1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kashmir: Khan aapa 'kupambana hadi mwisho'

Bruce Amani
14 Agosti 2019

Waziri Mkuu wa Pakistan Imran Khan leo ameituhumu India kupanga shambulizi kwenye eneo la jimbo la Kashmiri linalodhibitiwa na Pakistan na kuonya kuwa nchi yake itajibu mara moja iwapo hilo litatokea

https://p.dw.com/p/3Ntnr
Pakistan Imran Khan in Kaschmir
Picha: AFP/Getty Images

Wakati wa hotuba yake mbele ya bunge la eneo la Kashmir linalotawaliwa na Pakistan, Khan amesema jeshi la nchi hiyo liko tayari kujibu kitisho cha India na kumuonya waziri mkuu Narendra Mondi dhidi ya mipango ya kuishambulia Kashmir. Amesema Waziri Mkuu wa India Narendra Modi na chama chake cha BJP amefanya kosa kubwa la kimkakati na kuitumia karata yake ya mwisho "Sasa ulimwengu mzima unaitazama Kashmir na sasa inategemea na namna Pakistan itakavyolishughulikia suala hilo kimataifa. Mbele ya bunge lenu, nachukua dhamana na nitaipaza sauti ya Wakashmiri mbele ya ulimwengu. Nitakuwa balozi wa Kashmir.

Onyo la Khan linakuja siku chache tangu India ilipotangaza uamuzi wa  kuifuta hadhi maalum ya jimbo linalogombaniwa la Kashmir, hatua ambayo Pakistan imeitaja kuwa kinyume cha sheria.

Indien Pakistan Kaschmir Unruhen
Jimbo la Kashmir limewekwa chini ya ulinzi mkaliPicha: AFP/STR

Pakistan ilijibu hatua hiyo kwa kupunguza uhusiano wakidiplomasia na India, kusitisha biashara ya pamoja na kuzuia shughuli za usafiri kati ya mataifa hayo jirani.

Khan alilitembelea jimbo la Kashmir leo kuonyesha mshikamano na watu wake, wengi wao wakiwa wameathirika na hali ya usalama mkali ambayo iliwekwa baada ya uamuzi wa India wiki iliyopita.

Wakati huo huo, Gavana wa Kashmir Satya Pal Malik amesema vikwazo vya kusafiri katika jimbo hilo vitaondolewa kesho Alhamisi baada ya sherehe za leo za Siku Kuu ya Uhuru. Ijapokuwa amesema mawasiliano ya simu na mtandao wa intaneti vitaendelea kufungwa.

Huku hayo yakijiri, Pakistan imeutaka Umoja wa Mataifa kuitisha kikao cha dharura cha Baraza lake la Usalama kuhusiana na mzozo huo wa Kashmir.

Waziri wa Mambo ya Nchi za Kigeni wa Pakistan Shah Mehmood Qureshi amesema katika barua kwa Baraza la Usalama kuwa hali ya sasa inaweka kitisho kikubwa kwa amani na usalama wa kimataifa.

Rais wa Pakistan Arif Alvi pia aliilaani hatua hiyo ya India leo na kuiomba jamii ya kimataifa kuingilia kati. Nchi hizo jirani za Kusini mwa Asia Pakistan na India zimepigana vita mara tatu tangu zilizopopata uhuru kutoka kwa utawala wa kikoloni wa Uingereza mwaka wa 1947, ambapo vita viwili vilihusu jimbo la Kashmir.