1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yaimarisha ulinzi

Aboubakary Jumaa Liongo16 Septemba 2011

Israel imeimarisha ulinzi, katika Ukingo wa magharibi mnamo wakati ambapo wapalestina wanafanya maandamano makubwa kushajiisha dhamira yao ya kutaka kuwasilisha kwenye Umoja wa Mataifa uanachama kamili wa umoja huo.

https://p.dw.com/p/12ae7
PRais wa Palestina Mahmoud AbbasPicha: dapd

Radio ya Israel imearifu kuwa askari wa ziada wamepelekwa kwenye eneo hilo, kukabiliana na ghasia zinazoweza kutokea, ambapo tayari kiasi cha askari 1500 wamekusanywa na kupelekwa kwenye maeneo yanayokaliwa na Israel.

Jeshi la Israel nalo limeimarisha ulinzi kuzunguka makaazi ya walowezi katika ukingo wa magharibi, kwa ajili ya kuwalinda walowezi hao wa kiyahudi pamoja na kuzuia walowezi hao kuwashambulia wapalestina.

Msemaji wa jeshi hilo amesema vurugu na mapigano ya hapa na pale yaliibuka hii leo nje kidogo ya kitongoji cha Kusra kati ya wakaazi wa eneo hilo na watu wengine kutoka jirani na makaazi ya walowezi ya Esh Hakodesh.

Mapema wapalestina walisema kuwa walowezi kadhaa wa kiyahudi walijaribu kuingia katika kitongoji hicho cha Kusra, lakini walizuiwa na wakaazi wa eneo hilo wakihofu kuwa walitaka kushambuliwa hivyo wakaanza kuwapiga. Mpalestina mmoja na mlowezi mmoja walijeruhiwa katika mapigano hayo.

Walowezi wa kiyahudi kwa mujibu wa msemaji huyo wa jeshi la Israel, wamepanga kuandamana kuelekea katika miji ya wapalestina iwapo wapalestina nao wataandamana katika maeneo yao wanayoyakalia kimabavu.

Yaakov Katz ambaye ni mbunge mwenye msimamo mkali katika bunge la Israel, amesema kuwa wamepanga kuandama kwa amani katika miji ya Nablus, Ramallah au Hebron.

Siku mbili zilizopita kuta za msikiti mmoja pamoja na majengo ya chuo kikuu huko Birzeit karibu na Ramallah yalichorwa maandishi ya kumkashifu kiongozi wa waislamu, Mtume Muhammad SAW, pamoja na maandishi ya kuuawa kwa waarabu, matukio ambayo yanahisiwa kufanywa na walowezi wa kiyahudi.

Rais wa Mamlaka ya ndani ya Palestina Mahmoud Abbas leo alitarajiwa kuwahutubia wapalestina kabla ya kuelekea New York Marekani wiki ijayo kuwasilisha ombi hilo la kutaka uanachama kamili.

Maafisa wa Israel wamenukuliwa wakielezea wasiwasi wao kuwa iwapo hatua hiyo ya Palestina itafanikiwa, basi huenda wakaamua kuchukua hatua za kisheria kuhusiana na suala la makaazi ya walowezi.

Katika mkutano wake na wajumbe maalum kutoka Marekani, Umoja wa Ulaya, Urusi na Umoja wa Mataifa, ikiwa ni kundi la pande nne linalolishughulikia suala la Mashariki ya kati , Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alielezea shaka hiyo.

Marekani ambayo ni mshirika mkubwa wa Israel inapinga hatua hiyo ya Palestina ikisema kuwa hatua kama hiyo ni lazima ipitie njia ya majadiliano kwanza.

Mwandishi:Aboubakary Liongo/AP

Mhariri:Josephat Charo