1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiUganda

Kiwango cha mimba za utotoni nchini Uganda bado kiko juu

8 Agosti 2023

Kiwango cha wasichana wenye umri mdogo kupata mimba nchini Uganda kinazidi kuleta hofu na mashaka miongoni mwa umma ambapo hadi idadi robo ya watoto hao ambao hawajatimu miaka 18 wamejikuta katika hali hiyo.

https://p.dw.com/p/4UtWa
Zimbabwe | Schwangere Frau in Seitenstraße
Msichana mdogo aliyebeba ujauzitoPicha: Tsvangirayi Mukwazhi/AP/picture-alliance

Licha ya juhudi za wadau mbalimbali kujaribu kujitokeza na suluhu  kwa suala la watoto wa kike wa chini miaka 18 kupata mimba, takwimu za hivi karibuni za mashirika mbalimbali zinaonyesha kuwa kiwango cha hali hiyo ni cha juu. Kwa mujibu wa takwimu  za Shirika la takwimu Uganda  UNBS, hadi asli mia 25 ya watoto wa kike chini ya miaka 18 hupata mimba za utotoni.

Vyanzo vya mienendo hii vinaelezewa kuwa hali ya umasikini, kiwango cha juu cha wasichana kuacha masomo kutokana na sababu mbalimbali pamoja na malezi duni katika mazingira wanamoishi. Kamishna wa vijana na watoto Kyateka Mondo anatoa mtazamo huu.

Tanzania, wanafunzi
Baadhi ya wasichana wanaofadhiliwa na shirika la AGAPE katika mapambano ya mimba za utotoni huko TanzaniaPicha: DW/V. Natalis

Kama njia ya kuashiria suala la umasikini, wilaya moja Mashariki mwa Uganda ya Kamuli ambayo inaelezewa kuwa ndiyo yenye idadi kubwa ya wasichana wanaopata mimba  pia ndiyo inayoorodheshwa kuwa miongoni mwa wilaya masikini. Suala la baadhi ya wasichana kuacha masomo linasababibishwa pia na ukosefu wa sodo za hedhi. 

Wengi wa wasichana hao wakibaleghe na kuanza kushughulikia mambo ya hedhi kila mwezi, baadhi huingiwa na fedheha kwa kuwa hawana uwezo wa kukidhi mahitaji hayo na pia kuhisi unyanyapaa miongoni mwa wenzao wa kiume.

Soma hii: Mimba za utotoni zaongezeka nchini Burundi

Kulingana na wadaMimba za utotoni zaongezeka nchini Burundiu, shule nyingi siku hizi hazina walimu wa kike wanaoweza kuwasaidia wasichana kuelewa hali zao na kuwapa hima kustahimili. Katika baadhi ya shule walimu wa kiume ndiyo wamekubali kuwasughulikia wasichana, jambo ambalo bila shaka huwaweka wanafunzi katika hofu ya kudhulumiwa na walimu wao hao.

Ndoa za mapema, VVU na unyanyasaji wa kingono tatizo Kenya

Kwa mujibu wa takwimu hizo, kiwango cha juu cha wasichana kupata mimba za utotoni mbali na kuzingatia madhara mengine kama vile maambukizo ya magonjwa ya zinaa huigharimu Uganda dola milioni mia 700 kila mwaka kuwashughulikia wasichana hao kiafya pale wanapopata matatizo ya uzazi. Hii ni kwa sababu hawajakomaa kimwili kuweza kuzaa kwa njia za kawaida na wengine huhatarisha maisha yao wanapojaribu kutoa mimba hizo.  

Wadau wana mtazamo kuwa fedha hizi zingetumiwa kuwasaidia kubaki shuleni kuendelea na masomo yao hata baada ya kujifungua. Lakini pia familia na jamaa za wasichana hao zinakosolewa kwa kuhusika katika kuwaoza mapema, kuwaficha wale wanaowadhulumu kingono badala ya kuwafikisha kwa mamlaka za kisheria na la kusikitisha zaidi ni pale jamaa au mzazi anapokuwa yeye ndiye amehusika katika kitendo hicho.

Huku mwito ukitolewa kwa wanaume pia kujiepusha na mienendo ya kuingia mahusiano ya kimapenzi na wasichana walio  chini ya umri stahiki, wasichana wenyewe wanahimizwa kufahamu athari za matokeo ya kuingia majukumu ya uzazi wakiwa wenyewe hawawezi kukidhi mahitaji yao binafsi.