Hertha Berlin yaongoza bado Bundesliga | Michezo | DW | 16.03.2009
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Michezo

Hertha Berlin yaongoza bado Bundesliga

Manchester united yangolewa meno na FC Liverpool 4:1.

default

Veronin aendelea kutamba.

Bayern Munich licha ya kutamba mbele ya Bochum kwa mabao 3:0, ingali iko nyuma ya viongozi wa Ligi Hertha Berlin ilioitimua Bayer Leverkusen jumamosi kwa bao 1:0 ili kusalia kileleni.

Katika Premier League, Mghana Miichael Essen,aipatia jana Chelsea ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Manchester City , lakini Manchester United, ilichezeshwa kindumbwe-ndumbwe na Liverpool jumamosi ilipokomewa mabao 4-1.Katika kinyanganyiro cha mwishoni mwa wiki cha kombe la klabu bingwa barani Afrika ,Young Africans ya Tanzania, ilifungishwa virago na mapema kurudi Dar-es-salaam kwa kukatiwa matumaini na mabingwa Al Ahly ya Misri.

Katika Bundesliga,ndio mabingwa Munich wako bado nyuma ya viongozi Hertha Berlin kwa pointi 4 ,lakini Munich, imeanza kuitia shindo Berlin kwamba inapiga nayo hodi hodi kileleni.Mabao 15 kupitia ushindi mara tatu mnamo muda wa siku 8 kumerejesha imani tena katika kikosi cha mabingwa B.Munich huku Ligi ikifikia hatua za mwisho za kumtawaza bingwa.

Ushindi wa Munich wa mabao 3:0 dhidi ya bochum ,ulitanguliwa na wa mabao 5-1 dhidi ya Hannover na mabao 7-1 dhidi ya Sporting Lisbon katika champions League.Hertha Berlin inayoongoza Ligi ilitamba tena jana pale Muukrain wao Andrey Veronin alipokomea tena bao jengine katika klabu yake ya zamani Bayer Leverkusen.Kwa pointi 3 za jana ,Berlin inaendelea kuongoza kwa pointi 4 na kwa mara ya kwanza tangu kitambo kirefu inalinusa taji.Hii ikifanikiwa itakua ni kwa mara ya kwanza kwa berlin kutwaa ubingwa tangu 1931 na hicho ni kitambo kirefu.Sasa Berlin inakabiliwa na mtihani mkubwa wa kubakia kileleni wakati mabingwa B.Munich baada ya kuzika misukosuko ya karibuni, jahazi lao sasa lime'acha kwenda mrama.

Ina miadi na Stuttgart ilioteleza jana ilipozabwa mabao 4 na Bremen.Halafu itakua zamu ya Hoffenheim na baadae Hamburg mwishoni mwa mwezi ujao.Baada ya ushindi wa Jumamosi, kocha wa Hertha Berlin kutoka Uswisi alisema;

"Tumeridhika mno kwa ushindi wa bao 1:0 dhidi ya Bayer Leverkusen."

Kipindi cha pili tulicheza bora zaidi -tulisonga mbele kwa nguvu zaidi na ingawsa bao hilo lilikuja kwa kusangaza, Andrey alikua atie bao hilo mapema zaidi."Ama katika mpambano mwengine wa kususimua uliokodolewa macho sana baina ya mahasimu 2 wa jadi: FC Cologne na Borussia Moenchen Gladbach,Borussia ilitamba kwa mabao 4-2.

Katika Premier League-Ligi ya Uingereza, mabingwa Manchester United walikiona jumamosi "kile kilichomtoa kanga manyoya". Kwani, siku hiyo FC Liverpool iliwafunza mabingwa hao wa dunia,ulaya na Uingereza vipi kucheza dimba.Kwa mabao 4:1, Liverpool ilitoa salamu zake na mapema kwa MANU kwamba msimu huu hata nao walitaka taji ingawa wapo pointi 4 nyuma ya Manchester United.

