1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kongamano la kudhibiti uhalifu wa kiholela Afrika mashariki

Charles Ngereza.27 Novemba 2018

Waendesha mashtaka na wakuu wa upelelezi Afrika mashariki wakutana Arusha tanzania kuzungumzia namna ya kudhibiti uhalifu wa kimataifa na ugaidi.

https://p.dw.com/p/38zcW
Tansania Wayamo Foundation Bettina Ambach
Picha: DW/C. Ngereza

Wakuu wa taasisi za kuendesha mashitaka na wakurugenzi wa idara za upelelezi wa makosa ya jinai kutoka nchi za Afrika mashariki wamekutana leo jijini Arusha kaskazini mwa Tanzania katika mkutano wa kuzungumzia haki jinai kikanda na kimataifa kwa lengo la kudhibiti uhalifu wa kimataifa na ugaidi. 

Mkutano huo pia utaangazia masuala ya uwajibikaji dhidi ya uhalifu wa kupangwa kutoka nchi moja hadi nyingine na upatikanaji wa haki na masuala ya ufisadi ambayo yanaelezwa kuchangia kuenea kwa makundi ya uhalifu ambao hufanya matukio ya uhalifu ndani na nje ya mipaka ya mataifa yao.

Mkutano huo ambao pia unahudhuriwa na wanasheria wawakilishi wa mahakama za kikanda na mahakama ya kimataifa ya jinai utaangalia mafanikio ya ushirikiano miongoni mwa watendaji wa ofisi za waendesha mashitaka katika nchi za Afrika mashariki katika kudhibiti uhalifu unaovuka mipaka miongoni mwa mataifa ya Afrika Mashariki.

Nurdin Haji ni mwendesha mashitaka nchini Kenya na hapa anaeleza ushirikiano huo ulivyosaidia katika udhibiti wa uhalifu nchini humo huku akisisitiza kuwa maafisa wa idara hiyo wanapaswa kuwa wajasiri na kufuata sheria na katiba za nchi zao ili kuweza kutoa haki bila kujali nafsi na nguvu ya mtu yeyote anayeshiriki katika uhalifu.

Kwa upande wake mkuu wa ofisi ya mwendesha mashitaka nchini Tanzania Biswalo Maganga amesema kuwa ushirikiano miongoni mwa waendesha mashitaka umerahisisha utendaji wa ofisi za wanesha mashitaka pamoja na kurudushwa kwa mali zinazoporwa kutoka nchini moja hadi nyingine

Mwakilishi wa kundi la watalaamu na wanasheria wabobezi wa haki jinai katika anga za kimataifa katika Afrika jaji Omari Chande amesema kuwa mafanikio ya uhalifu wa kimataifa umeanza kudhibitiwa vilivyo huku akitaja tukio la kinara usafirishaji haramu wa binadamu kwenda katika mataifa ya Ulaya kukamatwa nchini Sudan.

Mkutano huo umeandaliwa na wakfu wa Wayamo wenye makao yake Berlin nchini Ujerumani pamoja na kundi la wanasheria Afrika wanaoangazia uwajibikaji na haki na kufadhiliwa na serikali ya ujerumani kupitia ofisi ya maswala ya kimataifa katika wizara ya mambo ya nchi za nje ya nchi hiyo.

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman