Kansela Angela Merkel apokea tuzo ya ′Taa ya Amani′ | Matukio ya Kisiasa | DW | 12.05.2018
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

ITALIA

Kansela Angela Merkel apokea tuzo ya 'Taa ya Amani'

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel ametunukiwa tuzo ya Fransisca ya ‘'Taa ya Amani". Bibi Merkel amepewa tuzo hiyo kutokana na juhudi zake za kuhamasisha ushirikiano na amani miongoni mwa watu.

Wakati akipokea tuzo hiyo kansela wa Ujerumani Angela Merkel alisema njia ya amani na maridhiano mara nyingi hufaulu pale panapokuwa na jitihada na uvumilivu mwingi, na alisisitiza kuwa njia hiyo sio kizuizi cha imani ya kidini.

Akitolea mfano matatizo katika Umoja wa Ulaya unaojumuisha mataifa 28, bibi Merkel amesema ni muhimu kuangalia mbali zaidi ya upeo wa kitaifa, na kuongeza kuwa ni lazima uwepo uwezekano wa kuupa moyo Umoja wa Ulaya.

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel(Reuters/Y. Nardi)

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel

Kansela wa Ujerumani alielezea juu ya amani na jinsi inavyoendelea kuwa dhaifu duniani, akitolea mfano vita vya Balkans, iliyokuwa zamani Yugoslavia kwenye miaka ya tisini.Pia alizungumzia hatua ya Urusi ya kulitwaa jimbo la Crimea  mnamo mwaka 2014 pamoja na vita vya hivi karibuni vya wenyewe kwa wenyewe vya nchini Syria ambavyo amesema vimesababisha mgogoro mkubwa zaidi wa kibinadamu katika nyakati hizi za sasa. 

Kansela Merkel alizungumzia pia juu ya hatua ya rais wa Marekani Donald Trump ya kuiondoa nchi yake na kuiweka kando na mataifa makubwa kuhusiana na mkataba wa nyuklia wa Iran uliofikiwa mwaka 2015, maamuzi ambayo Merkel amesema yatalitumbukiza zaidi kwenye migogoro eneo la Mashariki ya Kati.

Rais wa Marekani Donald Trump (Getty Images/AFP/S. Loeb)

Rais wa Marekani Donald Trump

Tuzo hiyo ya "taa ya Amani"  ya Fransica ni mfano wa taa ya mafuta ya kioo inayowaka kwenye kaburi la mtakatifu Francis wa Assisi aliyeishi hadi mwaka 1226 na ambaye jitihada zake za kuwalinda wanyamapori zilihamasisha maadili ya kulinda mazingira.

Rais wa Colombia Juan Manuel Santos alipata tuzo ya amani ya Nobel na tuzo hiyo ya ‘Taa ya Amani' ya Francisca mnamo mwaka 2016 kutokana na jitihada zake zilizoleta upatanishi kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe vya nchini Colombia.

Rais wa Colombia Juan Manuel Santos(Imago/Agencia EFE)

Rais wa Colombia Juan Manuel Santos

Tuzo hiyo ilitolewa kwa mara ya kwanza mwaka 1981 kwa kiongozi wa jumuiya ya wafanyakazi wa Poland Lech Walesa. Wapokeaji waliofuatia baadaye ni pamoja na Papa John Paul wa pili, Dalai Lama, Mama Teresa wa Calcutta na kiongozi wa kisiasa wa Urusi Mikhail Gorbachev.

Mwandishi: Zainab Aziz/p.dw.com/p/2xa1C

Mhariri: Yusra Buwayhid

 

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com