Jana ilikuwa zamu ya mgahana Michael Essien, kupiga hodi katika lango la Manchester City na sasa Chelsea, ikiongozwa na Guus Hiddink,kocha pia wa timu ya Taifa ya Urusi, iko pointi 4 nyuma ya mabingwa Manchester United.Katika matokeo mengine Fulham imeikomea Bolton Wanderers mabao 4:1.Arsenal imenguruma kwa mabao 4:0 mbele ya Blackburn Rovers. Kileleni mwa Premier League, Manu yaongoza ikifuatwa na Chelsea na Liverpool huku Arsenal ikiwa nafasi ya 4.

Ama katika Serie A-Ligi ya itali, Roma iliteleza jana nyumbani na kumudu sare tu ya mabao 2:2 na Sampdoria .Mpambano huu ulikuwa patashika nyingi na mwishoe kila upande ulisalia ukicheza na wachezaji 10 tu.oma iko pointi 2 kuifikia nafasi ya 4 iliposimama Genoa kufuatia ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Cagliari.AC Milan wameangukia nafasi ya 3 baada ya ushindi wao wa mabao 5-1 dhidi ya Siena.

Jumamosi,Juventus iliopo nafasi ya pili nyuma ya viongozi Inter Milan, iliizaba Bolognia mabao 4-1 na sasa iko pointi 4 tu nyuma ya viongozi Inter Milan.Napoli imetoka sare bao 1:1 na Reggina inayoburura mkia wa ligi ya Itali.

Ligi ya Spain, Atletico Madrid imeparamia ngazi hadi nafasi ya 5 hapo jana baada ya kuizima Villareal kwa mabao 3-2.Malaga ilitoka sare mabao 2-2 na Sevilla iliopo nafasi ya 3. FC Barcelona inaendelea kuongoza la Liga ikifuatwa na Real Madrid.

Nje ya Ligi mashuhuri za Ulaya,Australia imetangaza itaania kuandaa Kombe la dunia la FIFA mwaka 2018 au 2022.Mwenyekiti wa shirikisho la dimba la Australia (FFA), Frank Lowy binafsi, ametoa ombi hilo katika Makao makuu ya FIFa mjini Zurich kabla tarehe ya mwisho kupita wiki hii.

Australia haikluwahi kuandaa kombe la dunia.Hatahivyo, itakumbana na changamoto ya nchi nyengine zinazoania kama Uingereza ilioandaa mara ya mwisho, 1966,Ubelgiji na Holland zinazopanga kugombea kwa ubia,China ilioandaa michezo ya Olimpik ya Beijing mwaka jana ,Japan tayari mwenyeji 2002,Mexico ,Indonesia,Uremo pamoja na Spian.Halkadhalika maombi mengine ni kutoka Qatar,Martekani na Urusi.

Nchi za kiafrika hazitaweza kugombea kuandaa kombe la dunia 2018 kwa sababu zamu yao wamepewa mwakani 2010 nchini Afrika kusini.Halkadhalika , nchi za Amerika Kusini hazitaweza kugombea nafasi hiyo kwavile Brazil itaandaa Kombe la dunia baada ya Afrika hapo 2014.Mara ya mwisho kwa Brazil kuandaa Kombe la dunia ilikuwa 1950 pale ilipopokonywa Kombe na Uruguay,mabingwa wa kwanza wa dunia,1930.

Kinyangan yiro cha Kombe la Afrika la klabu bingwa kilikuwa uwanjani mwishoni mwa wiki kwa duru ya pili: Mabingwa mara 6 Al Ahly, walitembelewa Cairo na mabingwa wa Tanzania-young Africans na kama kawaida yao,Al Ahly, hawakuacha kutamba nyumbani.Young Africans imekandikwa mabao 4:0. Iwapo wiki 2 kutoka sasa Yanga itafuta nyumbani mabao hayo na kuwatoa mabingwa Al Ahly ni kama kupanda kilimanjaro.

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com