1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Gereza la Guantanamo latimiza miaka 20

11 Januari 2022

Miongo miwili baada ya wafungwa wa kwanza kuwasili katika gereza la Guantanamo Bay linalotumiwa kuwashikilia washukiwa wa ugaidi, kundi la wataalamu wa Umoja wa Mataifa limeihimiza Marekani kulifunga gereza hilo.

https://p.dw.com/p/45NNS
Filmszene | Der Mauretanier
Picha: Graham Bartholomew/tobis Film/dpa/picture alliance

Kumekuwepo na malalamiko kutoka kwa wanaharakati wa haki za binaadamu kwamba kunafanyika ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu unaofikia kiwango cha mateso kwa wafungwa wa gereza hilo ambao ni watuhumiwa wa kesi za ugaidi. 

Mnamo Januari 10, mwaka 2002, gereza la Guantanamo Bay nchini Cuba lilifungua milango yake kwa wafungwa wa kwanza na hadi leo licha ya miito ya kulifunga, bado linaendesha oparesheni zake.

Soma Zaidi: Obama arejea ahadi ya kuifunga Guantanamo

Kundi la wataalamu huru wanaotetea haki za binadamu kutoka Umoja wa Mataifa wameonyesha kugadhabishwa kutokana na kuwa, gereza hilo lililofunguliwa kwenye kambi ya jeshi la Marekani nchini Cuba baada ya mashambulizi ya kigaidi ya Septemba 2001, bado linaendesha oparasheni zake hadi leo.

Wataalamu hao wa Umoja wa Mataifa wamesema gereza hilo linaloendeshwa na jeshi la wanamaji la Marekani, linatumiwa kama kituo cha mateso na kwamba uwepo wake unaitia doa serikali ya Marekani inayojinadi kote duniani kwa kuheshimu utawala wa sheria.

Militärgefängnis I Guantanamo
Baadhi ya wafungwa wakiwa wamepiga magoti wakati wa swala ya asubuhi katika gereza la Guantanamo. Miito inazidi kuongezeka kwa gereza hilo kufungwaPicha: John Moore/Getty Images

Katika taarifa, wataalamu hao wamesema na hapa nanukuu, "Miaka 20 ya kuwazuia kiholela na bila ya kuwafunguliwa mashtaka, pamoja na mateso na unyanyasaji ni jambo lisilokubalika kwa serikali yoyote hasa serikali ambayo inadai kuwa mstari wa mbele katika kulinda haki za binadamu," mwisho wa nukuu.

Soma Zaidi: Wikileaks yafichua uchambuzi wa Guantanamo 

Makundi mawili ya Umoja wa Mataifa yanayohusikana na kesi za watu kupotezwa na kuzuiliwa kiholela, pamoja na wataalamu huru watano wanaotetea haki za binadamu wameitaka Marekani kulifunga gereza hilo na kuwarudisha wafungwa katika nchi zao au kuwahamisha katika nchi nyengine zilizo salama. Kando na hayo, wameitolea mwito Marekani kuwalipa fidia wafungwa hao kutokana na mateso na kuwaweka kizuizini kiholela bila ya kuwafungulia mashtaka.

Kuna wakati gereza hilo lilikuwa limewashikilia karibu wafungwa 800 kutoka sehemu mbalimbali za duniani, japo sasa lina wafungwa wasiopungua 39, baadhi yao wakiwa kizuizini tangu gereza hilo lilipofunguliwa kwa mara ya kwanza mnamo Januari 10, mwaka 2002.

Aidha 13 kati yao wamepewa ruhusa ya kuhamishwa, ingawa kuwatafutia sehemu mbadala au mchakato wa kufanyia mipango ya kuwarejeshwa makwao ndio unaendeshwa kwa mwendo wa kobe. Wafungwa wengine 14 wanataka kuachiliwa huru, wakati 10 wakiwa katika mchakato wa kusikilizwa kwa kesi zao wakati wawili tayari wametiwa hatiani.

Msemaji wa wizara ya ulinzi ya Marekani Pentagon John Kirby alisema jana Jumatatu kuwa Rais Joe Biden anataka kulifunga gereza hilo japo hilo bado linasalia kuwa suala lenye utata.

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi