Joto la uchaguzi lapanda Uganda | Uganda Yaamua 2016 | DW | 26.01.2016
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Uchaguzi Mkuu Uganda 2016

Joto la uchaguzi lapanda Uganda

Zikiwa zimesaliwa wiki zisizozidi tatu kabla ya Waganda kushuka vituoni kwa ajili ya uchaguzi wa rais na wabunge, joto la uchaguzi huo linazidi kufuka kwenye miji, mitaa na vijiji vya taifa hilo la Afrika ya Mashariki.

Tarehe 18 Februari 2016 imekaribia na kinachoshuhudiwa nchini Uganda hivi sasa ni homa ya uchaguzi. Rais aliyeko madarakani, Yoweri Kaguta Museveni, ameshaitawala nchi hiyo kwa miaka 30. Akiwa na umri wa miaka 71, kiongozi huyo alitumia nafasi yake madarakani kuibadili katiba kuondoa kipengee kinachoweka ukomo wa kutawala, liicha ya kuwahi kusema kwamba hataki kugombea tena. Sasa anasema bado muda wake wa kuondoka madarakani haujafika, suala la ukomo wa madaraka "si jambo muhimu kwa Afrika".

Kuwepo katika kinyan'ganyiro hicho kwa Rais Museveni kunaangaliwa kwa jicho tafauti na hata wengi wa marafiki zake ndani ya chama tawala. Miongoni mwa wapinzani wake katika uchaguzi huo ni rafiki yake wa zamani na mshirika wake wa karibu, Amama Mbabazi, ambaye pia alikuwa waziri mkuu na katibu mkuu wa chama tawala cha NRM. Mbabazi anawania wadhifa wa urais kama mgombea binafsi.

Kawaida, kabla ya uchaguzi kumekuwa kukishuhudiwa mivutano na malumbano baina ya vyama mbali mbali, lakini kwa hivi sasa hali ya mambo ni shwari na Waganda wanasubiri kwa hamu uchaguzi huo. Ukiingia mji wa Kampala kinachoshuhudiwa kila eneo ni mabango ya kampeni, magazeti yamesheheni taarifa za kisiasa, huku redio na televisheni zikisikika kuwa na mijadala mizito kuhusu masuala ya uchaguzi.

Vijana na uchaguzi nchini Uganda.

Vijana na uchaguzi nchini Uganda.

Vijana na uchaguzi

Kimsingi kila kitu katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki kimejiweka katika kuuangalia uchaguzi huo wa mwezi Februari wa bunge na rais. Kila mmoja amekuwa akitoa mtazamo wake juu ya uchaguzi huo huku baadhi kama kijana Francis Kwizera, kijana wa miaka 28, wakitaraji kwamba uchaguzi huo utamuweka madarakani rais mpya.

"Mara hii tunahitaji uchaguzi huru na utakaoleta mabadiliko ya uongozi kwasababu tumekuwa na raisi huyu mmoja kwa kipindi cha miaka 30. Ahadi nyingi hazijatekelezwa na wala hatutegemei kama anaweza kuzitekeleza katika kipindi kingine cha miaka mitano.Hivi sasa ana umri wa miaka 71, mimi nina miaka 28 na sijawahi kuona raisi mwingine katika maisha yangu,'' anasema Francis.

Zaidi ya robo tatu ya raia wa Uganda ni vijana walio chini ya umri wa miaka 30 na wengi ya vijana hawa hawana ajira kama anavyosema Geofrey Murora kijana mwenye umri wa miaka 37 anayefanya kazi kama dereva wa teksi ni vigumu mno vijana kupata ajira.

"Mara nyingi wanaopata ajira ni wale wale wanaotokea kwenye kabila fulani,mimi ni mbaganda lakini wote walioko serikalini ni Wanyankole. kwahivyo kama unataka ajira hata ikiwa ni ya kuwa dereva wa teksi wanachukuliwa wanyankole. Sisi hatuna nafasi," anasema Geofrey.

Si katika suala la ajira tu lakini hata iwe ni kwenye shule, mahospitali na hata mitaani, Waganda wengi wanahisi wameelekezwa na serikali yao. Na hisia hizi zinajitokeza pia hata kwa wagombea wote saba wanaopambana dhidi ya Rais Museveni.

Wagombea wiwili wanaoonekana kuwa na nguvu zaidi kukabiliana na Museveni ni Kizza Besigye ambaye zamani aliwahi kuwa daktari wa Museveni wakati wakiwa vitani na sasa anakiongoza chama cha upinzani cha Forum For Demokratic Change (FDC) na amewahi mara kadhaa kupambana naye katika chaguzi zilizopita na Mbabazi.

Wachambuzi wa mambo wanasema upinzani uliopo hivi sasa ukimjumuisha Mbabazi, unaifanya hali ya kisiasa safari hii kuwa tete kuliko chaguzi zilizopita.

Mwandishi: Saumu Mwasimba /Simone Schlindwein (DW)
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com