1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran yalaani uchunguzi wa Baraza la Haki za Binaadamu la UN

25 Novemba 2022

Wizara ya mambo ya nje ya Iran imelaani uamuzi wa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa la kuchunguza majibu yaliyotolewa na jamhuri ya Kiislamu kwa machafuko yaliyozuka kufuatia kifo cha Mahsa Amini.

https://p.dw.com/p/4K5Hw
Iran I Präsident Ebrahim Raisi
Picha: Iranian Presidency/ZUMAPRESS/picture alliance

Tehran ilikuwa imepinga kufanyika kwa kikao cha dharura cha baraza hilo siku ya Alhamisi kama ilivyoombwa na Ujerumani na Iceland. Ilikataa kabisa azimio ambalo lilipitishwa Ijumaa hii la kuanzishwa tume ya kutafuta ukweli kwa matukio ya ukandamizaji dhidi ya waandamanaji nchini Iran.

Iran imeshuhudia maandamano kwa zaidi ya miezi miwili yaliyochochewa na kifo cha mwanamke mwenye umri wa miaka 22 raia wa Kikurdi Mahsa Amini. Alikuwa amekamatwa kwa madai ya kukiuka sheria kali za mavazi ya wanawake nchini humo.

Soma zaidi: UN yaitaka Iran kusitisha kamatakamata ya waandamanaji

Iran Mahsa Amini Proteste in Tehran
Maandamano ya kupinga kifo cha Mahsa Amini mjini Tehran, Iran.Picha: ZUMAPRESS.com/picture alliance

Maafisa wa serikali wameyashutumu mataifa ya kigeni kwa kuchochea machafuko hayo ambayo yanachukuliwa kama uvunjaji wa sheria. Wizara ya mambo ya nje ilisema Iran tayari imeunda tume ya kitaifa ya uchunguzi inayowahusisha wataalamu wa sheria na "wawakilishi huru".

Taarifa ya Wizara hiyo imebaini kuwa kuundwa kwa utaratibu wowote mpya wa kuchunguza matukio ya miezi miwili iliyopita nchini Iran ni kazi bure na inamaanisha ukiukaji wa mamlaka ya kitaifa ya nchi hiyo ya Kiislamu.

Tehran yapinga azimio hilo

Iran imesema "haiutambui ujumbe huo". Idadi kubwa kuliko ilivyotarajiwa ya baraza hilo lenye wanachama 47 waliunga mkono kuanzishwa kwa uchunguzi huo. Nchi 25 zilipiga kura ya Ndio, nchi 16 zilijizuia kupiga kura huku nchi 6 pekee ambazo ni Armenia, China, Cuba, Eritrea, Pakistan na Venezuela zikipinga hatua hiyo.    

Soma zaidi: Umoja wa Mataifa walaani ukandamizaji wa Iran

Iran | Kommandeure der Revolutionsgarde der Islamischen Republik
Kiongozi Mkuu wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei.Picha: khamenei.ir

Tehran iliishutumu Ujerumani na nchi nyingine ambazo ziliunga mkono azimio hilo kwa kutoa "madai ya uwongo na ya uchochezi kuhusu ukiukaji wa haki za wanaume, wanawake na watoto, madai ambayo Iran inayakanusha.

Wizara ya mambo ya nje ya Iran imedai kuwa azimio hili lilitolewa kwa shinikizo kutoka kwa makundi fulani ya kisiasa ambayo yanategemea habari za uongo zinazoenezwa na vyombo vya habari vinavyoipinga Iran.

Soma zaidi: Iran yazishutumu nchi za kigeni kwa machafuko yanayoendelea

Dänemark | Iran-Protest in Kopenhagen
Picha ya msichana Mahsa Amini aliyeuawa na Polisi wa maadili wa IranPicha: Thibault Savary/Le Pictorium/MAXPPP/picture alliance

Iran imeshutumu na kusema ni kosa la kimkakati la Ujerumani na nchi fulani za Magharibi na kwamba "upofu huo utakuwa na madhara kwa maslahi yao".

Wakati wa kikao cha Alhamisi, mkuu wa haki za Umoja wa Mataifa Volker Turk alisisitiza kuwa matumizi ya nguvu yasiyo ya lazima na yasiyo na usawa lazima yakomeshwe.

Turk alisema zaidi ya watu 300 wameuawa tangu kifo cha Amini na aliwaambia waandishi wa habari kwamba alijitolea kuitembelea Iran lakini hakupata jibu kutoka Tehran.