1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Diplomasia yashika kasi Ukraine

Admin.WagnerD13 Mei 2014

Ulaya imezidisha juhudi za kidiplomasia kuutatua mgogoro wa Ukraine leo, huku waziri wa mambo ya kigeni ya Ujerumani Frank-Walter Steinmeier akiushinikiza utawala mjini Kiev na waasi wa mashariki kufanya mazungumzo.

https://p.dw.com/p/1Bz0J
Waziri mkuu wa muda wa Ukraine Arsene Yatsenyuk na rais wa Halmashauri ya Ulaya Jose Manuel Barroso.
Waziri mkuu wa muda wa Ukraine Arsene Yatsenyuk na rais wa Halmashauri ya Ulaya Jose Manuel Barroso.Picha: picture alliance/AP Photo

Juhudi za waziri Steinmeier zimeanza wakati kukiwa na matumaini baada ya shirika la usalama na ushiriano la bara la Ulaya OSCE, kusema kuwa Urusi imeunga mkono mpango wake wa kuutatua mgogoro wa Ukraine kwa njia ya majadiliano, unyanganyaji silaha na uchaguzi.

Haya yanajiri baada ya waasi mashariki mwa Ukraine kuomba siku ya Jumatatu kujiunga na Urusi, kufuatia kile walichodai kuwa ni ushindi wa kishindo katika kura za maoni za uhuru. Maafisa waasi mjini Donetsk walisema asilimia 89 ya wapigakura waliunga mkono jimbo hilo kujitenga na Ukraine katika uchaguzi uliyofanyika siku ya Jumapili, wakati wanaotaka kujitenga jimboni Luhanski walisema asilimia 94 waliunga mkono uhuru.

Waziri Steinmeier akiwa na mwenzake wa Ukraine Andriy Deshchytsia mjini Kiev siku ya Jumanne.
Waziri Steinmeier akiwa na mwenzake wa Ukraine Andriy Deshchytsia mjini Kiev siku ya Jumanne.Picha: Reuters

Msisitizo wa majadiliano

Uidhinishwaji wa Urusi uliyopooza wa matokeo hayo, uliondoa hofu kwa rais Vladmir Putin kuchukuwa hatua za haraka kuyameza majimbo hayo katika shirikisho la Urusi, kama alivyofanya kwa jimbo la Crimea mapema mwaka huu.

Lakini Moscow imeendeleza shinikizo kwa serikali ya Kiev, ikisisitiza kuwa mazungumzo kuhusu haki za majimbo hayo yanapaswa kufanyika kabla ya uchaguzi wa rais wa Mei 25, na kuituhumu serikali hiyo inayoungwa mkono na mataifa ya magharibi kwa kukataa majadiliano ya kweli.

Halmashauri ya Ulaya imemkaribisha waziri mkuu wa muda wa Ukraine Arsene Yatsenyuk mjini Brussels kuonyesha uungaji wake mkono na kujadili hatua inayofuata katika jitihata za kuumaliza mgogoro ambao umeufikisha uhusiano wa mataifa magharibi katika kiwango cha chini kabisaa tangu kumalizika kwa vita baridi.

Baada ya kufanya mazunguzo na Yatsenyuk, waziri Steinmeier alisema hali nchini Ukraine inaendelea kuwa kutisha, lakini alielezea matumaini kwamba hatua zinapigwa kuutatua mgogoro huo kwa njia za amani.

Steinmeier alisema anatumai kuachiwa mara moja kwa wafungwa wote, kuyaachia majengo ya serikali na alisitiza umuhimu wa uchaguzi wa rais wa Mei 25. "Sasa hivi macho yetu yameelekezwa tarehe 25 Mei. Na natumai kuwa uchaguzi wa rais unafanyika, ili hatimaye tuweze kurejesha hali nzuri nchini Ukraine," alisema Steinmeier.

Bango la kampeni ya uchaguzi wa rais mjini Donetsk.
Bango la kampeni ya uchaguzi wa rais mjini Donetsk.Picha: DW/K. Oganesian

Urusi yaukaribisha mpango wa OSCE

Steinmeier alitarajiwa kukutana na rais wa muda Oleksander Turchynov na baadae asafiri kwenda mji wa kusini wa Odessa, katika ziara hii ambayo ililenga kuanza utekelezaji wa mpnago wa kuutatu mmgogoro huu uliopendekezwa na OSCE. Mjini Moscow, Urusi ambayo pia ni mwanachama wa OSCE, imekabirisha juhudi za shirika hilo na imezungumzia kuunga mkono mpango wake.

Wizara ya mambo ya kigeni ya Urusi imesema leo kuwa inataraji wasi wanaoiunga mkono nchi hiyo wataheshimu mpango wa OSCE ikiwa serikali ya Kiev itasitisha operesheni ya kijeshi mashariki na kuondoa wanajeshi wake. Taarifa ya wizara hiyo imesema ni muhimu kwa mpango huo kuanza kutekelezwa haraka iwezekanvyo.

Wakati huo huo, Urusi imejibu hatua ya Marekani kuiwekea vikwazo vya kiteknolojia, ambapo naibu waziri mkuu wa nchi hiyo Dmitry Rogozin, amesema kuwa Urusi itaipiga marufuku Marekani kutumia injini zilizotengenezwa nchini humo kuyatulia makombora, na pia Urusi haitarefusha mkataba ya matumizi ya kituo cha kimataifa cha angani zaidi ya mwaka 2020.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/ape,afpe.
Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman