1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ICC yapata mwendesha mashtaka mpya

Iddi Ssessanga
13 Februari 2021

Zaidi ya mataifa 120 yamemchagua mwanasheria wa Uingereza Karim Khan kuwa mwendesha mashtaka mpya wa mahakama ya kimataifa ya uhalifu ICC, kuchukuwa nafasi ya Fatou Bensouda anaemaliza muhula wake wa miaka 9 mwezi Juni.

https://p.dw.com/p/3pIwE
Karim Kahn wird Chefanklaeger des Weltstrafgerichts
Picha: Sabah Arar/AFP/Getty Images

Khan alichaguliwa katika kura ya pili ya siri na wanachama 123 wa mkataba wa Roma ulioianzisha mahakama hiyo, na kuhitimisha mchakato mgumu wa kutafuta mrithi wa Fatou Bensouda, wakati mhula wake wa miaka tisa utakapomalizika mwezi Juni.

Khan ambaye amejikita katika sheria ya kimataifa na sheria ya kimataifa ya haki za binadamu, alitazamwa na wengi kama mtu mwenye nafasi kubwa ya kushinda kura hiyo. Lakini si yeye wala wagombea wengine aliepata uungwaji mkono wa kutosha ili kuteuliwa kwa muafaka, na hivyo kupelekea kura ya Ijumaa katika ukumbi wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

Soma pia: Mahakama ya ICC kumchagua mrithi wa Bensouda

Wakati Michal Mlynar, makamu wa rais wa baraza la mataifa wanachama alipotangaza kwamba Khan ameshinda, makofi kidogo yalisikika katika ukumbi, ambako wanadiplomasia waliokuwa wamevaa barakoa walipiga kura moja baada ya mwingine, wakitumbukiza kura zao kwenye maboksi yalioweka mbalimbali kutokana na vizuwizi vya COVID-19.

Karim Kahn wird Chefanklaeger des Weltstrafgerichts
Karim Khan, mwendesha mashtaka mkuu ajaye wa ICC.Picha: Haidar Hamdani/AFP/Getty Images

Khan alipata kura 72, nyingi kabisaa kuliko wingi uliyohitajika, Fergal Gaynor kutoka Ireland, alishika nafasi ya pili kwa kupata kura 42, akifuatiwa na Mhispania Carlos Castresana Fernandez aliepata kura 5, na Francesco Lo Voi wa Italia alipata kura 3. Mwanachama moja hakupiga kura.

Khan kwa sasa anaongoza timu ya Umoja wa Mataifa iliyoundwa kuchunguza madai ya mauaji ya kimbari, uhalifu dhidi ya ubinadamu na uhalifu wa kivita vilivyotendekea na kundi linalojiita Dola la Kiislamu nchini Iraq na ana cheo cha katibu mkuu msaidizi wa Umoja wa Mataifa.

Soma pia: ICC yamkuta na hatia mbabe wa kivita wa kundi la LRA

Amefanya kazi kama mwendesha mashtaka wa mahakama inayoshughulikia uhalifu wa kivita katika Yugoslavia ya zamani, na uhalifu dhidi ya ubinadamu na mauaji ya kimbari nchini Rwanda.

Khan siyo mgeni ICC, ambako aliwahi kuwa wakili wa utetezi wa naibu rais wa Kenya William Ruto na kuwashawishi majaji kutupilia mbali kesi dhidi ya mteja wake. Gaynor alikuwa mwakilishi wa kisheria wa wahanga wa kesi ya Ruto, ambayo ilijikita kwenye vurugu za baada ya uchaguzi.

Soma pia: Fatou Bensouda apokonywa kibali cha kuingia Marekani

Khan pia alihudumu kama mwanasheria wa Seif al-Islam Gadhafi, mtoto wa kiume wa aliekuwa kiongozi wa Libya Moammar Gadhafi, ambaye mpaka leo anasakwa na ICC kwa makosa ya uhalifu dhidi ya ubinadamu.

Niederlande Den Haag | ICC | Internationaler Strafgerichtshof
ICC inakabiliwa na changamoto si haba.Picha: Everett Collection/picture alliance

"Kuchaguliwa kwa Karim Khan kama mwendesha mashtaka kunakuja katika wakati ambapo ICC inahitajika zaidi kuliko ilivyowahi kutokea lakini imekabiliwa na changamoto kubwa na shinikizo kuhusu jukumu lake," alisema Richard Dicker, mkurugenzi wa haki ya kimataifa wa shirika la Human Rights Watch.

