1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaMyanmar

Guterres "asikitishwa" na mauwaji Myanmar

19 Machi 2024

Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema "anasikitishwa" na ripoti za mashambulizi ya anga yanayoendelezwa na jeshi la Myanmar katika vijiji vya jimbo la Rakhine.

https://p.dw.com/p/4dtGV
Qatar Doha |  Antonio Guterres
Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akizungumza na waandishi wa habari.Picha: Karim Jaafar/AFP/Getty Images

Mapigano yametikisa jimbo la Rakhine magharibi mwa Myanmar tangu wapiganaji wa Arakan (AA) waliposhambulia vikosi vya usalama mnamo Novemba, na kumaliza usitishaji mapigano uliodumu kwa kiasi kikubwa tangu mapinduzi ya kijeshi ya 2021.

Guterres amesikitishwa na ripoti za mashambulizi ya anga yanayoendelea kufanywa na jeshi, ikiwa ni pamoja na shambulizi jengine usiku wa Jumatatu katika mji wa Minbya ambako raia wengi waliuwawa na wengine kujeruhiwa.

Mji wa Minbya uko mashariki mwa mji mkuu wa jimbo la Sittwe, ambao umekatizwa na wapiganaji wa AA katika wiki za hivi karibuni.

Soma pia: Vijana wakimbia Myanmar kuepuka kujiunga na jeshi

Kulingana na mkaazi mmoja aliyezungumza kwa sharti la kutotajwa jina kwa sababu za kiusalama, shambulio hilo la anga lilipiga kijiji cha Thar Dar Jumatatu usiku na kuwaua wanaume 10, wanawake wanne na watoto 10.

Mkazi mwingine ambaye pia aliomba jina lake lihifadhiwe, alisema watu 23 wameuawa katika mlipuko huo na wengine 18 kujeruhiwa.

Athari za mzozo

Watu waliokimbia Rakhine
Watu wakikimbia makaazi yao baada ya kuibuka mapigano mapya kati ya jeshi la Myanmar na Jeshi la Arakan (AA)Picha: STR/AFP

Tangu kuibuka tena kwa mzozo huu maelfu ya watu wameyahama makazi yao huko Rakhine, ambapo ukandamizaji wa kijeshi wa 2017 ulipelekea maelfu ya Warohingya kukimbilia nchi jirani ya Bangladesh.

Jeshi la Myanmar limekuwa na udhibiti katika mji wa Sittwe lakini katika wiki za hivi karibuni wapiganaji wa AA wamepata mafanikio katika wilaya jirani.

Aidha mapigano pia yameenea hadi nchi jirani za India na Bangladesh.

Mwezi uliopita, takriban watu wawili waliuawa nchini Bangladesh baada ya makombora yaliyorushwa kutoka Myanmar wakati wa mapigano kuvuka mpaka.

AA ni moja ya makundi yenye silaha kutoka makabila kadhaa ya watu wachache katika maeneo ya mpakani mwa Myanmar, ambao wengi wao wamepigana na jeshi tangu uhuru kutoka kwa Uingereza mwaka 1948 kuhusu uhuru na udhibiti wa rasilimali.