IAAF: Urusi itaendelea kupigwa marufuku | Michezo | DW | 27.11.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Michezo

IAAF: Urusi itaendelea kupigwa marufuku

Shirikisho la riadha la kimataifa – IAAF limeshikilia hatua yake ya kuipiga marufuku Urusi, likisema kuwa nchi hiyo bado haijafanya vya kutosha katika kupambana na matumizi ya dawa za kuongeza misuli nguvu

Kiongozi wa jopokazi la IAAF la kupambana na matumizi ya dawa hizo Rune Andersen, amesema masuala kadhaa muhimu bado hayajashughulikiwa kabla ya kutimizwa masharti kadhaa yatakayoweza kuiondolea Urusi adhabu hiyo. "Kama hawatakiri kuhusu kilichofanyika katika siku za nyuma, hapawezi kuwa na hakikisho kuwa hakitatokea tena. Hivyo basi jopo kazi limependekeza kwa baraza la IAAF kuwa Urusi isirejeshwe kwa wakati huu. Baraza lilikubali pendekezo hilo kwa kauli moja na jopokazi limefurahishwa na baraza la hatua hiyo ya baraza la IAAF na rais wake kwa uungwaji mkono ambao tumepokea katika majadiliano yetu"

Urusi ilipigwa marufuku kushiriki katika mashindano ya riadha ya kimataifa mnamo Novemba 2015 kuhusiana na tuhuma za mpango wa serikali matumizi ya dawa za kuongeza misuli nguvu, hatua iliyowazuia wanariadha wake kushiriki katika Michezo ya Olimpiki ya 2016 mjini Rio na mashindano ya mwaka huu ya Ubingwa wa Dunia mjini London.

Rais wa IAAF Sebastian Coe amesema amekubali kuwa Urusi haiko tayari kurejea, licha ya kuelezea matumaini katika mahojiano na AFP mwezi Oktoba kuwa maafisa wa Urusi wako kwenye mkondo sahihi. Uamuzi huo wa IAAF umetolewa kabla ya mkutano muhimu wa Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki – IOC mnamo Desemba 5 hadi 7 kuhusu kama Urusi inaweza kushiriki katika Michezo ya Olimpiki ya msimu wa barafu mwaka wa 2018 mjini Pyeongchang, Korea Kusini.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA
Mhariri:  Mohammed Abdul-Rahman