1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kikosi cha awali cha Umoja wa Mataifa chawasili Yemen

Zainab Aziz
22 Desemba 2018

Umoja wa mataifa umesema mkuu wa kikosi cha awali cha Umoja wa Mataifa jenerali mstaafu Patrick Cammaert amewasili nchini Yemen pamoja na kikosi chake kuangalia usitishwaji mapigano Hodeida.

https://p.dw.com/p/3AXTs
UN Sicherheitsrat Yemen
Picha: Reuters/C. Allegri

Cammaert anakiongoza kikosi hicho hicho kinachohusika na ufuatiliaji tangu kufikiwa makubaliano ya kusitisha mapigano katika mji wa bandari wa Hodeidah nchini Yemen, kati ya wapigananaji wa Houthi wanaoungwa mkono na Iran na vikosi vya majeshi ya muungano unaoongozwa na  Saudi Arabia.

Pande zote zililizokuwa zinashiriki kwenye vita vya Yemen kwa karibu miaka minne zilikubaliana kusitisha mapigano wakati wa mazungumzo ya amani yaliyofadhiliwa na Umoja wa Mataifa yaliyofanyika nchini Sweden mapema mwezi huu. Pamde hizo pia ziliahidi kuondoa majeshi yao kutoka kwenye jiji la Hodeidah. Makubaliano hayo yalianza kufanya kazi mnamo siku ya Jumanne lakini vurugu ziliripotiwa kutokea nje ya jiji hilo.

Mnamo siku ya Ijumaa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa liliidhinisha kupelekwa kikosi cha awali cha waangalizi chini ya usimamizi wa generali mstaafu Patrick Cammaert kwa muda wa siku 30.

Alipowasili kwenye uwanja wa ndege wa Aden, Cammaert alikutana na viongozi serikali inaoungwa mkono na Saudi Arabia ambapo pia anatarajiwa kwenda katika mji wa Sanaa ambako atakutana na wawakilishi wa Houthi.

Mkuu huyo wa kikosim cha Umoja wa mataifa baadae atakwenda Hodeidah kushuhudia makubaliano ya kusitishwa mapigano na uondoaji wa majeshi kutoka kwenye mji huo wa Hodeidah na miji mingine mitatu ya bandari.

Wapiganaji wa Houthi katika jiji la Hodeidah nchini Yemen
Wapiganaji wa Houthi katika jiji la Hodeidah nchini YemenPicha: Reuters/A. Zeyad

Kikosi cha jenerali mstaafu Cammaert hakitavaa sare rasmi wala kubeba silaha. Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa kikosi hicho kitakuwa na kazi ya kusaidia shughuli za usimamizi wa na ukaguzi katika bandari za Hodeidah, Salif na Ras Issa pamoja na kuimarisha uwepo wa kikosi cha Umoja wa mataifa katika kanda hiyo inayokabiliwa na vita.

Bandari hiyo kuu ya Hodeidah, iliyotumiwa kuingiza chakula kwa raia wa Yemen wapatao milioni 30 imekumbwa na machafuko mabaya katika mwaka huu, hali iliyosababisha hofu kwa jamii ya kimataifa kuwa mgogoro huo ungesababisha kukatizwa kabisa harakati za kuwafikishia chakula na mahitaji mengine karibu watu milioni 16 walio kwenye hatari ya kukumbwa na baa la njaa.

Mkataba wa Sweden, ni ufanisi wa kwanza muhimu katika jitihada za kutafuta amani katika kipindi cha miaka mitano, kwa maana ya kusafisha njia ya kusitisha mapigano katika nchi hiyo masikini na pia kuweka uwezekano wa kufanyika duru ya pili ya mazungumzo ifikapo mwezi Januari mwaka ujao.

Ushirikiano wa Waislamu wa madhehebu ya Sunni unaongozwa na Saudi Arabia na Falme za Kiarabu ziliingia kwenye vita mwaka 2015 dhidi ya wapigananji wa Houthi.

Kwa ajili ya kuirejesha mamlakani serikali inayotambuliwa kimataifa ya Abd-Rabbu Mansour Hadi, iliyotimuliwa kutoka kwenye mji mkuu wa Sanaa. Kundi la Houthi linadhibiti maeneo mengi ya mijini, ikiwa ni pamoja na mji mkuu wa Sanaa, wakati serikali ya Mansoour Hadi inadhibiti bandari ya kusini ya Aden.

Mwandishi:Zainab Aziz/RTRE
Mhariri: Bruce Amani