1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Japan Tokio | Premierminister Fumio Kishida, Ankündigung Ideen für Russland-Sanktionen
Picha: Stanislav Kogiku/AP Photo/picture alliance
SiasaUkraine

Kishida aanza ziara yake ya ghafla nchini Ukraine

John Juma
21 Machi 2023

Waziri Mkuu wa Japan Fumio Kishida ameanza ziara yake ya ghafla nchini Ukraine Jumanne, huku rais wa China Xi Jinping akizuru Urusi.

https://p.dw.com/p/4OyTa

Waziri Mkuu wa Japan Fumio Kishida atakutana na mwenyeji wake Volodymyr Zelensky katika mji mkuu Kiev Jumanne.

Anatarajiwa kutoa heshima kwa ujasiri na subira ya Waukraine wanaopambana katika kuilinda nchi yao pamoja.

Kulingana na wizara ya mambo ya nje ya Japan iliyotangaza ziara hiyo, Kishida ataihakikishia Ukraine uungwaji mkono na mshikamano kama kiongozi wa Japan na pia kama mwenyekiti wa mataifa saba tajiri zaidi ulimwenguni G-7.

Kishida anatarajiwa kushutumu vikali uvamizi wa Urusi nchini Ukraine. Ziara yake ambayo haikutangazwa mwanzo imejiri saa chache tu baada ya kukutana na Waziri Mkuu wa India Narendra Modi mjini New Delhi, na pia wiki moja tu baada ya mkutano wake wa kilele na Rais wa Korea Kusini Yoon Suk Yoel.

Viongozi wa Ujerumani na Japan wakutana Tokyo

Akiwa New Delhi, Kishida alitoa wito kwa mataifa yanayoinukia na yale maskini kupaza sauti zao ili kulinda sheria ya kimataifa na kusaidia kukomesha vita vya Urusi nchini Ukraine.

Josep Borrell (kushoto) akizungumza na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ubelgiji Hadja Lahbib wakati wa mkutano wa mawaziri wa nje na wa Ulinzi wa nchi za Umoja wa Ulaya Jumatatu Machi 20, 2023 mjini Brussels, Ubelgiji.
Josep Borrell (kushoto) akizungumza na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ubelgiji Hadja Lahbib wakati wa mkutano wa mawaziri wa nje na wa Ulinzi wa nchi za Umoja wa Ulaya Jumatatu Machi 20, 2023 mjini Brussels, Ubelgiji.Picha: Geert Vanden Wijngaert/AP Photo/picture alliance

Mivutano ya Japan dhidi ya Urusi na China

Japan ambayo ina mivutano ya visiwa kati yake na China na vilevile Urusi, ina wasiwasi kuhusu uhusiano wa karibu kati ya nchi hizo mbili ambazo tayari zimefanya luteka za pamoja karibu na pwani za Japan.

Japan imejiunga na nchi za Umoja wa Ulaya na vilevile Marekani kuipa Ukraine misaada ya kiutu lakini pia kuiwekea Urusi vikwazo kufuatia hatua yake ya kuivamia Ukraine.

Kando na hayo, nchi za Umoja wa Ulaya zinapanga kuipa Ukraine risasi za kivita milioni mojakatika kipindi cha miezi 12 ijayo. Hayo ni kulingana na makubaliano yaliyofikiwa Jumatatu mjini Brussels.

Viongozi duniani wazungumzia mwaka mmoja wa vita Ukraine

Mwanadiplomasia mkuu wa umoja huo Josep Borrell aliandika kwenye ukurasa wake wa twitter kwamba umoja huo unachukua hatua muhimu kuipa Ukraine risasi zaidi.

Makombora ya Urusi yaharibiwa Crimea?

Mji wa Bakhmut, uharibifu mkubwa ni thibitisho ya hasara kutokana na vita.
Mji wa Bakhmut, uharibifu mkubwa ni thibitisho ya hasara kutokana na vita.Picha: AP Photo/picture alliance

Kwingineko, mlipuko katika mji wa Dzhanko katika rasi ya Crimea umeharibu makombora ya Urusi yaliyokuwa yakisafirishwa kwa njia ya reli. Wizara ya Ulinzi ya Ukraine imesema hayo.

Ukraine imedai makombora hayo yalikusudiwa kutumiwa na vikosi vya majini vya Urusi katika Bahari Nyeusi.

Putin asema yuko tayari kuujadili mpango wa China kuhusu Ukraine

Wizara hiyo ya Ukraine haikuthibitisha ikiwa vikosi vyake vimehusika na mlipuko huo.

Urusi hali kadhalika haijathibitisha ikiwa makombora yake yaliharibiwa.

Haya yanajiri mnamo wakati, rais wa China Xi Jinping akikutana na rais wa Urusi Vladimir Putin mjini Moscow, ambapo mada inayotarajiwa kupewa kipaumbele kwenye mkutano wao wa kilele ni kuhusu vita vya Ukraine.

Vyanzo: APE, DPAE