1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Meli ya misaada kutoka Cyprus taratibu yakaribia Gaza

14 Machi 2024

Meli ya kwanza yenye tani 200 za chakula cha msaada taratibu inaelekea Ukanda wa Gaza leo, wakati juhudi za kupelekea misaada ya kiutu katika mamlaka ya Palestina iliyozingirwa na Israel zikiendelea

https://p.dw.com/p/4dW3A
Meli ya Uhispania |Open Arms
Meli ya shirika la misaada la Uhispania, Open Arms inayopeleka chakula Gaza Picha: Yiannis Kourtoglou/REUTERS

Meli hiyo ya shirika la misaada la Uhispania, Open Arms, inatokea Cyprus na ndiyo ya kwanza kutumia njia ya baharini iliyobuniwa kupelekea misaada Gaza. Itakapowasili karibu na Gaza, misaada hiyo itapakuliwa katika bandari ndogo iliyoundwa na shirika la misaada la Marekani World Central Kitchen, ambalo litaisambaza misaada hiyo.

Huko Gaza City, Wapalestina waliokata tamaa wanasubiri kuwasili kwa meli hiyo ambayo huenda ikachukua siku kadhaa kufika.

Msaada taratibu unaingia Ukanda wa Gaza japo Israel inaendelea na mashambulizi katika eneo hilo.

Kufikia sasa juhudi za upatanishi hazijafanikiwa kusitisha mapigano yaliyochochewa na shambulizi la Oktoba 7 dhidi ya Israel, lililofanywa na wanamgambo wa Hamas.

Waziri wa ulinzi wa Israel Yoav Gallant ameapa kwa mara nyengine tena kwamba vikosi vya Israel vitafika kila eneo ili kutimiza lengo lao la kulisambaratisha kundi la Hamas.