Guterres azuru Mashariki ya Kati | Matukio ya Kisiasa | DW | 28.08.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Guterres azuru Mashariki ya Kati

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres afanya ziara yake ya kwanza Mashariki ya Kati tangu achukue usukani na ameahidi kukabili matamshi ya chuki, misimamo mikali na ubaguzi

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameanza ziara yake ya kwanza nchini Israel na Palestina tangu alipochukua hatamu ya kuuongoza Umoja wa Mataifa mapema mwaka huu.  Anatarajiwa kufanya mkutano leo na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na Rais wa Israel Reuven Rivlin mjini Jerusalem na kesho ataelekea Palestina kukutana na Waziri Mkuu wa Wapalestina Rami Hamdallah.

Baada ya kuwasili Israel hapo jana ambapo alikutana na Jason Greenblatt ambaye ni afisa msaidizi mkuu wa Rais Donald Trump katika mchakato wa kutafuta amani kati ya Israel na Wapalestina, Antonio Guterres leo ametembelea eneo la kumbukumbu ya wahanga wa mauaji ya kimbari ya Wayahudi .

Waziri Mkuu wa Wapalestina Rami Hamdallah

Waziri Mkuu wa Wapalestina Rami Hamdallah

Akisema kuwa alishangazwa miaka michache iliyopita kusikia watu wakisema "damu na mchanga" ambayo ni kauli mbiu ya Wanazi Mamboleo, ameonya kuwa maneno ya chuki yapo kwa wingi katika dunia ya leo lakini ameahidi kukabili aina zote za ubaguzi na uchochezi. Akaongeza kuwa: "Ninaamini kuwa kufuatia maangamizi ya Holocaust, inapaswa kuwa matamshi ya uchochezi yawe yameangamizwa kabisa, lakini kwa bahati mbaya, tungali tunayashuhudia yakiwepo".

Maneno ya Guterres yanajiri kabla ya mkutano wake na viongozi wa Israel na Wapalestina ambapo atahimiza kuendelezwa kwa mazungumzo ya amani, huku suala la vikosi vya Umoja wa Mataifa nchini Lebanon likiwa mojawapo ya masuala kwenye ajenda yake.

Mzozo wa Gaza

Kulingana na gazeti moja la kila siku nchini Israel Haaretz, Guterres atawaomba Netanyahu na viongozi wa Wapalestina kuruhusu Wapalestina zaidi walioko Gaza kutafuta matibabu nchini Israel na waruhusu bidhaa zaidi kuingia katika ukanda wa Gaza. Guterres anasema: "Nimejitolea kikamilifu kupiga vita matamshi ya chuki, ugaidi, uchochezi na dharau dhidi ya Uislamu na aina zote za misimamo mikali ya kiimani ambayo kwa bahati mbaya hatujafaulu kutokomeza katika dunia yetu"

Maafisa wa usalama wa Israel katika Ukingo wa Magharibi

Maafisa wa usalama wa Israel katika Ukingo wa Magharibi

Siku ya Jumapili, naibu wa waziri wa mambo ya nje wa Israel Tzipi Hotovely aliwaambia waandishi wa habari kuwa Israel itamshinikiza Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuupatia mamlaka zaidi wakala wa  Umoja wa Mataifa, UNIFIL unaosimamia mpaka wa Lebanon na Israel.

Katibu mkuu huyo wa  Umoja wa Mataifa atakutana na Waziri Mkuu wa Wapalestina hapo kesho katika ukingo wa Magharibi kisha Jumatano, ataelekea Gaza ambayo inadhibitiwa na kundi la Hamas, lakini ambayo mizozo ya kibinadamu imeendelea kuongezeka.

Inatarajiwa kuwa katika ziara hiyo ya siku tatu, huenda Guterres analenga kufufua mazungumzo ya amani kuhusu vurugu na mizozo ya miongo mingi kati ya Israel na Wapalestina.

Ziara ya Guterres inajiri wakati Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa likijadili kuendeleza uwepo wa kikosi chake  nchini Lebanon kwa mwaka mmoja. Wajumbe watapiga kura juu ya suala hilo mnamo siku ya Jumatano.

Mwandishi: John Juma/DPAE/AFPE

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

 

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com