1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Gesi ya Carbon yaongezeka duniani kwa asilimia mbili

Caro Robi
13 Novemba 2017

Kiwango cha gesi ya Carbon inayotolewa duniani kinatarajiwa kuongezeka kwa asilimia mbili mwaka huu hiyo ikiwa ni rekodi mpya iliyotangazwa na wanasayansi katika mkutano wa kimataifa wa mazingira mjini Bonn.

https://p.dw.com/p/2nVyY
China | Illegale Stahlfabriken unterlaufen Chinas Emissionsgesetze
Picha: Getty Images/K. Frayer

Ripoti hiyo ya wanasayansi inadidimiza matumaini kuwa kutolewa kwa gesi chafu kulikuwa kumeshafika kilele chake na hivyo haikutarajiwa kuongezeka bali kupungua. Wanasayansi wamesema kiwango cha gesi ya Carbon kilikuwa hakijabadilika katika kipindi cha mwaka 2014 hadi mwaka jana, lakini mwaka huu kimeongezeka.

Takwimu hizo zilizotolewa na wanasayansi 76 wa kutoka nchi 15 ni pigo kwa malengo ya makubaliano ya kuyaokoa mazingira yaliyofikiwa mwaka 2015 mjini Paris, Ufaransa ya kupunguza kiwango cha gesi chafu hasa kutoka viwandani inayochafua mazingira na hivyo kusababisha majanga kama vimbunga, mafuriko, ukame na kina cha maji ya baharini kuongezeka.

China mchafuzi namba moja

China ambayo ni nchi ya kwanza duniani katika kuchafua mazingira imechangia asilimia 3.5 zaidi ya gesi ya Carbon mwaka huu kutokana na uzalishaji zaidi wa nishati ya makaa ya mawe wakati ambapo ukuaji wa kiuchumi wa taifa hilo ukiimarika. Nchi hiyo inachafua mazingira kwa asilimia 30.

Kohlekraftwerk in China
Kiwanda cha nishati ya mawe nchini ChinaPicha: picture alliance/dpa

Marekani ambayo ni ya pili katika uchafuzi wa mazingira inatarajiwa kushuhudia kupungua kwa asilimia 0.4 tu ya utoaji wa gesi chafu mwaka huu.

Hayo yanakuja huku mameya wa miji 25 ya nchi mbali mbali duniani, wakiwakilisha raia milioni 150 hapo jana waliahidii kupunguza viwango vya gesi chafu ya Carbon hadi sufuri ifikapo mwaka 2050 huku wakiimarisha juhudi za kuweza kuhimili zaidi athari za mabadiliko ya tabia nchi.

Mkutano wa Bonn waingia wiki ya pili

Mameya hao wameahidi kuweka mikakati kabambe ifikapo 2020 ya mpango mpya wa kuchukua hatua za kuyalinda mazingira na wakati huo huo kuwahamasisha wakazi wa miji yao kuhusu umuhimu wa kuchukua hatua zaidi kuyalinda mazingira ili kunufaika kijamii, kimazingira na kiuchumi. Waziri wa mazingira wa Ujerumani Barbara Hendrick amesema wanahitaji ushirikiano wa kila kiongozi kufikia malengo ya kuyaokoa mazingira.

Miji tisa mikubwa ya Afrika ikiwemo Cape Town, Addis Ababa, Lagos na Nairobi itasaidiwa kufikia mipango ya muda mrefu ya kuhimili athari za mabadiliko ya tabia nchi kuambatana na malengo ya makubaliano ya Paris ya kupunguza viwango vya joto hadi chini ya nyuzi mbili kwa kusaidiwa na serikali ya Ujerumani.

Mkutano huo wa mazingira ujulikanao COP23 ulioanza Jumatatu wiki iliyopita, unaingia katika hatua muhimu wiki hii, huku viongozi wa nchi takriban 20 wakitarajiwa kuhudhuria wakiongozwa na mwenyeji wao Kansela wa Ujerumani Angela Merkel. Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron na Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres pia wanatarajiwa kuhutubia katika mkutano huu.

Mwandishi: Caro Robi/afp/Reuters

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman