1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenyatta: Ruto anataka kukinyakua chama cha Jubilee

Shisia Wasilwa22 Mei 2023

Rais mstaafu wa Kenya Uhuru Kenyatta amemsuta Rais William Ruto kwa madai ya kutaka kukinyakua chama cha Jubilee. Akizungumza alipoongoza mkutano mkuu wa wajumbe wa chama hicho, Kenyatta amesema hatatishwa.

https://p.dw.com/p/4Rg7l
Kenia Nairobi | Jubilee Party hält National Delegates Council trotz interner Krise ab
Picha: Shisia Wasilwa/DW

Hatimaye mkutano mkuu wa chama cha Jubilee ambao ulikuwa umeahirishwa mara kadhaa umefanyika leo huku wajumbe 4000 wakihudhuria. Baada ya mkutano huo mabadiliko kadhaa yalifanywa huku viongozi waasi wakitimuliwa.

Sabina Chege ambaye alikuwa amejitangaza kuwa Kiongozi wa chama hicho na Katibu Mkuu Kanini Kega ambaye alikuwa amejitangaza kuwa Katibu Mkuu walitumuliwa baada ya mkutano huo. Kiongozi wa chama hicho ambaye ndiye Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta alitumia fursa hiyo kuikosa  serikali ya Rais William Ruto aliyekuwa naibu wake kwa mihula miwili kwa madai ya kuvuruga chama hicho.

"Fikira zangu zilisema nilegee niwache siasa...lakini wengine wameamua kwamba kazi ni ya vitisho na kulazimisha. Nawaambia Leo watafute mwingine wa kutisha sio uhuru wa Kenyatta.”

Kenia Nairobi | Jubilee Party hält National Delegates Council trotz interner Krise ab
Wajumbe wa chama cha Jubilee wakihudhuria mkutano mkuu wa kitaifaPicha: Shisia Wasilwa/DW

Chama hicho kimepata viongozi wapya: Mwenyekiti atakuwa Saitoti Torome nao Manaibu viongozi waliochaguliwa ni pamoja na Beatrice Gambo atakayeongoza mikakati, Maoka Maore atakayeangazia Operesheni za chama, Joshua Manje wa mipango na Kados Muiruri atakayehakikisha chama kinapata wanachama wapya. Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta atasalia kuwa kiongozi wa chama. Raila Odinga pamoja na viongozi wenza wa Azimio wamehudhuria mkutano huo.

Soma pia: Upinzani wa Kenya waishutumu serikali kwa kuchochea matabaka

Kambi ya siasa ya Sabina Chege na Kanini Kega imepuuzilia mbali maamuzi ya Jumatatu ikisema kuwa Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta si kiongozi halali wa chama, wakishikilia kuwa katiba inasema kuwa rais mstaafu hafai kuongoza chama chochote baada ya miezi sita ya kustaafu. Miezi tisa imekatika tangu uchaguzi mkuu uandaliwe. Sasa inasubiriwa iwapo kambi hiyo itachukua hatua ya kufika mahakamani na kupinga maamuzi hayo. Sabina Chege ameyasema haya:

Wasemaji walikosa serikali ya Rais William Ruto kwa sera zake ambazo zimechangia kuongezeka kwa gharama ya maisha. Chama cha Jubilee, kilitumika na Uhuru kuingia kwenye uongozi mwaka 2017 na ni moja ya vyama tanzu kwenye muungano wa Azimio. Aidha chama hicho kilimpigia debe Raila kuwania kiti cha urais kwenye uchaguzi mkuu uliopita ambapo William Ruto alishinda kinyume na matarajio ya wengi.