1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kauli ya dhihaka ya Macron yazidisha hasira barani Afrika

13 Januari 2025

Sifa ya Ufaransa katika makoloni yake ya zamani barani Afrika imekuwa ikidorora kwa muda. Hotuba ya hivi karibuni ya Rais Emmanuel Macron huenda ikazidisha mpasuko. Macron aliyatuhumu mataifa ya Afrika kukosa shukurani.

https://p.dw.com/p/4p46F
Guinea-Bissau | Ziara ya Rais Emmanuel Macron
Emmanuel Macron akiwa ziarani Guinea-BissauPicha: LUDOVIC MARIN/AFP/Getty Images

Katika video hiyo, uso wa Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron ni usiyo na  tabasamu, yumkini hata unaonyesha kukasirika. "Nadhani wamesahau kusema 'asante'," Macron alisema. Kisha akaongeza kwa maneno ya moja kwa moja: "Ninasema haya kwa serikali zote za Afrika ambazo hazikuwa na ujasiri mbele ya maoni ya umma kuonyesha kuwa hakuna hata moja yao ingekuwa nchi huru leo ikiwa jeshi la Ufaransa lisingepelekwa katika eneo hili." Macron alinyoosha kidole huku akiinua nyusi zake.

Tukio hili limeibua hisia kali tangu Jumatatu. Ni kipande cha hotuba ya Macron aliyoitoa kwenye mkutano wa kila mwaka wa mabalozi wa Ufaransa, ambao walikuja kutoka sehemu mbalimbali duniani kukutana katika Ikulu ya Elysee jijini Paris. Waandishi wa habari pia walialikwa — hivyo Macron alipaswa kuelewa kuwa maneno yake yangefika kwa hadhira pana.

Soma pia: Macron asisisita uwepo Djibouti Ufaransa ikipoteza ngome zake Afrika

Nina Wilén, mchambuzi katika Taasisi ya Uhusiano wa Kimataifa ya Kifalme ya Egmont nchini Ubelgiji, aliiambia DW kwamba kauli hizo huenda zilikuwa kosa la kimkakati.

"Na tunajua kwamba, wakati wa ziara zake barani Afrika, ametoa pia maoni ambayo hayajapokelewa vyema na viongozi wa Afrika, wakati mwingine akitoa mzaha mahali ambapo haikupaswa," alisema Wilén.

Wakati wa ziara yake ya kwanza kama rais barani Afrika mwaka 2017, Macron alisababisha kero wakati wa mazungumzo yasiyo rasmi na wanafunzi nchini Burkina Faso, akiwa ameandamana na Rais wa wakati huo Roch Marc Kabore.

Ufaransa Paris | Emmanuel Macron atoa hotuba yake kwa mabalozi wa Ufaransa
Mabalozi wa Ufaransa huenda wakalazimika kufafanua matamshi ya Macron kwa serikali za AfrikaPicha: Aurelien Morissard/AP Photo/picture alliance

Aliwaambia kuwa ni kazi ya Kabore, siyo ya Ufaransa, kurekebisha mfumo wa umeme, kwani Ufaransa haikuwa tena mkoloni. Kabore alipoondoka kwa muda kwenda chooni, Macron akasema kwa utani: "Tazama, anaondoka kwenda kurekebisha kiyoyozi!" — mzaha ambao umekosolewa baadaye kuwa wa kiburi.

Tukio zito zaidi lilitokea wakati wa mkutano wa waandishi wa habari mjini Kinshasa, mji mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, akiwa na Rais Felix Tshisekedi mwaka 2023. Tshisekedi alikasirishwa na matamshi kuhusu usimamizi mkali wa chaguzi barani Afrika ikilinganishwa na chaguzi za Magharibi.

Macron alijaribu kupunguza uzito wa matamshi hayo, akieleza kuwa hayo yalikuwa maoni ya mwandishi mmoja wa habari tu, si msimamo rasmi wa Ufaransa. Tshisekedi, kwa hasira, alimkatiza na kusema chanzo cha matamshi hayo alikuwa Jean-Yves Le Drian, ambaye hakuwa mwandishi wa habari bali alikuwa waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa wakati huo.

