Conservative wapiga kura ya mrithi wa Cameron | Matukio ya Kisiasa | DW | 05.07.2016
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Conservative wapiga kura ya mrithi wa Cameron

Mchakato huo wa Kura unafanyika wakati ukiongezeka wasiwasi kuhusu taathira za kiuchumi baada ya Uingereza kujitoa katika Umoja wa Ulaya. Sarafu ya pauni imeporomoka kiwango ambacho hakijapata kutokea kwa miaka 31.

Waziri mkuu Cameron akizungumza bunge 27 Juni.2016

Waziri mkuu Cameron akizungumza bunge 27 Juni.2016

Wasiwasi kuhusu taathira za kiuchumi baada ya Uingereza kujitoa katika Umoja wa Ulaya zinaipiga sekta ya biashara ya majumba pamoja na kuiporomosha thamani ya sarafu ya pauni katika kiwango ambacho hakijapata kutokea kwa miaka 31. Athari hizo zinajitokeza wakati ambapo wanachama wa chama tawala cha Conservative wameanza mchakato wa kupiga kura kumchagua waziri mkuu mpya.

Waziri wa mambo ya ndani Theresa May na Andrea Leadsom ambaye ni naibu waziri wa nishati ni wagombea wenye nafasi nzuri ya kumrithi waziri mkuu wa sasa aliyetangaza kujiuzulu David Cameron. Mchakato wa taratibu za kuanza mipango ya kujiondoa utakwenda hadi mwezi Septemba lakini dalili zinazidi kuonekana kwamba wasiwasi uliopo kuhusu taathira za kura ya Brexit katika biashara,uwekezaji na imani katika masoko ya biashara tayari yameanza kuumiza uchumi wa taifa hilo.'

Waingereza waliounga mkono Brexit

Waingereza waliounga mkono Brexit

Kampuni la uwekezaji la Aviva limesema limesimamisha biashara zake nchini Uingereza kwasababu ya hali iliyopo kwenye masoko,hatua ambayo imekuja siku moja tu baada ya kampuni la uwekezaji la Standard Life Investment kuchukua hatua kama hiyo iliyosababishwa na wawekezaji kuzihamisha fedha zao.Hisa zimeporomoka katika makampuni mengine pia ya sekta ya biashara ya majumba huku wafanyabiashara wakubwa wanaosimamia mali hizo na makampuni ya bima yakipata pigo.

Wafanyabiashara wa maduka pia kama John Lewis wanasema kiwango cha mauzo katika maduka yake kimeshuka katika kipindi cha wiki baada ya Uingereza kujitowa kutoka Umoja wa Ulaya,ingawa data za mauzo hayo zilikuwa zimefunikwa na taathira ya punguzo la bei la msimu wa joto pamoja na tafauti ya kila mwaka ya hali ya hewa.Sarafu ya Uingereza Pauni inatia mashaka kwa wafanyabiashara wengi hasa kuhusiana na uwezekano wa kusababisha kuporomosha uchumi wa nchi.Sarafu hiyo imeteremka thamani yake kwa kiasi ambacho hakijapata kutokea tangu mwaka 1985 na kwahivi sasa imeporomoka thamani kwa asilimia takriban 12.

Waziri wa ndani Theresa May na David Cameron

Waziri wa ndani Theresa May na David Cameron

Benki ya England imesema kwamba hali ya hivi sasa ya thabiti wa masoko ya fedha Uingereza ni changamoto ingawa pia benki hiyo imetangaza mipango ya kuzitia moyo benki kuendelea kukopesha.

Lakini pamoja na hayo wapiga kura wa Uingereza walionywa mara chungunzima kabla hata ya kura ya maoni ya Brexit ikiwemo na waziri mkuu David Cameron pamoja na taasisi za fedha na mashirika ya wasomi kwamba kura ya kujitoa katika Umoja wa Ulaya itaifanya nchi hiyo kujitumbukiza yenyewe katika mporomoko wa kiuchumi kwa kuharibu nafasi yake ya kuingia katika soko huru la pamoja bila ushuru.

Lakini walioendesha kampeini za kutaka nchi hiyo ijitoe katika Umoja wa Ulaya walidai kwamba kwauli hizo ni mpango wa kujenga khofu kwa wapiga kura wakitoa hoja zao kwamba Uingereza itakuwa bora na yenye maendeleo makubwa zaidi kwa kujitoa katika Umoja huo unaoendeshwa kutokea Brussels.Walitoa hoja kwamba Uingereza itakuwa na uwezo wa kujitungia sheria zake yenyewe na kuingia katika mikataba ya kibiashara itakayokuwa na manufaa kwake kama nchi pamoja na kulidhibiti suala na uhamiaji jambo ambalo haiwezi kulifanya ikiwa chini ya sheria za Umoja wa Ulaya ambazo zinasisitiza kuhusu uhuru wa kutembea wa wananchi wake katika kanda hiyo.

Wabunge wa chama cha Conservative wameanza kupiga kura katika duru ya mwanzo ambayo itafuatiwa na msururu wa duru nyingine za kupiga kura kuwachuja wagombea watano wanaowania kumrithi Cameron.Theresa Maya ambaye amekuwa akiendesha wizara inayosimamia usalama na sheria kwa miaka 6 chini ya serikali ya Cameron yuko katika nafasi nzuri akiungwa mkono na wabunge wengi.

Mpinzani wake Leadsom mwenye umri wa miaka 53 hana tajriba ya kuwa waziri lakini ana kitu kimoja kinachoweza kumsaidia,amekuwa katika upande uliopata ushindi kwenye kura ya Brexit.Pia ameungwa mkono wiki iliyopita na meya wa zamani wa London Boris Johnson ambaye alikuwa msitari wa mbele katika kuongoza kampeini ya Uingereza kujitoa katika Umoja wa Ulaya.Ikiwa ni May au Leadsom atakayechaguliwa inamaana kwamba Uingereza kwa mara ya pili itakuwa na waziri mkuu mwanamke baada ya Margaret Thatcher.

Mwandishi: Saumu Mwasimba

Mhariri: Mohammed Khelef

DW inapendekeza

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com