1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wabunge wa Tanzania waikosoa kauli ya Paul Makonda

Amina Mjahid
6 Mei 2020

Baadhi ya wabunge nchini Tanzania wameikosoa vikali kauli ya mkuu wa mkoa wa Dar es salaam, Paul Makonda aliyewatishia kuwakamata na kuwapa mashtaka ya uzururaji iwapo hawatohudhuria vikao vya bunge mjini Dodoma.

https://p.dw.com/p/3brJz
Tansania Daressalam Paul Makonda
Picha: DW/S. Khamis

Mkuu huyo wa mkoa ametoa muda wa saa 24 kwa wabunge wote walioko katika jiji hilo kuondoka vinginevyo atawatia mbaroni. 

Kauli yake hiyo mbali ya kuzua gumzo kubwa pia, imekuwa ikijadiliwa kwa kulinganisha na kauli zake zinazofanana na hizo alizowahi kuzitoa siku za nyuma ambazo nyingine ziliitia serikali katika mvutano na baadhi ya madola ya Magharibi.

Makonda ambaye amepigwa marufuku kuingia Marekani na serikali ya nchi hiyo amesema katika kipindi hiki cha janga la corona anataka kuona wabunge wote wanashiriki vikao vya Bunge mjini Dodoma na kama ataonekana mbunge yoyote ndani ya mkoa wake bila ruhusa ya spika basi atamshughulikia.

Wabunge wanasema kiongozi huyo wa mkoa amevuka mipaka kwa kutoa maagizo dhidi ya wabunge ambao hana mamlaka nao.

Mmoja wa wabunge hao, ni Peter Msigwa ambaye ni mbunge wa chadema Iringa mjini, amesema kauli ya mkuu huyo wa mkoa inakwenda kinyume na katiba ya nchi inayotoa ruhusa kwa kila raia kuwepo sehemu yoyote bila kuvunja sheria.

Spika wa bunge hajatoa tamko lolote kuhusu kauli ya Makonda

Tansania Wahl des Premierministers Kassim Majaliwa
Spika wa bunge la Tanzania Job NdugaiPicha: DW/H. Bihoga

Mara kadhaa Mkuu huyo wa mkoa amekuwa akitoa kauli zinazozua mivutano ikiwemo kauli yake moja ya kutaka kuendesha msako dhidi ya watu wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja, kauli ambayo baadaye ilifutiliwa mbali na serikali kuu iliyosema kuwa huo siyo msimamo wa Tanzania.

Kando na hayo kampeni zake nyingi anazotangaza ikiwamo kuendesha operesheni dhidi ya watumiaji shisha, wanaume wanaowatelekeza wake au wachumba zao, msako wa nyumba kwa nyumba kuwabaini wahalifu na nyinginezo nyingi, zimekuwa zikipotea kimya kimya bila mrejesho wowote.

Spika wa bunge hajazungumza lolote kuhusu kauli hii ya mkuu wa mkoa, lakini amekiambia kituo kimoja cha televisheni nchini kuwa wabunge waliosusia vikao kwa hofu ya vurusi vya corona wamefanya hivyo kwa utashi wao wenyewe, na bunge litaendelea hata kama hawatarejea bungeni.

Chanzo George Njogopa