1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

EU huenda ikatuma ujumbe wa kijeshi Msumbiji katika ijayo

Tatu Karema
28 Mei 2021

Mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya Josep Borell amesema huenda ikauchukuwa Umoja huo miezi kadhaa kupelekea ujumbe wa mafunzo ya kijeshi nchini Msumbiji.

https://p.dw.com/p/3u6Ip
Russland PK Sergei Lawrow und Josep Borrell
Picha: Russian Foreign Ministry/REUTERS

 

Kabla ya mkutano wa mawaziri wa ulinzi wa mataifa wanachama wa Umoja wa Ulaya mjini Lisbon nchini Ureno ambapo suala hilo linatarajiwa kuzungumziwa, Borrell amewaambia wanahabari kwamba anafikiri wanaweza kuidhinisha ujumbe huo wa mafunzo ya kijeshi.

 

Borrell amesema kuwa amewapa habari mawaziri hao kuhusu jibula ombi laMsumbiji la usaidizi wa Umoja wa Ulaya katika kushughulikia hali ya usalama nchini humo pamoja na vitisho wanavyokabiliana navyo katika eneo la Cabo Delgado na kwamba kazi bado inaendelea.

Borrell ameongeza kuwa tatizo ni kupata mataifa mengi zaidi mbali na Ureno kuongeza wanajeshi na kusema huenda ikachukuwa miezi kadhaa kupata ujumbe wa mafunzo kutoka Umoja huo.

Ureno yatuma wanajeshi wake

Awali, Borrell alisema kuwa huenda wanajeshi kati ya 200-300 wakapelekwa nchini Msumbiji kufikia mwishoni mwa mwaka. Tayari mwezi huu, Ureno imetuma wanajeshi wake 60 katika taifa hilo ambalo ni koloni lake la zamani ili kuanza kuwapa mafunzo wanajeshi kukabiliana na magaidi, kutoa habari za kijasusi na kutumia ndege zisizokuwa na rubani kushambulia maeneo ya wanamgambo.

Indien-Tag 2013 in Köln Joao Cravinho
Waziri wa ulinzi wa Ureno - Joao CravinhoPicha: Koelnmesse GmbH

Waziri wa ulinzi wa Ureno Joao Cravinho, amesema kuwa mataifa kati ya 7-8 yameelezea kujitolea kwao kutuma wanajeshi wake nchini humo lakini akakataa kuyataja. Cravinho ameongeza kuwa Ureno ndilo taifa litakalokuwa mshirika mkuu katika ujumbe huo. Cravinho anatarajia kuwa wanajeshi waliosalia watapelekwa nchini Msumbiji katika muda wa miezi mitatu hadi minne ama labda haraka zaidi.

Mkutano wa SADC wakosa kuafikia mpango thabiti kukabiliana na magaidi

Huku hayo yakijiri,viongozi wa mataifa matano ya jumuiya ya kiuchumi ya kusini mwa Afrika, SADC wamekubaliana kukutana tena baada ya wiki nne.

Mazungumzo ya jumuiya hiyo siku ya Alhamisi yalitarajiwa kufanya uamuzi juu ya pendekezo lililotolewa la kupeleka wanajeshi 3,000 katika jimbo la Cabo Delgado, ambapo waasi wamechukua udhibiti wa miji na vijiji, na kulazimisha mamia kwa maelfu ya watu kukimbia makazi yao. Lakini viongozi hao wamesema wamepiga hatua katika kupata suluhisho la kudumu la kupambana na ugaidi nchini Msumbiji na kwamba wamelizingatia suluhisho lililopendekezwa.

 Marais wa Afrika Kusini, Malawi, Zimbabwe na Botswana walikaribishwa katika mazungumzo hayo ya faragha na mwenyeji wao Rais Filipe Nyusi mjini Maputo. Tanzania iliwakilishwa na rais wa visiwa vya Zanzibar Hussein Mwinyi.