1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN yafunga kambi mbili za wakimbizi wa Mali nchini Niger

Amina Mjahid
6 Agosti 2020

Takriban raia 15,000 wa Mali wamehamishwa kutoka kambi 2 kubwa za wakimbizi Magharibi mwa Niger, mwishoni mwa mwaka wa 2019 ili kuishi katika miji ya karibu na salama kutokana na mashambulizi ya makundi ya itikadi kali.

https://p.dw.com/p/3gWBm
Dürre im Niger
Picha: picture-alliance/dpa

Umoja wa Mataifa umesema kufungwa kwa kambi hizo Desemba 2019 ulikuwa uamuzi wa pamoja wa shirika la wakimbizi la Umoja wa Mataifa na serikali ya Niger na likaharakishwa mwaka jana kufuatia kuzorota kwa hali ya usalama.

Kambi hizo katika maeneo ya Tabarey Barey na Mangaize ziliwahifadhi Wamali wanaokimbia machafuko katika nchi yao tangu mwaka wa 2012. Eneo la Magharibi mwa Niger  hushuhidia mashambilizi ya mara kwa mara ya makundi ya itikadi kali.

Mashambulizi katika kambi za Tabarey Barey na Mangaize yaliwauwa wakimbizi 10 na maafisa wa jeshi la Niger waliokuwa wakitoa ulinzi kati ya 2014 na 2016.