Hatimaye Wasomali wamchagua rais wao | Matukio ya Kisiasa | DW | 10.09.2012
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Hatimaye Wasomali wamchagua rais wao

Rais mpya wa Somalia anatarajiwa kuchaguliwa hii leo na kumaliza uzembe na rushwa iliyoubana utawala wa mpito nchini humo, ingawa Wasomali wana wasi wasi kama enzi mpya italeta mageuzi ya kweli yanayohitajika.

Bibi wakisomali anamfanyia kampeni rais anaemaliza wadhifa wake Sheikh Shariff

Bibi wakisomali anamfanyia kampeni rais anaemaliza wadhifa wake Sheikh Shariff

Uchaguzi huo wa rais unaogombaniwa na watu 25,akiwemo pia rais anaemaliza muda wake, Sheikh Sharif Sheikh Ahmed unatarajiwa kumaliza kipindi cha mpito kinachosimamiwa na Umoja wa mataifa na kuipatia Somalia taasisi imara - kwa mara ya kwanza tangu alipong'olewa madarakani Mohamed Siad Barre, mnamo mwaka 1991.

Tangu wakati huo Somalia imekuwa ikigubikwa na mapambano ya koo,mabwana vita, makundi ya kiislam na magengi ya wahalifu.

Juhudi zote za kuunda serikali kuu zimeshindwa.Viongozi wa mpito watakaong'atuka waliingia madarakani miaka minane iliyopita na kuungwa mkono miaka hii ya nyuma na jumuia ya kimataifa. Lakini na wao pia wanamaliza kipindi chao ofisini bila ya ufanisi wowote.

"Na vivyo hivyo ndivyo matokeo yatakavyokuwa-si ya kuridhisha-kuna uwezekano taasisi nyengine dhaifu na isiyo halali ikaibuka,kama serikali ya mpito,lakini ikawa na jina jengine tu." Anasema Mtaalam wa masuala ya Somalia katika taasisi ya Max-Planck, Markus Höhne. Anahisi uchaguzi wa leo wa rais ni kiini macho tu.

Parlamentsbildung in Mogadischu Somalia

Wabunge wepya wakaribishwa katika sherehe maalum mjini Mogadishu

Hata hivyo mjumbe maalum wa Umoja wa mataifa nchini Somalia, Augustine Mahiga, anahisi kuna mengi mema yaliyoweza kupatikana hata kama sio yote .

Umoja wa mataifa unahisi uchaguzi wa leo hata kama unaweza dakika ya mwisho kuakhirishwa, ni fursa nzuri ya amani baada ya kupita miaka zaidi ya 20.

Kabla ya hapo wasomali walilichagua bunge jipya lenye wawakilishi wachache ikilinganishwa na la awali na kumteuwa mtaalam wa masuala ya katiba Mohammed Osman Jawari kuwa spika. Hata hivyo wabunge wengi hawakuchaguliwa kutokana na ujuzi wao, bali kutokana na nafasi waliyokuwa wakiikalia katika orodha ya uchaguzi,baada ya kulipa dala 60 elfu.

Na wabun ge hao hao ndio watakaomchagua rais katika uchaguzi wa siri.

)

Rais anaemaliza mhula wake Sharif Sheikh Ahmed

Anaepewa nafasi nzuri ya kushinda ni rais anaemaliza wadhifa wake Sheikh Shariff Sheikh Ahmed.

Ripoti ya siri ya Umoja wa mataifa inamtuhumu Sheikh Shariff na serikali yake kutumia vibaya na kuiba mali ya umma tangu alipoingia madarakani mwaka 2009.

Mbali na rushwa,suala la kuendewa kinyume haki za binaadam pia ni miongoni mwa mambo yanayowatia wasi wasi walimwengu nchini Somalia.

Mwandishi: Ludger Schadomsky/Hamidou Oummilkheir
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com