habari la AFP kutokana na machafuko ya Jumatatu wiki hii.

Tume ya Umoja wa Mataifa nchini humo MINUSMA, iliyaeleza mapigano hayo kama ukiukaji mkubwa wa mkataba wa amani wa hivi majuzi.

Mali - Rebellgruppe CMA

Wajumbe wa kundi la CMA wakati wa kusainiwa mkataba wa amani Bamako

Baada ya duru kadhaa za mazungumzo kufeli, serikali ya Mali, wapatanishi wa kimataifa na makundi yenye silaha yalisaini mkataba wa amani Mei 15 mwaka huu katika mji mkuu Bamako. Hatimaye mnamo Juni 20 kundi la CMA ambalo lilikuwa lipinga nalo likayasaini makubaliano hayo.

Mkataba huo kwa upande mmoja unaonekana kuitambua serikali ya mjini Bamako na kwa upande mwingine unatoa haki zaidi kwa eneo la kaskazini la taifa hilo. Unazungumzia pande husika katika mgogoro huo kupewa baadhi ya maeneo - ingawa zimejihami na silaha - lakini zisiruhusiwe kuondoka maeneo hayo.

Mizizi ya kihistoria, miungano mipya

Kundi la Gatia linachukuliwa kama kundi la Watuareg wanaoiunga mkono serikali. Hata hivyo licha ya kuwa mshirika wa serikali kundi hilo hufuata ajenda yake katika eneo linalolidhibiti, mbali na maeneo yanayodhibitiwa na jeshi la Mali. Ndio kundi hili likajikuta katika mapigano kwenye eneo linalodhibitiwa na kundi la CMA. Sababu mojawapo pengine ni biashara haramu ya dawa za kulevya, ambayo ni chanzo muhimu cha kipato cha kundi hilo. Barabara nyingi zimekuwa hazipitiki wakati wa msimu wa sasa wa mvua. Anayeweza kuzidhibiti barabara zinazopitika, anadhibiti pia biashara hiyo.

MINUSMA Soldaten UN Mission Mali

Wanajeshi wa tume ya MINUSMA

Mzozo kati ya makundi yote mawili ya Watuareg umekuwepo kwa miongo kadhaa, amesema Georg Klute, profesa wa Ethnolojia, sayansi ya makabila na mahusiano kati ya binaadamu, katika chuo kikuu cha Bayreuth nchini Ujerumani. Majina ya makundi na miungano yalikuwa mengine - zamani kiongozi wa sasa wa kundi la Gatia alikuwa akipigana na serikali.

Ukanda maalumu wa usalama

Umoja wa Mataifa umetenga eneo maalumu la usalama nchini Mali. Kuanzia Jumanne asubuhi hakuna mfuasi yeyote wa waasi anayeruhusiwa kutembea katika eneo la kilometa 20 kuuzunguka mji wa Kidal. Tume ya MINUSMA itamchukulia hatua mtu yeyote atakayevunja amri hiyo. Profesa Klute ambaye aliishi mjini Kidal kwa muda na kuwa maingiliano na wakaazi, aliipongeza hatua hiyo akisema, "Ilikuwa hatua maufaka, kutuma ujumbe wa wazi kwa kundi Gatia: Mpaka hapa tu na hakuna kuvuka."

Wakati wa vita vya Mali kuanzia mwaka 2012 waasi wa Tuareg wa kundi la CMA, wanaopigania taifa huru kwa jina la Azawad kaskazini mwa Mali, waliungana kwa miezi kadhaa na wanamgambo wa kiislamu wa kundi la Ansar Dine na kuliteka eneo kubwa la kaskazini. Harakati ya kijeshi ya Ufaransa ya mwaka 2013 ndiyo iliyowazuia.

Mwandishi: Fischer, Hilke

Tafsiri:Josephat Charo

Mhariri:Daniel Gakuba

Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com