1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran yaitaka Marekani kuiondolea vikwazo

19 Februari 2021

Iran imeitolea mwito Marekani kuiondolea vikwazo vilivyowekwa na rais wa zamani Donald Trump kabla ya kuanza kwa mazungumzo ya nyuklia kati ya Iran na Marekani.

https://p.dw.com/p/3pbzf
Iran Revolutionsgarden Übung Ballistische Raketen
Picha: Irgc Official Webiste via Zuma/picture alliance

Utawala wa Biden umesema uko tayari kufanya mazungumzo na Iran pamoja na mataifa nyenye nguvu ulimwengu kujadili kurudi katika makubaliano ya nyuklia ya mwaka 2015.

Kupitia mtandao wa Twitter msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa Iran, Saeed Khatibzadeh aliandika  "Hakuwezi kuwa na mkutano wa nyuklia na Marekani kwa sababu imejiondoa katika makubaliano ya nyuklia ya Vienna. "

Wakati huo huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Mohammad Javad Zarif alituma mtandaoni ujumbe akitumia Hashtag ya iCommitActMeet, ambayo wizara ya mambo ya nje ilielezea kuwa ikiwa Marekani itatimiza jukumu lake la kuiondolea vikwazo, Iran itakuwa tayari kwa mkutano na Marekani na nchi zingine tano ambazo zilishughulikia makubaliano ya nyuklia ya 2015 na Iran.

Österreich Unterzeichner von Atomabkommen sprechen mit dem Iran in Wien
Picha: Reuters/European Commission

Marekani kwa upande wake imeonyesha nia yake ya kukubali mwaliko wa Umoja wa Ulaya ili kujadili juu ya mpango wa nyuklia wa Iran.

Urusi imeunga mkono hatua za mwanzo zilizochukuliwa na Marekani kutafuta maelewano juu ya makubaliano hayo. Msemaji wa Ikulu ya urusi, Dmitry Peskov amewaambia waandishi wa habari ni "jambo zuri" kwamba Washington haitoi tena vikwazo vya kimataifa juu ya Iran na kuhimiza kuwa juhudi zaidi zinahitajika.

Utawala wa Biden jana Alhamisi ulipendekeza mazungumzo na Iran yatakayoongozwa na washirika wa Ulaya na ulichukua hatua mbili muhimu dhidi ya Tehran zilizowekwa na Trump. Hatua hizo ni pamoja na kuondoa wito wa vikwazo vya kimataifa kwa Iran na kuondolewa kwa vizuizi vikali kwa wanadiplomasia wa Iran huko New York.

Israel Netanjahu
Benjamin NetanyahuPicha: Yonatan Sindel/AP/picture alliance

Taarifa kutoka ofisi ya Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu inaendelea kushinikiza Iran kutounda silaha za nyuklia. Israeli inaamini kwamba kurudi kwenye makubaliano ya zamani kutaipa Iran nafasi kubwa zaidi katika zana za kinyuklia.

Netanyahu ni mkosoaji mkuu wa makubaliano ya nyuklia ya 2015 yaliyofikiwa kati ya Iran, Marekani na nchi zengine tano zenye nguvu za ulimwengu, na anaituhumu serikali ya Iran kuwa haijawahi kufuata makubaliano yaliyoafikiwa na imekuwa ikiendelea na kutengeneza silaha za nyuklia kwa siri.

dpa/AP