Ethiopia, Misri, Sudan zakubali kuahirishwa ujazaji wa bwawa la Nile | Matukio ya Afrika | DW | 27.06.2020
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Ethiopia, Misri, Sudan zakubali kuahirishwa ujazaji wa bwawa la Nile

Misri, Sudan na Ethiopia zimekubaliana kwamba Ethiopia itachelewesh kujaza bwawa lake la umeme kwenye mto wa Blue Nile na kufanya mazungumzo kumaliza mzozo. Hatua hii imekuja baada ya wiki kadhaa za malumbano na vitisho.

Viongozi wakuu wa Misri, Sudan na Ethiopia wamekubaliana kwamba Addis Ababa itachelewesha ujazaji wa bwawa lake lililoko kwenye mto wa Blue Nile hadi mataifa hayo matatu yatakapofikia makubaliano juu ya mgawo wa maji ya mto huo, serikali za Misri na Sudan zilisema siku ya Ijumaa.

Tangazo hilo linakuja kama msaada mdogo baada ya wiki kadhaa za kuongezeka kwa mzozo kati ya Ethiopia, ambayo awali ilikuwa imeamua kuanza kujaza bwawa lake la mabilioni ya dola la Grand Ethiopian Renaissance mnamo mwezi Julai, na mataifa unakoelekea mto huo ya Misri na Sudan.

Misri na Sudan zote zililiomba Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wiki iliyopita kuingilia kati mzozo huo uliodumu kwa miongo kadhaa.

BG Grand Renaissance Dam | Der äthiopische Premierminister Abiy Ahmed Ali mit dem ägyptischen Präsident Abdel-Fattah al-Sisi (2018)

Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed akiwa katika mazungumzo na rais wa Misri Abdel-Fattah el-Sissi kuhusu mradi wa bwawa la Grand Renaissance.

"Mktaba wa mwisho unaofungamanisha kisheria kwa pande zote unaosisitiza uzuwiaji wa hatua zozote za upande mmoja, ikiwemo kujaza bwawa, utatuma katika barua kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ili liuzingatie katika kikao chake kinachojadili suala la bwawa la Rebaissance siku ya Jumatatu," ilisema ofisi ya rais wa Misri Abdel-Fattah el-Sissi siku ya Ijumaa.

Waziri Mkuu wa Sudan Abdalla Hamdok pia alitoa taarifa akisema, "imekubaliwa kwamba ujazaji wa bwawa utacheleweshwa hadi makubaliano yafikiwe." Ofisi yake ilisema kamati za kiufundi za mataifa yote matatu zitaanza majadiliano kwa lengo la kufikia makubaliano katika muda wa wiki mbili.

"Sudan no moja ya wanufaikaji wakubwa zaidi wa bwawa na pia mmoja wa watakaopata hasara kubwa zaidi ikiwa hatari hazitapunguzwa, hivyo inazisihi Misri na Ethiopia kuzingatia umuhimu wa kutafuta suluhisho," alisema Hamdok.

Taarifa kutoka kwa viongozi hao wawili wakitangaza mafanikio ilikuwa baada ya mkutano wa dharura wa kilele wa Umoja wa Afrika uliofanyika kwa njia ya mtandao, na kuongozwa na rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa.

Wakati hakukuwa na majibu ya mara moja kutoka Ethiopia, waziri Mkuu Abiy Ahmed kwenye ukurasa wa Twitter, aliyataja mazungumzo kuhusu bwawa hilo kuwa yenye "ufanisi." 

BG Grand Renaissance Dam | Treffen zwischen Äthiopiens Premierminister Abiy Ahmed Ali und Südafrikas Präsident Cyril Ramaphosa

Abiy Ahmed akiwa na rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa ambaye ni rais wa sasa wa Umoja wa Afrika na alieongoza juhudi za usuluhishi kati ya mataifa ya matatu.

Ethiopia imekuwa ikipaza sauti kuhusu nia yake ya kujaza bwala hilo, ambalo inasema ni muhimu kwa mahitaji yake ya umeme na maendeleo. Inasema mradi huo wa bwawa la umeme wenye thamani ya dola bilioni nne, utakuwa na uwezo wa kuzalisha megawati 6,450 na utasidia kuwaondoa mamilioni ya watu kutoka kwenye dimbwi la umaskini.

Misri kwa upande mwingine, inautegemea mto Nile kwa asilimia 97 ya mahitaji yake ya maji safi. Inasema bwana hilo linaweza kupunguza ugavi wake wa maji na kuwa athari mbaya kwa wakaazi wake. Sudan pia inategemea mto Nile kwa ugavi wa maji na imetoa mchango muhimu katika kuzileta pande mbili pamoja.

Misri na Ethiopia zote zimegusia uwezekano wa kuchukua hatua za kijeshi kulinda maslahi yake, na kuibua hofu ya kutokea kwa mgogoro wa wazi.

Chanzo: Afpe, AP, Reauters