Kiongozi wa upinzani Urusi, Navalny, arejeshwa jela | Matukio ya Kisiasa | DW | 29.07.2019
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Kiongozi wa upinzani Urusi, Navalny, arejeshwa jela

Kiongozi wa upinzani nchini Urusi Alexei Navalny amerejeshwa jela baada ya kupelekwa hospitali kwa kile anachodai daktari wake kuwa alipewa sumu. Serikali inasema haikuwa sumu, bali ni tatizo dogo la ngozi.

Mwakilishi wa hospitali ameliambia shirika la habari la Urusi TASS kwamba Navalny tayari ameshapatiwa matibabu na amerejeshwa jela.

Awali leo hii, daktari wa Navalny, Anastasiya Vasilyeva, amesema sumu huenda ikawa imemsababishia kuugua na anapinga hatua ya kurejeshwa jela mwanasiasa huyo.

Navalny alipelekwa hospitali Jumapili kutoka jela ambako anatumikia kifungo cha siku 30 kwa kuitishwa maandamano yaliyokatazwa na serikali. Alikamatwa siku chache kabla ya kufanyika maandamano makubwa ya upinzani Jumamosi iliyopita, ambayo yalipelekea  watu 1,400 kutiwa mbaroni na polisi.

Vasilyeva, ambaye ni daktari wa Navalny kwa miaka kadhaa, amesema leo kuwa alimkuta mwanasiasa huyo akiwa amevimba uso pamoja na kujawa na vipele hali inayoashiria kuwa alipewa sumu.

"Ninawasihi wenzangu wamuweke chini ya uangalizi wa kimatibabu kwa angalau siku tatu, hadi uchunguzi wa kitafiti utakapokuwa tayari. Lakini, nasikitishwa na amri iliyotolewa kutoka juu. Sasa hivi ameongozwa na polisi hadi chumba cha ulinzi," amesema Vasilyeva.

Russland Moskau Protest Opposition Polizei (Reuters/S. Zhumatov)

Polisi wa Urusi wakimtia mbaroni mwandamanaji kwa kutumia nguvu

Elena Sibikina, mmoja wa madaktari waliomtibu Navalny amewaambia waandishi habari kwamba madai ya kuwa amepewa sumu hayakuweza kuthibitishwa. Daktari huyo ameongeza kwamba maisha ya Navalny hayapo hatarini.

Ujerumani yataka waandamanaji waachiliwe huru

Navalny amekuwa akiikosoa serikali ya Urusi tangu mwaka 2011, alipoongoza maandamano makubwa ya kumpinga Rais Vladimir Putin na chama chake tawala.

Tangu wakati huo ameshakutikana na hatia kwa mshtaka ya aina mbili tofauti, na amekuwa akishikiliwa jela mara kwa mara kwa kuvuruga utulivu wa umma na kuongoza maandamano yaliyopigwa marufuku na serikali.

Ujerumani leo imeitolea wito serikali ya Urusi, haraka kuwaachilia huru watu 1,400 waliokamatwa wakati wa maandamano makubwa ya mjini Moscow yaliyofanyika mwishoni mwa juma. Maripota wa shirika la habari la AFP wameshuhudia waandamanaji kadhaa waliopata majeraha, kutokana na polisi kutumia marungu wakijaribu kuwatawanya.

Ulrike Demmer, msemaji wa kansela wa Ujerumani Angela Merkel, pia ameisisitizaUrusi kuheshimu uhuru wa kujieleza na kuandamana na kuhakikisha viwango vya kimataifa vinazingatiwa wakati wa uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika mwezi Septemba.

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com