1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mimba za utotoni zaongezeka nchini Burundi

29 Septemba 2021

Baraza la seneti nchini Burundi limesema linatiwa wasiwasi na ongenzeko la idadi ya wasichana wanaoacha shule kutokana na kupata ujauzito au kuolewa mapema.

https://p.dw.com/p/412AE
Zimbabwe | Schwangere Frau in Seitenstraße
Picha: Tsvangirayi Mukwazhi/AP/picture-alliance

Hayo yamebainishwa katika mkutano wa wadau wa haki za binadamu, ambapo imedhihirika  kuwa mimba na ndoa za mapema miongoni mwa wanafunzi wa kike zimeongezeka nchini humo.

Kulingana na uchunguzi uliofanywa na halmashauri ya baraza la seneti inayo husika na usawa wa jinsia na haki za binaadam, katika shule za kiserikali na hata za kibinafsi wasichana wengi huacha shule baada ya kubeba mimba  na wengine kuolewa mapema.

Seneta  Faida Devote mkuu wa halmashauri hiyo, amesema katika mwaka wa shule wa 2019 hadi 2020 wasichana zaidi ya 1200 waliacha shule kutokana na kubebe mimba wakiwa katika elimu ya msingi  na hivyo kuacha masomo.

''Takwimu tulizo nazo zaonesha kuwa wanafunzi 1233 walibebe mimba nchini zima katika mwaka peke wa shule wa 2019 hadi 2020 kote nchini. Mkoa wa Muyinga ukiongoza kwa kuwa na idadi ya wanafunzi 101, Ukifuatiwa na mkoa wa Rutana ambako walibebe mimba za utotoni wasichana wakiwa 70. Mkoa wa Kayanza ukichukuwa nafasi ya 3.''

Naye Mwanasheria Muhigwa Solenge ambaye pia ni mdau wa maswala ya usawa kijinsia, ameonesha washiriki  sababu kuu zinazosababisha watoto wa kike kubeba mimba za mapema.

Mwanasheria huyo amesema kuna sababu hizo  ni pamoja na umasikini na matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii. Lakini pia amewalaumu baadhi ya wazazi kutowajibika katika majumu yao ya kulea.

Tansania - AGAPE Frauenkollektiv - Proteste von Schülerinnen
Wanafunzi wakiandamana kupinga ndoa za mapemaPicha: DW/V. Natalis

''Watoto wetu tumekuwa tukiwaacha muda mrefu na wasaidizi wa nyumbani, aidha na waalimu wa masomo ya ziada, tukisahau kuwa wakati mwingine baada ya masomo watoto hao hufundishwa mambo mengine yanayowaharibu, na hawawezi kuwaambia wazazi wao.''

Baraza la seneti limekiri kuwepo na umuhimu wa kubuniwa mikakati ya kukabiliana na sababu hizo zinazo changia wasichana kubeba mimba za utotoni na kuozwa mapema.

Seneta  Faida Devote mkuu wa halmashauri ya usawa kijinsia na haki za binaadam ameseama lazima baraza hilo lihakikishe haki kwa wasichana ya kusoma  na kuwasaidia waliobeba mimba za utotoni.

''Mkutano huu unadhihirisha dukuduku la baraza la seneti katika kukabiliana na mimba za utotoni na wasichana kuolewa mapema. Hivyo katika mkakati mojawapo ni kufanyika kampeni ya kuwahamasisha, wazazi kuwajibika  matika majumu yao ya kulea, waalimu pia na wasichana kuwaonesha hatari juu ya swala hilo"

Takwimu za nyuma kwenye ngazi ya kitaifa zilizotokana na ripoti ya mwaka 2014 zilionesha kuwa wasichana elf 14 104 walibeba mimba za utotoni. Tayari sheria ilifanyiwa marekebisho na kuwaruhusu wasichana waliojifungua kuendelea na shule.