1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kremlin: Putin hatoshiriki mkutano wa G20

7 Septemba 2023

Ikulu ya Kremlin imesema rais Vladimir Putin hana mpango wa kushiriki mkutano wa kilele wa mataifa 20 yaliyostawi kiviwanda na yanayoinukia kiuchumi G20 hata kwa njia ya video.

https://p.dw.com/p/4W4mi
Russland Präsident Sprecher Peskov vor Putin
Picha: Alexander Zemlianichenko/AP/picture alliance

Msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov amewaambia waandishi wa habari kwamba shughuli zote zitaongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje Sergei Lavrov, anayeongoza ujumbe wa Urusi mjini New Dehli.

Lavrov aliiwakilisha Urusi katika mkutano wa Agosti wa BRICS mjini Johannesburg, kufuatia mzozo kuhusu iwapo Afrika Kusini italazimika kumkamata Putin chini ya kibali cha Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu ICC.

Soma pia: Marekani kujadiliana na ICC juu ya uhalifu dhidi ya Putin

Mkutano huu unajiri huku kukiwa na uhusiano mbaya kati ya Moscow na nchi za Magharibi kuhusu mzozo wa Ukraine, ambao ulisababisha mvutano mkubwa katika mkutano wa kilele wa mwaka jana mjini Bali.

Aidha rais wa China Xi Jingping pia hatohudhuria mkutano wa G20 nchini India wakati kuna mvutano wa mpaka kati yake, Marekani na India.