Harry Maguire aitwa tena kwenye kikosi cha England
20 Machi 2026
Meneja wa England Thomas Tuchel ametangaza kikosi cha wachezaji 35, Ijumaa wakati timu yake ikiendelea na maandalizi ya Kombe la Dunia.
Harry Maguire, ambaye amecheza mechi 64, aliichezea England mara ya mwisho mwaka wa 2024 na alikuwa kwenye kikosi kilichokosa ubingwa wa Ulaya wa 2024, ambapo England ilimaliza ikiwa ya pili.
Hata hivyo, nyota ya mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 33 imeng'ara tena baada ya kuitwa na hasa kutokana na kiwango cha sasa cha Manchester United iliyofufuka hivi karibuni, pamoja na mchezaji mwenzake Kobbie Mainoo.
"Harry anastahili. Amekuwa akicheza vizuri sana, hasa tangu Michael Carrick achukue nafasi yake, na kuwa na matokeo mazuri sana," Tuchel alisema.
Beki wa AC Milan, Fikayo Tomori, aliyeichezea England mara ya mwisho mwaka 2023, na mshambuliaji wa Leeds United, Dominic Calvert-Lewin, ambaye alicheza mara ya mwisho mwaka 2021, wote wamejumuishwa katika kikosi hicho.
England kuwakaribisha Uruguay Wembley
England itawakaribisha Uruguay katika Uwanja wa Wembley Machi 27, ikifuatiwa na mchezo na Japan katika uwanja huo huo siku nne baadaye. Tuchel alisema ametangaza kikosi kikubwa hivyo kwa sababu angewagawanya wachezaji katika vikosi viwili tofauti kwa michezo hiyo miwili.
Kiungo wa kati wa Everton James Garner na kipa wa Brighton & Hove Albion Jason Steele waliitwa kwa mara ya kwanza, huku kipa huyo akitarajiwa pia kujiunga na kikosi cha Kombe la Dunia kama kipa wa mazoezi.
Kiungo wa kati wa Real Madrid, Jude Bellingham ambaye amekuwa nje kwa wiki kadhaa kutokana na jeraha la misuli ya paja, pia aliitwa, lakini beki Trent Alexander-Arnold hakupata nafasi.
England pia imepangwa kucheza mechi za ziada dhidi ya New Zealand na Costa Rica mwezi Juni kama sehemu ya maandalizi ya Kombe la Dunia, litakaloandaliwa na Marekani, Canada na Mexico
England iko katika Kundi L la Kombe la Dunia, ambapo watakabiliana na Croatia, Ghana na Panama katika hatua ya makundi. Mechi yao ya ufunguzi imepangwa kufanyika Juni 17 dhidi ya Croatia mjini Dallas
KIKOSI
Walinda lango: Dean Henderson, Jordan Pickford, James Trafford, Aaron Ramsdale, Jason Steele
Walinzi: Dan Burn, Marc Guehi, Lewis Hall, Ezri Konsa, Tino Livramento, Harry Maguire, Nico O'Reilly, Jarell Quansah, Djed Spence, John Stones, Fikayo Tomori
Viungo: Elliot Anderson, Jude Bellingham, James Garner, Jordan Henderson, Kobbie Mainoo, Declan Rice, Morgan Rogers, Adam Wharton
Washambuliaji: Jarrod Bowen, Dominic Calvert-Lewin, Eberechi Eze, Phil Foden, Anthony Gordon, Harry Kane, Noni Madueke, Cole Palmer, Marcus Rashford, Bukayo Saka, Dominic Solanke