Kura ya maoni Crimea | Matukio ya Kisiasa | DW | 16.03.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Kura ya maoni Crimea

Wakaazi wa Crimea wamepiga kura Jumapili (16.03.2014) kuamuwa iwapo ijienguwe kutoka Ukraine na ijiunge na Urusi wakati serikali ya Ukraine ikiishutumu Urusi kwa kuimarisha vikosi vyake kwenye rasi hiyo.

Mwanamke akijiandaa kutumbukiza kura yake katika kituo cha kupigia kura cha Simferopol , Crimea(16.03.2014)

Mwanamke akijiandaa kutumbukiza kura yake katika kituo cha kupigia kura cha Simferopol, Crimea(16.03.2014)

Kutokana na kukumbwa na mzozo unaokumbushia enzi ya Vita Baridi kaimu waziri wa ulinzi wa Ukraine Ihor Tenyuk amesema idadi ya wanajeshi wa Urusi huko Crimea imeongezeka maradufu kupindukia kiwango kilichokubaliwa na nchi hizo mbili na kwamba vikosi vya Ukraine vinachukuwa hatua zinazofaa mpakani na Urusi.

Tenyuk amepuzilia mbali dokezo kwamba Ukraine ikiwa dhaifu kijeshi na kiuchumi inaweza kusalimu amri mbele ya nguvu za Urusi.

Ameliambia shirika la habari la interfax kwamba maamuzi yatachukuliwa kwa kuendana na hali ya mambo na amesisitiza kwamba hiyo ni ardhi yao na katu hawatoiachia.

Kura ni batili

Vitaly Churkin balozi wa Urusi katika Umoja wa Mataifa akizuwiya kwa kura ya turufu rasimu ya kulaani kura ya maoni ya Crimea, New York(15.03.2014).

Vitaly Churkin balozi wa Urusi katika Umoja wa Mataifa akizuwiya kwa kura ya turufu rasimu ya kulaani kura ya maoni ya Crimea, New York(15.03.2014).

Mataifa ya magharibi yanasema kura hiyo ambayo yumkini ikaunga mkono kuungana na Urusi kwa mkoa huo wenye idadi kubwa ya wakaazi wenye kuzungumza Kirusi ni batili na inafanyika chini ya mtutu wa bunduki.

Katika Umoja wa Mataifa nchi wanachama 13 wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa zimepiga kura kuunga mkono rasimu ya azimio lenye kusema matokeo hayo hayapaswi kutambuliwa kimataifa lakini Urusi ilitumia uwezo wake wa kura ya turufu kulipinga azimio hilo wakati China haikupiga kura. Waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov amepinga shutuma za mataifa ya magharibi na amemwambia waziri mwenzake wa Marekani John Kerry kwamba kura hiyo ya maoni inafanyika kwa mujibu wa sheria ya kimataifa.Mataifa ya magharibi na serikali ya Ukraine zote zimeshindwa kuzuwiya kufanyika kwa kura hiyo.

Waziri Mkuu Sergei Aksyonov wa jimbo la Crimea akiondoka kituo cha kupigia kura baada ya kupiga kura yake. (16.03.2014)

Waziri Mkuu Sergei Aksyonov wa jimbo la Crimea akiondoka kituo cha kupigia kura baada ya kupiga kura yake. (16.03.2014)

Katika kituo kimoja cha kupiga kura kwenye mji mkuu wa Crimea wa Simferopol watu kadhaa walikuwa katika misururu ya kupiga kura mapema leo asubuhi.

Svetlana Vasilyeva muuguzi wa wa wanyama ambaye ana umri wa miaka 27 amekaririwa akisema "Nimeipigia kura Urusi. Hiki ndio tulichokuwa tukisubiri. Sisi ni familia moja na tunataka kuishi na ndugu zetu."

Vasilyeva amesema wanataka kuachana na Ukraine kwa sababu Waukraine wamewaambia kuwa wao ni watu wa daraja la chini,jambo linalowafanya wajiulize vipi waendelee kubakia katika nchi hiyo?

Wasi wasi watu wenye asili ya Kirusi

Kura zikiwa kwenye kisanduku cha wazi cha kura cha kioo Crimea. (16.03.2014)

Kura zikiwa kwenye kisanduku cha wazi cha kura cha kioo Crimea. (16.03.2014)

Kuangushwa mwezi uliopita kwa Rais Viktor Yanukovich aliekuwa akiungwa mkono na Urusi kufuatia maandamano yaliyosababisha maafa katika mji mkuu wa Kiev, kumezusha hofu miongoni mwa baadhi ya wenyeji wa nchi hiyo wenye kuzungumza Kirusi.

Urusi imesema ina haki ya kubakisha vikosi vyake katika rasi ya Bahari Nyeusi kwenye bandari ya Sevastopol chini ya mkataba uliosainiwa baada ya Ukraine kujipatia uhuru wake kufuatia kusambaratika kwa Muungano wa Kisovieti hapo mwaka 1991.

Waziri wa Ulinzi wa Ukraine ameishutumu Urusi kwa kuweka wanajeshi kupindukia kiwango cha wanajeshi 12,500 kilichokubaliwa kwa mwaka 2014 Hivi sasa wanajeshi hao wanatajwa kufikia 22,000.

Wakaazi wengi wa Crimea wanatumai kuungana kwao na Urusi kutawapatia mishahara mizuri na kuwafanya kuwa raia wa nchi yenye uwezo wa kujititimua kwenye jukwaa la kimataifa.Lakini wengine wanaiona kura hiyo ya maoni kuwa ni unyakuaji wa ardhi unaofanywa na Urusi kutoka Ukraine ambao viongozi wake wanataka kuielekeza nchi hiyo kwenye Umoja wa Ulaya na kuepuka kuyumbishwa na Urusi.

Watu wa jamii ya Tatar na Waislamu wa madhehebu ya Sunni ambao ni asilimia 12 ya wakaazi wa Crimea wanasema wanasusia kura hiyo ya maoni licha ya ahadi kutoka maafisa wa ya serikali ya mkoa huo kuwapa msaada wa kifedha na haki za kumiliki ardhi.

Mwanajeshi anayeaminika kuwa wa Urusi akilinda kwenye kambi ya kijeshi ya Ukraine karibu na mji wa Simferopol ,Crimea.

Mwanajeshi anayeaminika kuwa wa Urusi akilinda kwenye kambi ya kijeshi ya Ukraine karibu na mji wa Simferopol ,Crimea.

Rais Vladimir Putin wa Urusi ameutetea msimamo wake kwa Crimea kwa kusema kwamba analazimika kuwalinda watu kutokana na mafashisti walioko Kiev waliompinduwa Yanukovich kufuatia uasi uliosababisha kuuwawa kwa zaidi ya watu 100

Vituo vya kupiga kura huko Crimea vimefunguliwa saa mbili asubuhi na kufungwa saa 12 baadae. Matokeo ya awali yatatolewa baadae usiku na matokeo rasmi ya mwisho yatatangazwa baada ya siku mbili tatu.

Wapiga kura milioni 1.5 wa Crimea wanatakiwa waamuwe kati ya mambo mawili : kuungana na Urusi au kuupa mkoa wao ambao unadhibitiwa na wanasiasa wenye kuunga mkono Ikulu ya Urusi haki kamili ya kujiamulia majaaliwa yake na kuchaguwa nchi inayotaka kujenga nayo uhusiano ikiwemo Urusi.

Mwandishi : Mohamed Dahman/ Reuters

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com