1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran, IAEA wafikia makubaliano ya muda kuhusu nyuklia

22 Februari 2021

Iran itaanza kuwapa wakaguzi wa Umoja wa Mataifa nafasi ndogo ya kuuchunguza mpango wake wa nyuklia kama sehemu ya shinikizo lake kwa nchi za Magharibi, ijapokuwa wachunguzi wataweza bado kufuatilia shughuli za Iran. 

https://p.dw.com/p/3pg6M
Iran I International Atomic Energy Agency (IAEA)
Picha: STR/AFP/Getty Images

Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Nishati ya Atomiki - IAEA Rafael Grossi ametangaza alichokiita kuwa ni "suluhisho la muda" la kuruhusu kuendelea kwa ukaguzi wa vinu vya nyuklia vya Iran baada ya siku kadhaa za mazungumzo na maafisa wa Iran hatua inayotoa muda kidogo wa kufanyika mazungumzo ya kidiplomasia kuhusu suala la nyuklia la Iran.

Soma pia: Iran yaitaka Marekani kuiondolea vikwazo

Hata hivyo, amekiri kuwa chini ya mpango huo mpya wa miezi mitatu, IAEA haitakuwa na kiwango sawa cha ruhusa, mara tu sheria mpya itakapoanza kutekelezwa kesho ikilenga kuzuia ukaguzi wa baadhi ya maeneo. "Matumaini yangu, matumaini ya IAEA, yamekuwa ni kuituliza hali ambayo ilikuwa mbaya zaidi. Na nadhani maelewano haya ya kiufundi yanatimiza hilo ili mazungumzo mengine ya kisiasa katika viwango vingine yafanyike, na muhumu zaidi tunaweza kuepuka hali ambayo tungejikuta ndani, yaani...kusafiri kwa kubahatisha:" Amesema Grossi.

Iran I International Atomic Energy Agency (IAEA)
Mkuu wa IAEA Rafael Grossi akiwa IranPicha: Hadi Zand/WANA/REUTERS

Ziara ya Grossi nchini Iran ilikuja wakati kukiwa na juhudi zilizoimarishwa kati ya utawala wa Rais wa Marekani Joe Biden, madola ya Ulaya na Iran ili kuunusuru mkataba wa nyuklia wa 2015 ambao umekuwa ukingoni mwa kuvunjika tangu Donald Trump alipojiondoa na kutangaza vikwazo dhidi ya Iran.

Soma pia: Ulaya na Marekani kujadili utata wa mkataba wa Iran

Desemba mwaka jana, bunge la Iran linalodhibitiwa na wahafidhina lilipitisha sheria inayotaka kusitishwa kwa ukaguzi wa maeneo Fulani kama Marekani itashindwa kuondoa vikwazo kufikia jana Jumapili.

Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran – IAEO limesema chini ya mpango huo wa muda, kwa miezi mitatu Iran itarekodi na kuhifadhi taarifa za baadhi ya shughuli zake na vifaa vya ufuatiliaji.

Taarifa ya shirika hilo imesema wakati wa kipindi hicho, IAEA haitapewa taarifa hizo, lakini itaweza kuruhusu upatikanaji wa taarifa hizo kama vikwazo vitaondolewa kabisa katika miezi mitatu, la sivyo taarifa hizo zitafutwa milele.

Biden amedhamiria kujiunga tena na mazungumzo kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran ikiwa ni kuondokana na sera ya Trump ya "shinikizo kubwa” kuelekea jamhuri hiyo ya Kiislamu.

Mkurugenzi wa kisiasa wa Umoja wa Ulaya Enrque Mora amependekeza mkutano usio rasmi unaoihusisha Iran, huku Marekani ikikubali kimsingi. Iran imesema inalitathmini pendekezo hilo, na kulijadili na marafiki na washirika wake China na Urusi.

Wakati huo huo, rais Recep Tayyip Erdogan wa nchi jirani Uturuki, amesema kuna fursa ya kuondolewa vikwazo vya Iran, akiita hatua hiyo kuwa ”halali na ya kimantiki.”

afp