1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

China: Mgogoro wa Afghanistan na Pakistan unatupa wasiwasi

Amina Abubakar ap, reuters
13 Oktoba 2025

Wizara ya mambo ya nje ya China imesema taifa hilo lina wasiwasi kuhusu mzozo wa hivi karibuni kati ya Pakistan na Afghanistan na kutoa wito kwa mataifa hayo mawili kuwalinda raia wake na uwekezaji.

https://p.dw.com/p/51u2f
China | Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya China Lin Jian
China yasema ina wasiwasi kuhuuu mgogoro kati ya Afghanistan na PakistanPicha: Ichiro Ohara/Yomiuri Shimbun/AP Photo/picture alliance

Wapiganaji kadhaa waliouwawa katika mapigano ya usiku kucha katika maeneo ya mpakani mwa Pakistan na Afghanistan. Mapigano hayo yamesemakana kuwa mabaya kati ya jirani hao wawili tangu Kundi la Taliban lilipochukua udhibiti nchini Afghanistan. 

China inapakana na Afghanistan na Pakistan katika eneo lake la Magharibi na imeamua kuchukua jukumu la upatanishi na kutuliza uhasama kati ya pande hizo mbili ambao walikuwa washirika wakubwa kabla ya ushirika wao kuingia doa katika siku za hivi karibuni.

China yatoa wito wa mshikamano

"China iko tayari kuchukua jukumu la kuimarisha na kuendeleza mahusiano ya Pakistan na Aghanistan" alisema msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya China Lin Jian wakati walipozungumza na vyombo vya habari.  Amesema anatumai mataifa hayo yatavumiliana na kutatua tofauti zao kupitia mazungumzo huku zikijiweka kando na matendo yatakayochochea ghasia zaidi. 

Msemaji mkuu wa serikali ya Taliban, Zabihullah Mujahid.
Utawala wa Taliban wasema Pakistan imekuwa mara kwa mara anga yake Picha: Xinhua /imago images

Mwezi Agosti, Waziri wa mambo ya nje wa China Wang Yi alishiriki mkutano na wenzake wa  Pakistani na Afghan mjini Kabul  akitoa wito wa mshikamano. Na katika mkutano mwengine uliofanyika wiki tatu kabla ya mkutano huo wa hivi karibuni China ilisema mataifa hayo hasimu yalikubaliana kuimarisha mahusiano yao ya kidiplomasia. 

Pakistan yasema matendo ya Afhanistan ni ya kichokozi

Lakini huku hayo yakiarifiwa jana Jumapili (12.10.2025), Waziri Mkuu wa Pakistan Shehbaz Sharif alilaani kitendo alichokiita ni cha uchokozi kutoka nchi jirani ya Afghanistan, akisisitiza kwamba nchi yake itajibu vikali baada ya pande hizo mbili kushambuliana usiku kucha katika eneo la mpakani.

Makabiliano hayo yalianza siku ya Jumamosi usiku  wakati vikosi vya Afghanistan kushambulia ngome kadhaa za kijeshi za Pakistan  na kusababisha mauaji ya wanajeshi 58 wa Pakistan huku wengine zaidi ya 30 wakijeruhiwa. 

Msemaji mkuu wa serikali ya Taliban, Zabihullah Mujahid, alisema vikosi vya Afghanistan sasa vinadhibiti vituo 25 vya jeshi la Pakistan. Amesema operesheni ni majibu ya ukiukaji wa mara kwa mara kwenye anga yake unaofanywa na Pakistan. Pakistan kwa upande wake imesema idadi ya wanajeshi wake waliouwawa ni 23 na sio 58 kama Afghan inavyodai. Imesema pia imewauwa wapiganaji zaidi ya 200 wa Taliban na washirika wake wa kigaidi. 

Afghanistan imekuwa ikiilaumu Pakistan kwa kuushambulia kwa mabomu mji mkuu, Kabul, na soko la mashariki mwa nchi hiyo.

Mashambulizi hayo makali yamesababisha mpaka kati ya pande hizo mbili kufungwa kwa siku ya pili mfululizo na kuathiri pakubwa biashara.

Mataifa mengi ya kigeni ikiwemo Saudi Arabia, yameomba nchi hizo hasimu kuacha mara moja kushambuliana.