Ghasia za Hamburg katika mkutano wa G20 | Matukio ya Kisiasa | DW | 10.07.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Hamburg

Ghasia za Hamburg katika mkutano wa G20

Maoni ya wahariri wa magazeti ya hapa Ujerumani leo hii wanazungumzia juu ya athari za ghasia zilizotokea wakati wa mkutano wa nchi zinazoongoza kiviwanda, G20 mjini Hamburg. 

Mhariri anasema waliofanya ghasia walivuruga maandamano yalilyokuwa halali.  Waandalizi wa maandamano hayo walikuwa na lengo la kusisitiza umuhimu wa kulinda mazingira na vile vile umuhimu wa kuyazingatia madhila ya wakimbizi.  Mhariri huyo wa gazeti la Kölner Stadtanzeiger pia anatilia maanani kwamba waandamanaji hao walikuwa na nia ya kupinga sera za marais wa Urusi Vladimir Puttin,rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan na rais wa Marekani Donald Trump. Vilevile mhariri wa gazeti hilo anawataka waandamanaji wanaolemea mrengo wa shoto wajiweke kando na vitendo vya ghasia katika siku za usoni.

Naye mhariri wa gazeti la Mittledeutsche anasema kiwango cha ghasia zilizotokea katika mji wa Hamburg hakijawahi kushuhudiwa tangu kumalizika kwa vita vya pili vya dunia. Mhariri huyo anaendelea kueleza kwamba baraza la seneti la mji wa Hamburg halikujiandaa vyema kukabiliana na ghasia zilizotokea.  Mhariri wa gazeti la Süddeutsche anaiunga mkono hoja hiyo kwa kumtaka meya wa mji wa Hamburg Olaf Scholz ajiuzulu badala ya kuwalaumu wengine.

Wahariri leo pia wanazungumzia juu ya kuimarika kwa upinzani dhidi ya sera za rais wa Uturuki RecepTayyip Erdogan zinazohatarisha demokrasia nchini humo.  Maalfu ya wapinzani walishiriki kwenye maandamano yaliyofanyika katika mji wa Istanbul. Mhariri wa gazeti la Die Welt anasema lingekuwa jambo la manufaaa kama maandamano hayo yangelikuwa ndio mwanzo wa vuguvugu la kiraia nchini Uturuki.

Deutschland, G20, Tayyip Erdogan (Reuters/W.Rattay)

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan

Na mhariri wa gazeti la Neue Osnabrücker anatilia maanani upinzani dhidi ya rais Erdogan unaoendelea kupamba moto na huku sauti zinazidi kupazwa dhidi yake. Mhariri wa gazeti hilo ameandika maoni yake kwa kusema hata hivyo Erdogan ni kiongozi anayefahamika kwa kutouvumilia upinzani na ni wazi kwamba katika muda usio mrefu atachukua hatua dhidi ya wapinzani nchini mwake.

Mwandishi: Zainab Aziz/DPA

Mhariri:Josephat Charo

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com