Erdogan aapa ′kuvisafisha′ vyombo vya dola | Matukio ya Kisiasa | DW | 18.07.2016
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Erdogan aapa 'kuvisafisha' vyombo vya dola

Siku tatu baada ya jaribio la kumpindua kushindwa, Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki ameapa kuzisafisha taasisi zote za dola dhidi ya kile alichokiita "saratani", huku watu 6,000 wakikamatwa kwa jaribio hilo.

Rais Tayyip Erdogan akiwahutubia waandamanaji mjini Instanbul baada ya mazishi siku ya Jumapili.

Rais Tayyip Erdogan akiwahutubia waandamanaji mjini Instanbul baada ya mazishi siku ya Jumapili.

Akizungumza na maelfu ya waandamanaji waliohudhuria mazishi ya watu kadhaa waliouawa kwenye jaribio hilo la Ijumaa, Erdogan amesema waliopanga njama hiyo hawana pa kukimbilia. Aliwaambia waombolezaji hao hapo jana kwamba "saratani" imeenea ndani ya vyombo vya dola, lakini akasisitiza kwamba hatachelea kuiangamiza.

Tayari, viongozi kadhaa duniani, wakiwemo Rais Barack Obama wa Marekani na Kansela Angela Merkel wa Ujerumani, wameitolea wito serikali ya Uturuki kufuata utawala wa sheria katika wakati huu inapowashughulikia washukiwa wa njama hiyo.

Mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya, Federica Mogherini amesema Umoja huo ungelipenda kuona sheria inachukuwa mkondo wake kikamilifu na inalindwa kwa maslahi ya Uturuki yenyewe. Akizungumza na waandishi wa habari kabla ya kuanza kikao na mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya mjini Brussels asubuhi ya leo, Mogherini ameitaka Uturuki kutochupa mipaka kwenye kushughulikia suala hili.

"Kwa hakika, tutaijadili Uturuki pamoja na mawaziri wa mambo ya nje mwanzoni mwa kikao. Kama ambavyo tulikuwa wa kwanza kusema kwenye usiku ule wa msiba kuwa lazima taasisi za kidemokrasia na halali ziheshimiwa, leo tutasema tena kwa pamoja kuwa hilo halimaanishi kuwa utawala wa sheria na usimamizi hauna maana. Kinyume chake, unahitajika kulindwa kwa maslahi ya Uturuki yenyewe," alisema.

Kamatakamata yaendelea

Waombolezaji wakiwa kwenye mazishi ya wahanga wa jaribio la mapinduzi lililoshindwa nchini Uturuki.

Waombolezaji wakiwa kwenye mazishi ya wahanga wa jaribio la mapinduzi lililoshindwa nchini Uturuki.

Erdogan anamtuhumu kiongozi wa kidini na rafikiye wa zamani, Fethullah Gulen, anayeishi Marekani, kwa kuendesha serikali mbadala. Lakini Gulen, anayeendesha jumuiya ya huduma za kijamii iitwayo Hizmet, amekanusha kuhusika na jaribio hilo, ambalo limesababisha watu 290 kuuawa, 100 kati yao wakiwa waliokula njama ya mapinduzi, na wengine zaidi ya 1,100 kujeruhiwa.

Tayari jeshi limetangaza kumalizika rasmi kwa njama hiyo ya mapinduzi, ingawa bado linabakia kwenye hali ya tahadhari, na msako ukiendelea. Mapema leo, kikosi maalum cha kupambana na ugaidi kilikivamia chuo cha kijeshi katika operesheni mpya ya kuwasaka na kuwakamata wanaoshukiwa kupanga njama ya mapinduzi hayo. Miongoni mwa viongozi wa ngazi za juu waliotiwa nguvuni, ni pamoja na Jenerali Mehmet Disli, ambaye ndiye aliyemteka nyara mkuu wa Jeshi, Hulusi Akar, siku ya Ijumaa.

Vyombo vya habari vya Uturuki vinasema jumla ya majenerali 36 wamekamatwa hadi sasa, kumi kati yao wakifikishwa mahakamani na kuamriwa kurudi kizuizini.

Erdogan ameendelea kuwataka wafuasi wake kumiminika barabarani hata baada ya kushindwa kwa jaribio hilo la mapinduzi, kwa kile anachosema ni kuonesha namna wanavyoilinda demokrasia yao. Tangu usiku wa jana takribani miji yote mikubwa ya nchi hiyo imejaa maelfu ya waandamanaji wanaomuunga mkono Erdogan.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/dpa/Reuters
Mhariri: Josephat Charo

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com