IMF yatoa mwelekeo wa uchumi wa dunia | Matukio ya Kisiasa | DW | 16.01.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

IMF yatoa mwelekeo wa uchumi wa dunia

Mkuu wa shirika la fedha la kimataifa IMF, Christine Lagarde amesema kushuka kwa bei za mafuta na kuimarika kwa uchumi wa Marekani havitatosha kuboresha mwelekeo wa uchumi wa dunia mwaka huu wa 2015.

Mkuu wa IMF Christine Lagarde.

Mkuu wa IMF Christine Lagarde.

Lagarde alisema wakati mafuta ya bei nafuu yatasaidia watumiaji katika sehemu nyingi za dunia, Marekani ndiyo itakayo kuwa nchi pekee yenye uchumi mkubwa itakayoepukana na udhaifu katika sekta ya uwekezaji na ununuzi.

Katika hotuba inayoangazia ripoti ya IMF kuhusu matarajio ya uchumi wa dunia, inayotarajiwa kutolewa wiki ijayo, Lagarde alisema kanda inayotumia sarafu ya euro na Japan zingali katika hatari ya kutwama katika kipindi cha muda mrefu cha ukuaji dhaifu na mfumko hatari wa bei.

Mtambo wa kuzalisha mafuta wa Yuko katika eneo la Siberia Magharibi nchini Urusi.

Mtambo wa kuzalisha mafuta wa Yuko katika eneo la Siberia Magharibi nchini Urusi.

Hatari ya kupungua ukuaji wa uchumi

Kitisho cha kupunguza fedha kwenye mzunguko, kushuka kwa bei za bidhaa na viwango vya mishahara, vinaendelea kuwa hatari kwa bara la Ulaya, Lagarde aliliambia baraza ya Uhusiano wa nje la Marekani. Wakati huo huo IMF imesema kuna uwezekano wa kupungua kwa kasi ya ukuaji wa uchumi katika mataifa yanayoinukia, yakiongozwa na China.

"Maswali ya wazi tuliyonayo wakati huu ni je, kushuka kwa bei za mafuta na uchumi imara nchini Marekani vitupe matumaini kuhusu uchumi wa dunia? Jibu ni hapana, hapana, hapana, kwa nini? Kwa sababu kuna masuala chungu mzima, athari za mgogoro wa kiuchumi ambazo bado tunazo, na ambazo zinadhofisha uchumi wetu," alisema Lagarde katika hotuba yake kwa baraza la masuala ya kigeni la Marekani.

Alisema kupungua kwa bei za mafuta ni jambo zuri sana kwa uchumi wa dunia, lakini uchumi huo uko katika hali mbaya sana, na hilo halitasaidia. Alisema kupungua kwa bei ya mafuta kunasaidia kupandisha uwezo wa wananchi kununua bidhaa, kunaongeza mahitaji binafsi ya mafuta katika mataifa yanayonunua kutoka nje, na kutegemea ni kwa muda gani bei zitaendelea kuwa chini, hili linaweza kutoa mchango katika ukuaji wa uchimi wa dunia kwa muda.

Kuimarika kwa uchumi wa Marekani pia kunaelekea kuwa maumivu kwa baadhi ya mataifa. Wakati data za Marekani kutoka Desemba zimewasukuma wawekezaji kuamini kuwa benki kuu ya nchi hiyo itasubiri pengine hadi mwezi Oktoba kupandisha viwango vya riba, Lagarde alisema kukazwa kwa sera ya fedha kunakotarajiwa kunaweza kuvuruga masoko ya fedha, hasa katika mataifa masikini zaidi ambako mabenki na makampuni yamekopa dola zaidi katika miaka ya karibuni.

Rais wa Benki Kuu ya Ulaya ECB, Mario Draghi, amesema benki hiyo imeyaanda masoko ya fedha kwa ununuzi wa dhamana kubwa za fedha ili kukabiliana na kuongezeka kwa fedha katika mzunguko.

Rais wa Benki Kuu ya Ulaya ECB, Mario Draghi, amesema benki hiyo imeyaanda masoko ya fedha kwa ununuzi wa dhamana kubwa za fedha ili kukabiliana na kuongezeka kwa fedha katika mzunguko.

Bei za mafuta kushuka zaidi

Kushuka kwa bei za mafuta na bidhaa nyingine tayari kumeziweka katika shinikizo Nigeria, Urusi na Venezuela, alisema Lagarde. Mafuta ghafi yamepoteza karibu asilimia 60 ya thamani yake tangu mwezi Juni, na wachambuzi wanasema bei za mafuta zitaendelea kushuka angalau kwa kipindi chote cha nusu ya kwanza ya mwaka huu.

Matamshi ya Lagarde yalikuja wakati benki kuu ya Ulaya ECB, ikiyaanda masoko ya fedha kwa jaili ya mpango wa ununuzi wa dhamana kubwa za fedha ili kukabiliana na hatari ya kuongezeka kwa fedha kwenye mzunguko. Siku ya Jumatano, rais wa ECB Mario Draghi alisema benki hiyo ilikuwa na njia chache mbadala kwa mpango huo.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/afpe,rtre.
Mhariri: Saum Yusuf

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com