Erdogan:Vikwazo dhidi ya Qatar havikubaliki | Matukio ya Kisiasa | DW | 13.06.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Erdogan:Vikwazo dhidi ya Qatar havikubaliki

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan ameitaja kuwa kinyume cha utu na  na maadili ya kiislamu hatua ya mataifa ya eneo la Ghuba kuitenga Qatar kiuchumi na kisiasa.

Mgogoro huo umeiweka Uturuki katika nafasi tete kutokana na Qatar kuwa mshirika wake mkuu katika eneo hilo la Ghuba huku pia ikidumisha uhusiano wake unaoimarika na Saudi Arabia, taifa lenye ushawishi mkubwa katika eneo hilo. Matamshi ya Erdogan yametolewa  siku  nane baada ya Saudi Arabia, Umoja wa falme za kiarabu,Bahrain na Misri kuvunja  uhusiano wao na Qatar kwa madai ya kuunga mkono makundi ya wapiganaji wa kiislamu,madai aliyoyakanusha vikali. Akiwahutubia wanachama wa chama chake cha AK bungeni,Erdogan amesema leo  atashiriki mkutano kwa njia ya simu  na mwenzake wa Ufaransa Emmanuel Macron na Emir wa Qatar Tamim Bin Hamad al Thani kuujadili mgogoro huo.

Türkei Parlament in Ankara (picture-alliance/dpa/EPA/STR)

Bunge la Uturuki mjini Ankara

Hatua zilizochukuliwa na mataifa ya Ghuba dhidi ya taifa hilo ndogo lenye utajiri wa mafuta na gesi na lilo na idadi ya watu millioni 2.7 zimekatiza hata uagizaji chakula na vifaa vyengine kutoka nje."Uamuzi huo ni kama hukumu ya kifo dhidi ya Qatar.Taifa hilo limeathirika upande wa chakula,dawa  na chochote unachoweza kufikiria.Hata kufunga anga zake kwa ndege za Qatar” amesema Erdogan. Qatar, ambayo asilimia 80 ya chakula chake kilikuwa ni kutoka mataifa jirani kabla ya kuvunjika uhusiano wa kidplomasia sasa imelazima kuzigeukia  Iran na Uturuki  kupata chakula na maji.

Qatar Doha - Leute versorgen sich mit Lebensmitteln (picture-alliance/AP Photo/shalome05)

Wasiwasi wa maji na chakula umepungua

Erdogan aitetea Qatar kuhusu ugaidi

Rais Erdogan amekanusha vikali madai kuhusishwa  Qatar na magaidi,na kusema taifa hilo limesadia kukabiliana na wapiganaji wanaojiita dola la kiislamu-IS. "Qatar sio nchi inayounga mkono ugaidi. Badala yake Qatar pamoja na Uturuki zimeonyesha msimamo mkali dhidi ya dola la Kiislamu IS  ambalo  limesababisha uharibifu mkubwa na maumivu  katika eneo letu."Rais Erdogan pia anatazamiwa kufanya mazungumzo kwa njia ya simu na rais wa Marekani Donald Trump kuhusiana na mzozo huo wa eneo la ghuba japo siku ya mazungumzo hayo haijatangazwa. Erdogan ameahidi kuendelea kuisaidia Qatar na kusema  mzozo huo unapaswa kushughulikiwa kabla ya kumalizika  mwezi mtukufu wa Ramadhani.Ingawa mgogoro huo  kwa kiasi fulani umetulia ,lakini malumbano yanaendelea  katika vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.

Mwandishi:Jane Nyingi AFP/AP
Mhariri : Mohammed Abdul-Rahman

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com