KLABU BINGWA AFRIKA-COPA AMERICA NA ASIAN CUP | Michezo | DW | 09.07.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Michezo

KLABU BINGWA AFRIKA-COPA AMERICA NA ASIAN CUP

Vinyan'ganyiro hivyo 3 vyaendelea wakati mashindano ya Tennis ya wimbledon yameshatawaza malkia na mfalme.

KOMBE LA KLABU BINGWA LA AFRIKA:

Mabingwa watetezi Al Ahly ya Misri wamefungua mwanya wa pointi 3 usoni katika kundi lao baada ya kuizaba jana ASEC Abidjan ya Ivory Coast bao 1:0.Aboutrika,mchezaji wao wa kiungo ndie alielifumania lango la ASEC muda mfupi kabla kipindi cha mapumziko.

Al Hilal ya Sudan ,ilitamba nayo jana katika kundi B ilipoitimua Espereence ya Tunisia kwa mabao 2:0 huko Oumdurman.Huo ni ushindi wa kwanza kwa wasudani.Mnigeria Eze ndie alietia mabao yote 2.

Tayari hapo jumamosi Al Itihad ya Libya ilimudu suluhu 0:0 huko Tunisia na Etoile du sahel.JS Kabylie ya Algeria, inafuata nyuma ya timu hizo 2 ikiwa na point 3.Duru ijayo itachezwa mwishoni mwa wiki ya julai 20.

Katika Kombe la dunia la chipukizi chini ya umri wa miaka 20 Austria na Chile zimeingia kundi la duru ijayo ya timu 16 baada ya kutoka suluhu 0:0.

Kongo imeingia pia kundi hilo na kuiacha nyuma kanada wenyeji.

Kongo iliizaba Kanada mabao 2:0 kufuatia magoli ya Ngakosso na Ikouma.

Katika kundi C ,Gambia ilichapa Ureno 2:1 licha ya mchezaji wao 1 kutolewa nje ya uwanja na rifu.

Ilikua lakini Ureno iliotangulia kutia bao kabla Ousman Jallow kusawazisha.Mnamo dakika ya 68 ya mchezo Abdoilie Mansally, akaipatia Gambia bao la ushindi.Ureno pia ikiwa imemaliza nafasi ya 3 inaingia duru ijayo.

Katika Copa America,Brazil imeanza kutamba ,kwani mwishoni mwa wiki Brazil-mabingwa wa kombe hilo walirarua Chile kwa mabao 6-1.Venezuela wenyeji walikiona cha mtema kuni walipopigwa kumbo na Colombia kwa mabao 4-1.

Mexico iliinyeshea mvua ya magoli Paraguay ilipoichapa mabao 6-0 na hivyo kama Brazil, imekata tiketi ya nusu-finali kati yake na Argentina. Argentina iliilaza Peru mabao 4-0.

Brazil ina miadi na Colombia katika nusu-finali na ishara zaonesha kana kwamba finali ya Copa America yamkini ikawa kati ya Brazil na Argentina,mradi tu Mexico haiitili kitumbua chake mchanga Argentina.

Wakati Copa Amerika inakaribia ukingoni,Kombe la bara la Asia-ASIAN CUP ndio kwanza lapambamoto baada ya kufunguliwa jumamosi mjini Bangkok:

Dola kuu barani Asia-China laweza kesho kuzusha msangao likiingia uwanjani na Malaysia.Malaysia ndio chipukizi kabisa katika orodha ya timu 16 zinazoania Asia Cup.

Mabingwa Japan,Iran,saudi Arabia na Korea ya Kusini,ndizo zinazotazamiwa mno kutamba katika Kombe hili.

Leo zawadi Cup inaanza huko Tanzania,lakini mashabiki wa dimba la chipukizi na hasa nchini Burundi wafurahia kuanzishwa kwa kombe la CECAFA la chipukizi chini ya umri wa miaka 17 -kombe lililotolewa na rais wa Tanzania-Jakaya Kikwete.Pia wanafurahia litachezwa katika uwanja mpya wa nyasi ya kimamboleo inayotandazwa kwenye uwanja wa Bujumbura:

Huko Tanzania,Simba imeivua taji Young Africans na sasa inarudi katika kombe la klabu bingwa barani Afrika:Simba ilihitaji lakini, changamoto ya mikwaju ya penalty kuitoa Yanga.

Wimbledon:

Baada ya msichana wa Marekani Serena williams kuvaa kwa mara ya 4 taji la Wimbledon upande wa wanawake hapo jumamosi,jana ilikua zamu ya maswisi Roger Federer kutamba mbele ya Rafael Nadal.Hatahivyo, alitolewa jasho kali na mspain Nadala kabla Federer kuondoka na taji lake la 5 la Wimbledon kupitia seti 5.

Kwa ushindi huo wa 5 wa taji la wimbledon,Roger Federer,amesawazisha rekodi ya Mswede Bjorn Borg ambae binafsi alikuwapo uwanjani kuangalia changamoto hiyo.Borg alizuwiliwa ushindi wa 6 1981 alipotiwa munda na John McEnroe wa Marekani.

Roger Federer anapanga kurudi mwakani Wimbledon kuivunja rekodi ya Bjorn Borg,lakini anajua Nadal analinyatia mno taji hilo.

 • Tarehe 09.07.2007
 • Mwandishi Ramadhan Ali
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHbl
 • Tarehe 09.07.2007
 • Mwandishi Ramadhan Ali
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHbl
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com