1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

China,Ufaransa zaujia juu muungano wa Indo-Pacific

Angela Mdungu
16 Septemba 2021

China imelaani muungano mpya wa kiusalama wa kimkakati uliotangazwa jana Jumatano na viongozi wa Marekani, Australia na Uingereza

https://p.dw.com/p/40PZa
USA I Washington I Präsident Joe Biden
Picha: Andrew Harnik/abaca/picture alliance

 Muungano huo uliokosolewa pia na Ufaransa unakusudia kuendesha ushirikiano unaojulikana kama AUKUS, utakaoziruhusu nchi husika kushirikiana katika teknolojia katika masuala ya usalama wa mtandao, teknolojia ya akili bandia (AI) mifumo ya majini, pamoja na mashambulizi ya masafa ya mbali

Kauli ya China iliyotolewa mjini Beijing na msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni wa China Zhao Lijian kuhusu ushirikiano mpya wa kimkakati kuhusu masuala ya ulinzi kati ya  Marekani, Uingereza na Australia imesema, nchi hizo zinapaswa kuachana na mtazamo huo wa vita baridi wenye lengo la kunufaisha upande mmoja na kusababishia hasara upande wa pili.

Msemaji huyo wa wizara ya mambo ya kigeni wa China aliongeza kuwa, Australia siyo taifa linalozalisha silaha za nyuklia, lakini ghafla  sasa litaanza kuingiza manowari za kivita zinazoendeshwa kwa nguvu za nyuklia, ameongeza kuwa huenda kufanya hivyo kukayafanya mataifa mengine katika jumuiya ya kimataifa kuhoji majukumu ya nchi hizo katika kudhibiti silaha za nyuklia.

Ufaransa nayo yakasirishwa

Kwa upande wake Ufaransa, imekasirishwa na hatua ya Australia kununua teknolojia ya manowari za nyuklia kutoka Marekani na kuachana na mkataba iliyoingia na Ufaransa wenye thamani ya euro bilioni 56 wa kuipatia manowari za kawaida.

Hata hivyo awali, waziri mkuu wa Uingereza Boris Johnson alipokuwa akizungumzia ushirikiano huo mpya aliutetea akisema kuwa haulengi kuleta uhasama kwa taifa jingine lolote, bali unaakisi tu uhusiano wa karibu iliyonao Uingereza, Marekani na Australia na kiwango kikubwa cha kuaminiana baina ya washirika hao.

London, UK | Kabinettsumbildung | Parlament | Boris Johnson
Waziri mkuu wa Uingereza Boris JohnsonPicha: Reuters

Naye Rais wa Marekani Joe Biden amesema  ushirikiano huo wa ulinzi , AUKUS utadumisha utangamano katika kukabiliana na vitisho vya kiusalama kwenye karne 21 kama walivyofanya pamoja katika karne ya 20.

Katika hatua nyingine, mkuu  wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya  Josep Borell amesema, Umoja huo haukufahamishwa kuhusu ushirikiano mpya wa kiusalama wa mataifa hayo matatu. Borell anasema, watajadiliana na nchi hizo washirika ili kutathmini athari zake.