" Tutamtegemea bwana Khan kushughulikia kasoro za kiutendaji za mahakama hiyo, huku akionesha uhuru thabiti katika kutafuta kuwawajibisha hata wakiukaji wa haki wenye nguvu zaidi."

Mkataba wa Roma ambao ndiyo ulianzisha mahakama ya ICC ulisainiwa Julai 17, 1998 na mahakama hiyo ilianza kufanya kazi Julai 1, 2002, ikiwa na mamlaka ya kuendesha kesi za uhalifu wa kivita, uhalifu dhidi ya ubinadamu na mauaji ya kimbari - lakini inaingilia kati tu wakati mahakama za ndani zinaposhindwa kuanzisha uchunguzi wake na mashtaka. Wanachama wake 123 wanafungamanishwa na vipengele vyake, ambavyo vinajumlisha kukamata watu wote wanaotafutwa na mahakama hiyo.

Soma pia: ICC yaitaka Sudan kuruhusu wachunguzi kuwafikia mashahidi 

Wakati Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa limetumia madaraka yake chini mkataba wa Roma kuipeleka mizozo ya Darfu Magharibi nchini Sudan na Libya katika ICC, miito kwa chombo hicho chenye nguvu zaidi kuipeleka Syria, na hivi karibuni zaidi Myanmar katika mahakama hiyo imeshindwa kuvuna matunda.

Dicker alisema katika mahojiano kwamba "mahakama hiyo katika miaka 18 imejitanabahisha kama anuani ya kudumu kwa uwajibikaji kwa makosa mengi makubwa."

Niederlande Den Haag Internationaler Strafgerichtshof | Fatou Bensouda
Mwendesha mashtaka wa sasa wa ICC Fatou Bensouda.Picha: Getty Images/AFP/ANP/B. Czerwinski

Katika muda wa miaka kadhaa iliyopita, Bensouda alijaribu kupanua wigo wake mbali ya muelekeo wake wa awali wa kuilenga Afrika, na kuhusisha mataifa kama Afghanistan, Palestina, ambayo ni mwanachama wa mkataba wa Roma, na Georgia.

Kitisho dhidi ya uwepo wake

ICC inahitajia sasa zaidi kuliko awali, alisema Dicker, "kwa sababu ya kuongezeka kwa uhalifu huo," lakini mahakama hiyo imekabiliwa na kitisho dhidi ya uwepo wake, kutoka kwa utawala wa rais wa zamani wa Marekani Donald Trump.

Utawala wa Trump ulimuwekea Bensouda vikwazo pamoja na mmoja wa wasaidizi wake wa juu mwaka uliyopita kwa kuendelea kuchunguza madai ya uhalifu wa kivita dhidi ya Wamarekani, ingawa mahakama hiyo ilikuwa inakosolewa mara kwa mara huko nyuma kwa kujikita zaidi kwenye uhalifu unaotendekea Afrika.

Wiki iliyopita, majaji wa ICC waliikasirisha Israel kwa kusmea mamlaka ya mahakama hiyo yanakwenda hadi kwenye maeneo yanayokaliwa na Israel tangu vita vya Mashariki ya Kati vya mwaka 1967, na kuweka uwezekano wa mwendesha mashtaka kufungua uchunguzi juu ya vitendo vya jeshi la Israel na ujenzi wa makaazi ya walowezi katika eneo linalokaliwa na Ukingo wa Magharibi na Jerusalem Mashariki iliyotwaliwa kimabbavu na Israel.

Mahakama ya ICC yamkuta Dominic Ongwen na hatia

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu aliuita uamuzi huo kuwa ni "upotovu wa haki." Dicker alisema changamoto za ICC zinajumlisha kushughulikia baadhi ya maamuzi mabaya ya kisheria, na kuwa matumizi makubwa kuliko wafanyakazi wake wa sasa."

Mchakato wa uteuzi wa mwendesha mashtaka na madai ya kushindwa kwa baraza la mataifa wanachama wa ICC kufanya upembuzi yakinifu kuhusu wagombea kuhakikisha kuwa wanakidhi vigezo, vya maadili ya hali ya juu, vimesababisha ukosoaji kutoka mashirika ya kiraia yanayofanya kazi na mahakama hiyo.

Mwandiplomasia aliezungumza kwa sharti la kutotajwa jina akijadilia upana wa mikutano ya siri, alisema ukweli kwamba mikutano mingi ya kujadili wagombea wenye uwezekano wa kumrithi Bensouda ilifanyika kwa njia ya mtandao, ulifanya iwe vigumu kwa mataifa wanachama kujadili wasiwasi wakati wa mikutano isiyo rasmi.

Chanzo: APE