G7: Hatua nyingi ndogo kwa ulimwengu bora | Matukio ya Kisiasa | DW | 09.06.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

G7: Hatua nyingi ndogo kwa ulimwengu bora

Kwa waliotarajia maajabu saba kutoka kwa mataifa saba ya jadi yalioendelea, watakuwa wamekatishwa tamaa. Lakini kwa wale ambao hawakutarajia chochote kutoka mkutano wa kilele wa G7 wameelimika, anasema Christian Trippe.

Kuna tabia iliyojengeka nchini Ujerumani, hasa miongoni mwa waandishi wa habari, ya kuonyesha kwamba wanajua kila kitu kuhusu jambo hata kabla halijafanyika na kulitathmini. Mkutano wa kilele wa G7 umetoa mfano mzuri wa tabia hii ya ujuaji ya waandishi wa Ujerumani: Mkutano umepotoka, na kuwa tukio linalogharimu fedha nyingi kupita kiasi, usiyo na ufanisi, usiojihusisha na jamii, na uliojiweka mbali na raia, na kwamba bila Putin, bila Urusi ya Putin, mazungumzo hayo hayangekuwa na tija. Huu ndiyo ulikuwa mtazamo mkuu wa taarifa za habari zilizoripotiwa nchini Ujerumani kote kabla ya Mkutano huo wa kilele uliyofanyika katika kasri la Elmau.

Pamoja na hayo, mwangalizi yeyote anaweza kushangazwa na uhalisia. Kwa sababu kuna matokeo yanayoweza kuthabitishwa kwa kuangalia yaliyopita. Katika upande wa sera ya maendeleo kumekuwa na msukumo wa kisiasa, makubaliano na mipango, kama vile kusaidia mfuko unaonuwia kuendeleza usalama kazini na afya katika mataifa yanayoendelea.

Msaada unaweza kuwa maslahi binafsi

Mapambano dhidi ya umaskini na sera za kimataifa za kijamii siyo vielelezo vya uhisani tu, lakini kuna manufaa binafsi pia. Misaada hiyo inanuwia kuweka utulivu wa kijamii katika mataifa ya Kiislamu yanayoinukia na yanayoendelea ili kuepusha kuzagaa kwa itikadi kali za Kiislamu katika mataifa hayo. Na katika mataifa yaliyo na utulivu na msingi imara wa uchumi, watu hawakimbii. Mwenye kuzungumzia maadili yake hahitaji kuficha maslahi yake, na mwenye kuwakilisha maslahi yake, hufanya hivyo kwa ubora zaidi.

Mwandishi wa DW Christina Trippe.

Mwandishi wa DW Christina Trippe.

Pia katika ulinzi wa mazingira, mataifa saba yalioendelea kiviwanda yamepata mtazamano sawa. Kwa upande mmoja wamerejelea tu yale yaliokubaliwa tayari. Lakini kwa dhamira yao ya kufikia lengo la matumizi ya wa nishati safi katika karne hii, mataifa hayo saba yameweka shabaha mpya inayostahili. Wakati makubaliano mapya kuhusu mazingira yatakaposainiwa mwishoni mwa mwaka huu, hicho ndicho kitakuwa kigezo cha utashi wa kisiasa wa mataifa hayo saba makubwa zaidi kiviwanda duniani.

Hizi ni ahadi zinazohitaji kutimizwa. Kuna mabadiliko ya kisiasa, ambayo tutakuja kujua kama yameshughulikiwa.Lakini suala la muhimu ni matokeo. Hata kwenye sera ya kigeni, mataifa hayo saba yametoa msimamo thabiti dhidi ya Urusi kuhusiana na sera yake ya kibabe dhidi ya majirani zake, wakikubalina kuendeleza vikwazo hivyo na kutishia hata kuviongeza makali.

Ulaya yaamua ajenda

Ulaya imeudhibiti mkutano huu wa G7 kuliko ilivyowahi kutokea. Ukiangalia tu orodha ya washiriki utagundua ni jinsi gani matazamo wa Ulaya ulivyotawala mkutano huo. Kati ya washirki tisa wa mkutano huo, sita walikuwa wawakilishi wa taifa la Umoja wa Ulaya au taasisi ya umoja huo. Mageuzi ya G7 yanaweza kuanzia hapa.

Mada nyingi pia zilikuwa na upande wa pili wa Umoja wa Ulaya - mfano mgogoro wa madeni wa kanda inayotumia sarafu ya euro, hatma ya malumbano juu ya Ugiriki, mgogoro mashariki mwa Ukraine na wimbi la wahamiaji katika bahari ya Mediterania, ambalo ni matokeo ya kuparaganyika kwa utawala katika mataifa ya Mashariki ya Kati na vita vya wenyewe kwa wenyewe katika mataifa ya Afrika.

Kwa hili la mwisho, Marekani ina maslahi kutokana na sababu za siasa za kijiografia, lakini Kanada na Japan hazihusiani kwa vyovyote na sera ya wakimbizi na uhamiaji ya Umoja wa Ulaya.

Kwa hivyo kwa mtazamo wa Ulaya, mbali na suala la maandalizi yapo mengi yaliyojitokeza kwenye mkutano huo. Kwamba kila kitu kimekwenda kwa uhafifu, hilo wamelielewa pia viongozi wa G7. Hawatakosea watu wakijadiliana, kama inavyotokea katika matukio mengine yanayokuzwa na vyombo vya habari. Viongozi wa G7 wameweza kusonga mbele na pengine kitachofuata kitawavutia zaidi wale wanaoamini wanajua kila kitu kabla hakijatokea.

Mwandishi: Christian Trippe

Tafsiri: Iddi Ssessanga

Mhariri: Oummilkheir Hamidou

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com