Wilén anasema matamshi ya hivi karibuni ya Macron yanaendana na makosa aliyowahi kufanya hapo awali.

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Kinshasa | Felix Tshisekedi na Emmanuel Macron
Rais wa DRC Tshisekedi pia amejihisi kudharauliwa na mwenzake wa Ufaransa, Macron.Picha: JACQUES WITT/POOL/AFP/Getty Images

"Ni vigumu kujua kama haya ni matamshi aliyoyapanga kwa makini," alisema Wilén, "au kama ni kitu alichotaka kusema kwa sababu anahisi kwamba ndiyo njia sahihi ya kufanya."

"Lakini, kwa hakika, kuna maafisa na maofisa wa kijeshi wa Kifaransa wanaofanya kazi kwa bidii kuondoa taswira ya Ufaransa kama mkoloni wa zamani mwenye kiburi barani Afrika," alisema Wilén. "Matamshi kama haya yanayotolewa na Macron yanaharibu juhudi zao."

Shukrani za Macron ziko wapi?

Juste Codjo, profesa msaidizi wa masomo ya usalama katika Chuo Kikuu cha New Jersey City, aliambia DW kuwa haoni sababu yoyote ya kuhalalisha kauli za Macron. Codjo, ambaye aliwahi kuhudumu katika jeshi la Benin kwa miaka 20, alisema kuwa, kwa mfano, kupelekwa kwa vikosi vya Ufaransa katika eneo la Sahel kuanzia mwaka 2013 hakukuwa msaada wa bure, bali kulilenga maslahi ya kitaifa ya Ufaransa.

Soma pia: Togo "Koloni la Mfano"

"Hili pia ni upuuzi kutoka katika mtazamo wa kihistoria," alisema Codjo. "Macron anaonekana kusahau kuwa Waafrika walilazimishwa kupigana kwa niaba ya Ufaransa wakati wa Vita vya Kwanza na vya Pili vya Dunia, pamoja na vita vya ukoloni katika ukanda wa Indo-Pasifiki na sehemu nyingine."

Codjo alisema, "Afrika imetoa mchango mkubwa sana katika kudumisha nguvu za Ufaransa" katika nyanja za uchumi, jeshi, diplomasia na utamaduni.

Wanajeshi wa Kiafrika wa Senegal ("Tirailleurs") | Uhusiano wa Macron na Afrika
Wanajeshi wa Kiafrika wa Senegal waliopigana kama "tirailleurs" walipigana kwa ushindi wakiwa bega kwa bega na Ufaransa katika vita viwili vya dunia.Picha: The Print Collector/Heritage-Images/picture alliance

"Ufaransa isingekuwa ilipo leo bila michango ya Afrika, michango ambayo haijawahi kulipwa kwa haki na Ufaransa," alisema. "Kwa hiyo, labda Rais Macron anapaswa tu kukaa kimya na kusema: 'Asante Afrika kwa kuturuhusu kusimama juu ya mgongo wenu."

Shinikizo la ndani kwa Macron

Ufaransa imepoteza wanajeshi 58 katika eneo la Sahel tangu kuanza kwa operesheni hiyo miaka kumi iliyopita. Kulingana na wanadiplomasia, Macron alikatishwa tamaa na kushindwa kwa operesheni hiyo kuleta utulivu katika eneo hilo, alisema Lisa Louis, mwandishi wa DW jijini Paris.

"Hata hivyo, sera za kigeni ndiyo eneo pekee ambalo Macron bado anaweza kudai kuwa ni mafanikio yake," alisema Louis. "Baada ya uchaguzi wa mapema, chama chake siyo tena kundi kubwa zaidi bungeni."

Soma pia: Vikosi vya Ufaransa vyaanza kuondoka Niger

Waziri mkuu mpya anatoka katika kambi nyingine ya kisiasa, jambo ambalo limemwacha Macron akiwa na ushawishi mdogo katika ajenda ya serikali.

"Ni vigumu kuamini kuwa matamshi haya yataongeza umaarufu wa rais aliyeishiwa nguvu," Louis alisema.

Urathi wa ukoloni wa Ufaransa

Nchi ishirini za Afrikazilipata uhuru kutoka Ufaransa, 14 kati ya hizo zilipata uhuru mnamo mwaka wa "Afrika" wa 1960 pekee.
Hata hivyo, Ufaransa iliendelea kuwa na ushawishi mkubwa katika nchi hizo huru ikilinganishwa na madola mengine ya kikoloni. Nchi nyingi bado zinatumia mojawapo ya matoleo mawili ya Franc CFA kama sarafu yao, ambazo zote zimefungwa thamani yake na euro, iliyorithi faranga ya Ufaransa.

Mnamo 1960, Guinea ilifuta matumizi ya Franc CFA na kuanzisha Franc ya Guinea, hali iliyoibua kisasi kutoka Ufaransa: Idara za ujasusi za Ufaransa zilijaribu kudhoofisha sarafu hiyo mpya kwa kusambaza noti bandia.

Mpiganaji Vita II Dunia, anahisi kutelekezwa na Ufaransa

Ufaransa pia imekuwa ikihusika katika masuala ya kiusalama ya baadhi ya koloni zake za zamani: Jeshi la Ufaransa liliendesha shughuli zake kutoka kambi mbalimbali kote Afrika.

Hata hivyo, ushawishi wa Ufaransa umekuwa ukipungua: Baada ya mfululizo wa mapinduzi ya kijeshi, nchi za Sahel kama Mali, Burkina Faso, na Niger zilikomesha ushirikiano wao wa muda mrefu na Ufaransa na kuanza kushirikiana na Urusi kama nguvu mpya ya ulinzi.

Ingawa vikosi vya Urusi huenda visiwe suluhisho la muda mrefu dhidi ya waasi, vinathaminiwa kama hatua ya muda inayoweza kuleta utulivu.

Au Revoir, France

Gabon na Djibouti sasa ndizo zitakazosalia kama kambi za mwisho za jeshi la Ufaransa barani Afrika: Mwishoni mwa mwaka 2024, Senegal na Chad zilitangaza kukomesha ushirikiano wao na mkoloni huyo wa zamani. Kambi ya kwanza nchini Chad tayari imefungwa.

Rais wa Ivory Coast, Alassane Ouattara, alitoa tangazo sawa katika hotuba yake ya Mwaka Mpya.

"Ufaransa haijarudi nyuma," Macron aliwaambia mabalozi wake. "Tunajipanga upya tu."

"Kwa kuwa sisi ni wastaarabu," alisema Macron, "tuliwaacha wao watangaze kwanza."

Rais wa Chad, Mahamat Idriss Deby Itno, alisema kuondoka kwa Ufaransa ni uamuzi wa uhuru uliofanywa na Chad.

"Ningependa kueleza hasira yangu kuhusu matamshi ya hivi karibuni ya Rais Macron, ambayo ni dhihaka kwa Afrika na Waafrika," alisema Deby. "Nadhani yuko katika zama zisizo sahihi."

Chad Faya Largeau 2022 | Ufaransa imeanza kurejesha kambi zake kwa Chad
Ufaransa imeanza kurejesha kambi zake kwa Chad.Picha: Aurelie Bazzara-Kibangula/AFP/Getty Images

Codjo, profesa kutoka New Jersey, pia haamini kuwa Senegal na Chad zilishauriana na Ufaransa kabla ya kufanya maamuzi hayo.

Soma pia: Chad yamshutumu Macron kwa kuwadharau Waafrika

"Kinyume chake, kuna uwezekano mkubwa kwamba Côte d'Ivoire ilishinikizwa na Macron," alisema Codjo. "Kuondoka Côte d'Ivoire na kumshinikiza Rais Ouattara kukubali kuondoka kwa wanajeshi wa Ufaransa huenda ilikuwa mbinu ya kimkakati, baada ya kuwa dhahiri kwa Macron kuwa uwepo wa Ufaransa haukubaliwi tena Senegal na Chad."

Ivory Coast bado ina takriban wanajeshi 600 wa Kifaransa. Kambi hiyo sasa itarejeshwa kwa jeshi la kitaifa. Katika hotuba yake ya Mwaka Mpya, Ouattara aliwaambia wananchi wake wajivunie jeshi lao, "ambalo sasa limeimarishwa rasmi."