1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yapokea miili ya mateka wawili zaidi kutoka kwa Hamas

19 Oktoba 2025

Serikali ya Israel imesema leo kuwa Hamas imekabidhi mabaki zaidi ya mateka wa Israel, huku kucheleweshwa kupatikana kwa miili iliyozikwa chini ya vifusi katika eneo la Gaza kukitishia makubaliano ya usitishaji vita.

https://p.dw.com/p/52EkN
Israel Tel Aviv 2025 | Maandamano ya kutaka kurejeshwa kwa mateka wa Israel
Maandamano ya kutaka kuachiwa kwa mateka wa Israel Gaza mjini Tel Aviv, IsraelPicha: Fadel Senna/AFP

Kitengo cha kijeshi cha Hamas kinachojulikana kama Ezzedine Al-Qassam, kilikabidhi mabaki ya mateka wawili jana Jumamosi usiku kama sehemu ya makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyosimamiwa na Marekani.

Ofisi ya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu imethibitisha kuwa Shirika la Msalaba Mwekundu lilipokea mabaki hayo na kuyakabidhi kwa wanajeshi wa nchi hiyo kwa utambulisho.

Hamas yadaiwa kupanga mashambulio dhidi ya raia wa Gaza

Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imesema kuwa ina ripoti za kuaminika kwamba Hamas inapanga shambulio dhidi ya raia huko Gaza, na ikaonya kwamba itakuwa ukiukaji wa makubaliano hayo ya amani.

Katika taarifa, wizara hiyo imesema ikiwa Hamas itafanya shambulizi hilo, hatua zitachukuliwa kuwalinda watu wa Gaza na kudumisha uadilifu wa makubaliano hayo bila ya kutoa ufafanuzi zaidi.