1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroMamlaka ya Palestina

Israel yatuhumiwa kuwaua watu 20 waliokuwa wakisubiri msaada

15 Machi 2024

Wizara ya afya ya ukanda wa Gaza inayodhibitiwa na kundi la Hamas imesema hii leo kuwa watu 20 wameuawa na wengine 155 wamejeruhiwa kufuatia mashambulizi ya Israel.

https://p.dw.com/p/4dart
Gaza- Wakaazi wakipokea msaada huko Rafah
Raia wa Gaza wakipokea msaada wa chakula huko RafahPicha: Ahmad Hasaballah/Getty Images

Watu hao walikuwa wakisubiri kupokea misaada inayohitajika mno katika eneo hilo lililozingirwa, lakini Israel imekanusha taarifa hizo.      

Wizara ya afya huko Gaza imewashutumu wanajeshi wa Israel kwa kufyatua risasi kutoka kwenye "vifaru na helikopta" wakati Wapalestina walikuwa wamekusanyika kaskazini mwa jiji la Gaza.

Mohammed Ghurab, mkurugenzi wa huduma za dharura katika hospitali moja kaskazini mwa Gaza, ameliambia shirika la habari la AFP kwamba " vikosi vya uvamizi" vilifyetua risasi dhidi ya watu waliokuwa wakisubiri msaada wa chakula. Mwandishi wa habari wa AFP aliyekuwa kwenye eneo la tukio alishuhudia miili kadhaa pamoja na watu waliokuwa wamepigwa risasi.   

Jeshi la Israel hata hivyo limekanusha kuwafyetulia risasi watu hao  na kusema kuwa taarifa hizo ni za uongo na kuongeza kuwa "inatathmini tukio hilo kwa umakini."

Misaada muhimu ya chakula yawasili Gaza

Hayo yanajiri wakati Umoja wa Mataifa ukionya juu ya tishio la njaa huko Gaza. Juhudi za kuwasilisha chakula na misaada mingine zimeongezeka, zikiwemo za angani na baharini kwa kupitia katika nchi za Jordan, Israel na Misri.

Mashuhuda wamesema meli ya misaada ya Uhispania ya Open Arms, iliyosheheni takriban tani 200 za chakula kilichotolewa na shirika lisilo la kiserikali la Marekani World Central Kitchen (WCK), imewasili katika pwani ya Gaza mchana wa leo. Abu Issa Ibrahim Filfil ni mkaazi wa Gaza anasema wanausubiri mno msaada huo kwa maana watu wanakufa njaa na anataraji kuwa msaada huo utawatosheleza:

Cyprus | Meli ya misaada ya Open Arms ikijiandaa kuelekea Gaza
Meli ya misaada ya Uhispania ya Open Arms, iliyosheheni takriban tani 200 za chakula kilichotolewa na shirika lisilo la kiserikali la Marekani World Central Kitchen (WCK), ikijiandaa kuondoka kutoka bandari ya Larnaca nchini Cyprus kuelekea Gaza: 12.03.2024Picha: AFP

"Nahitaji msaada kwa ajili ya watoto wangu. Nataka waishi na wasife kwa njaa. Wamekuwa wakila mimea ya porini, hakuna mkate. Hakuna chakula hapa Gaza. Namaanisha, huu ni mwezi wa Ramadhani, na hakuna kitu. Kila kitu ni ghali sokoni na hakuna bidhaa. Unaona hali hii baada ya miezi mitano au sita ya vita. Hata kama kungelikuwa na bidhaa, basi hakuna pesa ya manunuzi. Kwa mapenzi ya Mungu wataleta chakula cha watoto, hilo ndilo tunaloomba."

Soma pia: Meli ya misaada kutoka Cyprus taratibu yakaribia Gaza

Lakini mapigano makali yanaendelea baada ya wapatanishi kushindwa kufikia makubaliano ya usitishwaji mapigano katika kipindi hiki cha mwezi mtukufu wa Waislamu wa Ramadhan.

Rais wa Misri Abdel Fattah al-Sisi
Rais wa Misri Abdel Fattah al-Sisi akihutubia mkutano wa kilele wa kundi la G20Picha: John Macdougall/AP Photo/picture alliance

Rais wa Misri Abdel Fattah al-Sisi amesema leo Ijumaa kuwa nchi yake inaendelea na juhudi za kujaribu kufikiwa kwa mpango wa kusitisha mapigano huko Gaza, kuruhusu misaada zaidi na kuwawezesha watu waliohamishwa kusini kurejea eneo la Kaskazini. Al-Sisi ameonya pia dhidi ya hatari ya uvamizi wa Israel katika mji wa Rafah, ambako ni kimbilio la watu wanaokadiriwa kufikia milioni 1.5.  

Soma pia: Bado hakuna mwelekeo wa amani kati ya Israel na Hamas

Kundi la Hamas limewasilisha kwa wapatanishi pamoja na Marekani, pendekezo la mpango wa kusitisha mapigano linalohusisha kuachiliwa kwa mateka wa Israel wakiwemo wanawake, watoto, wazee, na mateka wagonjwa. Lakini pia kundi hilo linahitaji kuachiliwa kwa wafungwa kati ya 700-1000 wa Kipalestina.

Ofisi ya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ilisema hapo jana kuwa pendekezo jipya lililowasilishwa na Hamas bado limegubikwa na kile walichokitaja kuwa "matakwa yasiyotekelezeka."

(Vyanzo: Mashirika)