Ghasia dhidi ya kukashifiwa Uislamu zapamba magazeti ya Ujerumani | Magazetini | DW | 13.09.2012
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Magazetini

Ghasia dhidi ya kukashifiwa Uislamu zapamba magazeti ya Ujerumani

Miongoni mwa masuala muhimu kwenye magazeti ya Ujerumani leo (13.09.2012) ni pamoja na hamaki dhidi ya filamu ya kuukashifu Uislamu iliyosababisha mauaji ya balozi wa Marekani nchini Libya.

Maandamano nchini Iraq.

Maandamano nchini Iraq.

Kuhusu Libya Muhariri wa gazeti la Financial Times anahoji ikiwa Balozi wa Marekani nchini Libya alihusika kwa vyovyote na filamu iliyozusha balaa? Hapana. Je ni diplomasia ya Marekani ndiyo inayohusika? Hapana.

Pamoja na ukweli huo waisilamu wenye itikadi kali wamepandisha mori na ghasia dhidi ya wawakilishi wa Marekani. Ni bayana kwamba matukio haya yanaonyesha kuweko uhusiano na zile chuki zisizoangalia ukweli kuelekea nchi za Magharibi.

Hata hivyo, pamoja na kuweko nguvu hizi za wenye itikadi kali zinazoonekana pembeni pembeni bado hakuna anayetaka kuona nchi hii ikiwa ya kiislamu.Katika uchaguzi wa bunge mwezi Julai vyama vya kidini vilishindwa vibaya na waliberali.

Sasa wenye itikadi kali wanataka kuitumia filamu hii ya aibu dhidi ya Uislamu ksio tu kusukuma mbele agenda zao,bali pia kuwatia wahaka na mshawasha wapiga kura ili wajipatie ushindi.

Maandamano nchini Yemen.

Maandamano nchini Yemen.

Kwa upande mwingine, mhariri wa gazeti la Saarbrücker anasema kuweka amani katika Mashariki ya Kati ilikuwa moja kati ya malengo yake muhimu katika sera yake ya nje Rais Barack Obama.

Ndio, lakini kwa mara nyingine pia Obama analazimika kuukubali ukweli unaouuma kwamba eneo hilo litabakia kuwa chanzo hatari cha kuzusha moto. Mvutano wa hivi karibuni unaonyesha ni jinsi gani Israel inavyoonekana kuongeza kitisho cha uwezekano wa kuishambulia kijeshi Iran, jambo ambalo haliridhiwi na Marekani.

Bila shaka kuishambulia Iran sio suala litakalozihusu tu nchi mbili hizo maadui yaani Israel na Iran bali ni hali itakayoibadili hali nzima ya usalama wa nchi nyingi, na hasa katika nchi nyingi za Kiislamu ambazo zinaitazama Marekani kama mshirika wa karibu wa Israel.

Maandamano nchini Misri.

Maandamano nchini Misri.

Wahariri wa Ujerumani pia wametuwama zaidi leo hii katika suala la juhudi za kuutafutia ufumbuzi mzozo wa madeni barani Ulaya. Wengi wa wahariri hao wamezichonga kalamu zao kuandika kuhusu uamuzi uliopitishwa na mahakama kuu ya katiba ya humu nchini juu ya suala hilo.

Mahakama hiyo imeuridhia mpango wa kudhamini utulivu wa sarafu ya yuro yaani ESM lakini kwa mujibu wa katiba.Mhariri wa Gazeti la Reutlinger General Anzeiger anasema nchi za Ulaya zinapata faida sio tu kutokana miongoni mwao, zinalazimika pia wakati wa dhiki kusaidiana, na hivyo ndivyo alivyoamua jaji wa mahakama ya mjini Karlsruhe.

Haiwezekani kubadili mfumo na sheria zilizopo lakini mlango wa kuliendeleza suala hilo kisiasa bado upo wazi. Uamuzi wa Karlsruhe ni tukio pia la kihistoria kwa nchi za Ulaya kutoka kwenye mshikamano wa kiuchumi kuelekea umoja wa kisiasa.

Mwandishi: Saumu Mwasimba
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman