1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yawaachia huru wafungwa 19

2 Oktoba 2009

Israel imewaachia huru wafungwa 19 wa KiPalestina kama sehemu ya makubalianao ya kukabidhiwa ukanda wa video ulio na maelezo yanayothibitisha kuwa mwanajeshi wa Israel Gilad Shalit ambaye amekuwa akizuiliwa Gaza yu hai.

https://p.dw.com/p/JwDV
Gari lililowasafarisha wafungwa wa PalestinaPicha: AP

Hatua hiyo imefikiwa baada ya mazungumzo yaliyodumu kwa kiasi cha miaka mitatu chini ya upatanishi wa Misri.Kulingana na Israel kitendo hicho ni ishara ya kuaminiana na Palestina.Jumla ya wafungwa 7200 wa Palestina wanazuiliwa katika magereza ya Israel.

Wanawake 19 wa KiPalestina waliachiwa kutoka jela ya Ha Sharon ya wanawake hii leo kama sehemu ya makubaliano ya kuipa Israel ukanda wa video ulio na maelezo kumhusu mwanajeshi wake Gilad Shalit anayezuiliwa katika Ukanda wa Gaza tangu mwaka 2006.18 kati ya wanawake hao wanaelekea kwenye kambi moja ya jeshi iliyo katika Ukingo wa Magharibi watakakojiunga na familia zao.Mfungwa wa mwisho wa 19 atasafirishwa hadi jela moja iliyo kwenye mji wa kusini wa Ashkelon kisha atahamishiwa hadi eneo la mpaka wa Erez na Ukanda wa Gaza.Kulingana na maafisa wa serikali wa Israel mwanamke mwengine mmoja ataachiwa katika kipindi cha siku chache zijazo.

Ujerumani yatoa mchango mkubwa

Taarifa zinaeleza kuwa Ujerumani iliyojiunga mwezi Julai na majadiliano hayo ya upatanishi ilitoa mchango mkubwa katika tukio hilo la leo.Mohammed aliye mkazi wa Gaza na mume wa mmoja wa wanawake hao walioachiwa anaishukuru serikali ya Ujerumani kwa mchango wao''Ningependa kuishuruku serikali na watu wa Ujerumani kwa juhudi zao zote zilizomuwezesha mke wangu kuachiwa huru.Na nina imani kuwa serikali ya Ujerumani itaendelea na juhudi za kuwaachia wafungwa wengine waliosalia katika harakati za kumaliza mizozo kote ulimwenguni''.

Israel Gaza Palästinenser Hamas Pressekonferenz Gilad Schalit
Wapiganaji wa Hamas katika mkutano na waandishi wa habari,GazaPicha: AP

Kitendo hicho cha kubadilishana wafungwa ni mafanikio makubwa baada ya majadiliano kati ya Hamas na Israel yaliyodumu kwa kiasi cha miaka mitatu chini ya upatanishi wa Misri.Kwa mujibu wa afisi ya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu nchi yake itapokea thibitisho jipya kuwa Gilad Shalit yu hai na yupo buheri wa afya.Thibitisho hilo litakuwa ukanda wa video utakaokabidhiwa Israel na wapatanishi wakuu wa mzozo huo. Kwa upande wao kundi moja lililohusika katika shambulio la kumkamata Gilad Shalit aliye na umri wa miaka 23,ukanda huo wa video una urefu wa dakika moja n ani thibitisho kuwa mwanajeshi huyo yu hai.Gilad Shalit alikamatwa mwezi Juni mwaka 2006 baada ya wapiganaji wa Ukanda wa Gaza wakiwemo Hamas walipokivamia kituo kimoja cha polisi cha Israel na kuwauwa wanajeshi wawili baada ya kupitia kwenye matobwe yaliyotokea eneo la Palestina.Gilad Shalit amekuwa akizuiliwa katika Ukanda wa Gaza bila kuwa na mawasiliano ya aina yoyote na hata wahudumu wa misaada wa shirika la Msalaba Mwekundu hawana ruhusa ya kumtembelea.

Bado kibarua ni kigumu

Hata hivyo Israel imesisitiza kuwa tukio hili la leo ni ishara ya kuaminiana na Hamas ila bado kuna kibarua kigumu katika mchakato mzima wa kusaka amani ya eneo la mashariki ya kati.

Benjamin Netanyahu bei Hosni Mubarak in Kairo
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na Rais wa Misri Hosni Mubarak katika mazungumzo,CairoPicha: AP

Ni mwanamke mmoja tu kati ya wafungwa walioachiwa anayetokea Ukingo wa Magharibi.Hata hivyo hakuna yeyote kati yao anayetuhumiwa kwa kuhusika na mauaji ya moja kwa moja ya Waisraeli hao.Wapiganaji hao wanaaminika kuwa wanachama wa makundi ya Hamas,Fatah,Islamic Jihad na Popular Front for the Liberation of Palestine.

Msichana mmoja wa Kipalestina Braah Mulki aliye na umri wa miaka 15 aliyekuwa kwenye orodha ya mwanzo ya wafungwa watakaoachiwa aliruhusiwa kuondoka jela hapo jana baada ya kifungo chake cha miezi 11 jela kupunguzwa.Mulki alihukumiwa kifungo cha jela baada ya kujaribu kumchoma kisu mwanajeshi mmoja mwaka 2008 kwenye kituo cha kijeshi cha Qalandia cha ukaguzi.Tukio hilo hata hivyo halihusiani na shughuli nzima ya kubadilishana wafungwa.Kundi la Hamas limeitaka Israel kuwaachia wafungwa 1000 dai ambalo mpaka sasa halijatimizwa kikamilifu.Vifungo vya wengi ya wafungwa hao walioachiwa vilikuwa vihitihishwe mwakani au mwaka 2011.

Mwandishi:Thelma Mwadzaya-DPAE/AFPE

Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman