1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kahawa yawainua wazazi wa watoto wa Cerebral Palsy Kenya

22 Aprili 2026

Kilimo cha kahawa nchini Kenya kinageuka kuwa tumaini jipya kwa familia za watoto wenye Cerebral Palsy, zikikabiliana na changamoto za malezi na kujitegemea kiuchumi.

https://p.dw.com/p/5Cdyf
Kenya, Nyeri County | Kilimo cha kahawa na Cerebral Palsy | Godfrey Wanjohi wakati wa uvunaji wa kahawa
Godfrey Wanjohi, mzazi wa watoto wawili wanaoishi na Cerebral Palsy, akihudumia zao lake la kahawa katika eneo la Mathira, Kaunti ya NyeriPicha: Wakio Mbogho

Nchini Kenya, kilimo cha kahawa kimekuwa tegemeo muhimu kwa kundi la wazazi na walezi wa watoto wenye ugonjwa wa Cerebral Palsy. Licha ya kukumbwa na changamoto za kijamii na kiuchumi, kundi hili limeanza kubuni mbinu za kujitegemea kupitia kilimo na biashara ya kahawa.

Kwa familia hizi, ulezi wa watoto wenye hali hiyo ni jukumu la muda wote. Mbali na changamoto za kiafya, wazazi hukumbana na unyanyapaa, lawama na kutengwa na jamii. Nichodemous Muchangi anaeleza kuwa baada ya mtoto wake kuzaliwa na hali hiyo, baadhi ya ndugu walimlaumu, huku wengine wakihusisha hali hiyo na imani za kishirikina.

Hali kama hiyo pia inathibitishwa na Godfrey Wanjohi, ambaye ana watoto wawili wenye ugonjwa huo. Anasema kulea mtoto mmoja mwenye kupooza ubongo ni kazi kubwa inayohitaji nguvu na muda mwingi, sawa na kulea watoto kadhaa kwa wakati mmoja.

Changamoto za kifedha pia ni kubwa. Esther Kariuki anakumbuka walivyowahi kuomba msaada wa kununua mahitaji muhimu kama nepi, lakini badala yake wakahimizwa kutafuta suluhisho la kudumu kupitia shughuli za kiuchumi.

Hatua hiyo ilisababisha kuanzishwa kwa kundi la Cerebral Palsy Warriors Family mwaka 2021, linalowaleta pamoja wazazi na walezi wa watoto wenye hali hiyo. Kundi hilo lina wanachama 66, wengi wao wakiwa wanawake.

Kenya, Nyeri County | Kilimo cha kahawa na Cerebral Palsy | Agnes Wanjiku akinyunyizia dawa mimea yake ya kahawa
Agnes Wanjiku akinyunyizia dawa mimea yake ya kahawa; akiwa mzazi wa mtoto wa miaka 14 anayeishi na Cerebral Palsy, katika eneo la Mathira, Kaunti ya Nyeri County, KenyaPicha: Wakio Mbogho

Kahawa kuwa chanzo cha matumaini

Kahawa, moja ya mazao makuu ya biashara nchini Kenya, imekuwa njia muhimu ya kuwawezesha kiuchumi. Wanachama wa kundi hilo wameanza kuuza kahawa yao kwa pamoja na kutafuta masoko ya moja kwa moja nje ya nchi.

Kwa mujibu wa Esther Kariuki, hatua ya kuondoa utegemezi kwa madalali imeleta mabadiliko makubwa. Anasema hapo awali hawakuwa na uhakika wa mwelekeo wao, lakini sasa wana matumaini kutokana na kupata wanunuzi wa moja kwa moja.

“Tunajivunia kahawa yetu kwa sababu imelimwa na mikono inayowalea watoto wetu,” anasisitiza.

Mafanikio haya yamewezeshwa na msaada kutoka Alliance of Bioversity International and CIAT pamoja na wadau wengine, wakiwemo miradi inayofadhiliwa na GIZ.

Kwa wakulima kama Agnes Wanjiku, maisha ni mchanganyiko wa malezi na kilimo. Anasema huanza siku yake mapema kumhudumia mtoto wake kabla ya kuelekea shambani, huku akiendelea kumuangalia mara kwa mara siku nzima.

Kenya, Nyeri County | Kituo cha Cerebral Palsy Warriors Family kilichopo Mathira
Wahudumu wakisukuma watoto katika kituo cha Cerebral Palsy Warriors Family huko Mathira, Kaunti ya Nyeri County, Kenya.Picha: Wakio Mbogho

Ujumbe wa kijamii kupitia kahawa

Ili kuongeza thamani ya bidhaa yao, wakulima hao wameanzisha nembo maalum ya “Impact PLWD” kwenye pakiti za kahawa, ikionyesha kuwa bidhaa hiyo inatoka kwa watu wanaoishi na ulemavu.

Kwa mujibu wa Brian King, hatua hiyo inawasaidia wakulima kujitambulisha si tu kama wazalishaji, bali pia kama sehemu ya mabadiliko ya kijamii.

“Wanunuzi wanapoona nembo hiyo, wanaelewa kuwa wanachangia moja kwa moja katika kuboresha maisha ya jamii,” anaeleza.

Wakulima hawa wana matumaini kuwa juhudi zao zitachangia pia mabadiliko ya sera, hasa katika kuhakikisha ujumuishaji unazingatiwa katika biashara, mifumo ya usimamizi na kanuni mbalimbali.

Kwa sasa, hadithi yao ni mfano wa jinsi ubunifu na mshikamano vinaweza kusaidia kukabiliana na changamoto kubwa za kijamii na kiuchumi.